Watano kushtakiwa nchini Uingereza kwa kuipelelezea Urusi

Chanzo cha picha, BBC/LINKEDIN/BISER
Watu watano wanaoshukiwa kufanya ujasusi kwa ajili ya Urusi watafunguliwa mashtaka ya kula njama ya kufanya ujasusi nchini Uingereza.
Orlin Roussev, Bizer Dzhambazov, Katrin Ivanova, Ivan Stoyanov, na Vanya Gaberova watafikishwa katika Mahakama ya Westminster siku ya Jumanne.
Raia hao wa Bulgaria wanadaiwa kula njama ya kukusanya taarifa ambazo zingemfaa adui kati ya Agosti 2020 na Februari 2023.
Ni kufuatia uchunguzi wa Polisi wa Metropolitan - wanashutumiwa kwa kufanya ujasusi nchini Uingereza na Ulaya na kukusanya na kupitisha habari kwa ajili ya Urusi.
Roussev, 45, anadaiwa kuendesha oparesheni nchini Uingereza na kuwa kiungo wa wale waliopokea taarifa hizo za kijasusi.
Maafisa waliopekua makaazi ya watuhumiwa watatu Roussev, Dzhambazov, 41, na Bi Ivanova, 31, huko London na Norfolk - walipata hati za kusafiria zinazodaiwa kuwa bandia na hati za utambulisho za Uingereza, Bulgaria, Ufaransa, Italia, Uhispania, Croatia, Slovenia, Ugiriki, na Jamhuri ya Cheki.
Baadhi ya hati hizo zilikuwa na picha za Roussev na Bw Dzhambazov.
Kundi hilo pia linashutumiwa kwa kuandaa operesheni ya ujajusi huko Montenegro, Canada iliyohusisha utengenezaji wa vitambulisho ghushi vya wanahabari, kikiwemo kimoja chenye sura ya Ivanova.



















