'Nilikuwa mwanasoka tajiri na mraibu wa kamari'

j

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Dean Sturridge alitumia misimu kadhaa kuichezea Wolves
    • Author, Kath Stanczyszyn & Gavin Kermack
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 3

Dean Sturridge, mzaliwa wa Birmingham, alikuwa mshambuliaji mwenye mafanikio, haswa alipokuwa akicheza Ligi Kuu ya England, katika timu ya Derby County, Leicester City na Wolverhampton Wanderers, na pia aliwahi kuichezea Sheffield United na Kidderminster Harriers.

Lakini nyuma ya pazia, alikuwa akipambana na uraibu mkubwa wa kucheza kamari. Baada ya kupona, Sturridge anatumia uzoefu wake kuwasaidia wengine waliokwama kwenye uraibu.

Pia unaweza kusoma
j

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Sturridge, pichani kushoto akiwa na wachezaji wenzake Robin Van Der Laan na Gary Rowett, wakiwa Derby County.

Sturridge ni balozi mpya wa shirika la usaidizi dhidi ya kamari la Gordon Moody, ambalo lipo Uingereza tangu mwaka 1971, likitokea nchini Marekani.

"Ninajua hisia ya kuwa katika uraibu, kuwa mpweke, kutengwa, kuhisi hatia, kuhisi aibu, kuhisi fedheha," anasema Sturridge, ambaye sasa ana umri wa miaka 51. "Kisa cha kila mtu ni cha kipekee, lakini natumai nitaweza kumhamasisha japo mtu mmoja ili aache kamari."

Tatizo la Sturridge la kucheza kamari lilianza alipokuwa mdogo lakini lilizidi kuwa baya alipokuwa maarufu na bahati ya kuwa mwanasoka wa kulipwa. Anasalia kuwa mfungaji bora wa Derby County kwenye Ligi Kuu ya England.

"Malipo yangu ya kwanza ya kusaini yalikuwa ya kiwango kikubwa," anaeleza. "Pesa hiyo ilipaswa kununua gari langu la kwanza, Ford Fiesta Firefly.

"Lakini sikuweza kulinunua kwa sababu nilipoteza pesa hiyo ya kusaini ndani ya saa chache baada ya kuingia kwenye akaunti yangu."

Sturridge aliishia kukopa pesa kutoka kwa mchezaji mwenzake ili kulipia gari.

"Nilikuwa nikienda benki...nikiandika hundi na kisha kutoa pesa. Mwisho wa siku unaona ziro kwenye akaunti yako, wakati mwanzoni mwa siku ilikuwa na maelfu ya pesa."

jn

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Sturridge, pichani akiichezea Leicester City

Sturridge anasema mshahara wake ulimruhusu kufadhili uraibu wake - lakini aliona athari katika maeneo mengine.

"Nilipokuwa na watoto wangu [na mke wangu], baadhi ya wakati ningekuwa kwenye simu yangu nikicheza kamari," anakumbuka. "Sikuwepo nao kwenye mazungumzo.

"Na hilo ndilo jambo la kukatisha tamaa zaidi kwangu ambalo ninajutia. Lakini nina furaha sasa kwamba nimepata nafuu, ni mtu bora sasa.

"Na nina muda wa kutosha sasa na mjukuu wangu, ambaye ana umri wa mwaka mmoja, na naweza kumuonyesha Dean mpya aliyebora."

Mambo yalibadilika siku moja, pale mke wa Sturridge alipofika nyumbani mapema na kumkuta akitazama mbio za farasi na kucheza kamari. Ndani ya saa 24, alikuwa kwenye mkutano na Gordon Moody.

"Mwanzo ilikuwa ni ngumu. Kama mcheza kamari, kila mara nilikuwa nikisukuma hisia zangu kando na kujaribu kuzificha."

kn

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Sturridge sasa anafanya kazi kama wakala wa soka

Sasa ni wakala wa soka, Sturridge anaamini wachezaji wachanga wameandaliwa zaidi kukabiliana na mitego ya umaarufu - ingawa anasisitiza kuwa bado wanahitaji kuungwa mkono.

"Ni muhimu... kwa watu kama mimi, kwa watu kutoka mashirika kama Gordon Moody, kwenda shuleni na katika vilabu vya soka na kuwasaidia vijana katika safari zao."