Wanawake wanaocheza Kamari: 'Siku nilioshinda pauni 127,000, ndiyo siku mbaya zaidi maishani mwangu'

Chanzo cha picha, LISA
Kampeni ya uhamasishaji inazinduliwa ili kusaidia takriban wanawake milioni moja nchini Uingereza walio katika hatari ya kucheza kamari ya kuwaathiri.
Shirika la kutoa misaada la Gamble Aware linasema wengine huenda wasitambue dalili za onyo au wanaona aibu na kunyanyapaliwa wanapotafuta usaidizi.
Makadirio hayo yanatoka katika kura ya maoni iliyowakilisha kitaifa ya YouGov ya wanawake 9,649, kwa kutumia mfumo kwa jina Problem Gambling Severity Index - kupima madhara ya kucheza kamari.
Inapendekeza kuwa huenda watu nusu milioni wako kwenye shughuli hiyo .
Kampeni itaendelea hadi Machi katika vituo vya televisheni, kijamii na dijitali.
Lisa Walker, 49, kutoka Rainham mashariki mwa London, alipambana na uraibu kucheza kamari kwa zaidi ya muongo mmoja. Tabia yake iliongezeka mwishoni mwa umri wa miaka yake ya 20, baada ya kushinda kiasi kikubwa cha pesa akicheza kamari.
"Nilishinda zaidi ya pauni 127,000 kwa usiku mmoja. Huo ulikuwa usiku mbaya zaidi maishani mwangu kwa sababu hapo ndipo uraibu wangu ulianza kukosa kudhibitiwa.
"Kasino ilinitaka nirudi na walinipa chochote nilichotaka - vinywaji vya bure, milo ya bure ili kunishawishi."
"Siku nyingi nilifikiria kuhusu kucheza kamari na siku nyingi nilicheza. Ilifikia hatua ambayo sikuwa na thamani yoyote ya pesa tena."
Hatimaye, alipoteza pesa zake zote alizoshinda, pamoja na nyumba yake, baada ya kuweka rehani nyumba yake ili kuendelea kucheza kamari.
Aliishia kukaa katika hosteli kwa muda na watoto wake wawili, ambao walikuwa 10 na 11 wakati huo.
Zaidi juu ya uraibu wa kamari
Katika miaka 45, uraibu wa Lisa uliendelea. Hata alichagua kuolewa na mpenzi wake katika ukumbi mmoja huko Vegas - kisha akatumia usiku wa harusi yake kucheza kamari kwenye kasino badala ya kusherehekea na bwana harusi na wageni wake.
Aliporudi kutoka Vegas, Lisa alitambua kwamba alihitaji msaada, kwani kucheza kamari kulikuwa kumempeleka kwenye "mahali pa kina penye giza" ambapo hangeweza kufikiria kitu chochote kingine.
Lisa aliamua kuhudhuria mkutano kwa jina 'Gamblers Anonymous', ambapo alikuwa mmoja wa wanawake wawili kati ya wanaume 35. Sasa anahudhuria mikutano kila juma na anaanza kuona wanawake wengi zaidi wakija kwenye mikutano.
Lisa yuko katika hali ya kupata nafuu. Anasema kucheza kamari mtandaoni ni njia mpya ambayo watu wananaswa.
"Tunaona watu wengi wakiingia mtandaoni. Una simu ya mkononi ya saa 24 na kasino ya saa 24 mfukoni mwako na ndani ya dakika chache unaweza kucheza kamari mtandaoni."
Liz Karter, mtaalamu wa uraibu wa kucheza kamari na mshauri wa uraibu wa kucheza kamari, anasema hivi: "Tabia za kucheza kamari hujidhihirisha kwa njia tofauti kwa wanawake kuliko wanaume.
"Kwa mfano, tunajua upatikanaji rahisi wa kamari ya mtandaoni hupelekea wanawake wengi kwenye michezo ambayo inaonekana kuwa haina hatia na kukubalika kijamii. Michezo inaonekana kuwa salama na inayofahamika, kwani inafanana sana na michezo ya kidijitali ya kucheza bila malipo ambayo sote tumezoea kucheza sasa.
"Kwa kuongezea, matumaini ya kupata faida ya kifedha yanaweza kuwa kichocheo chenye nguvu. Ingawa kamari haileti madhara kila wakati, ni muhimu wanawake watambue dalili za mapema ikiwa ni pamoja na kupoteza muda, kuongeza deni, au tabia ya kuficha kamari kutoka kwa wengine au kucheza kamari ili kusahau matatizo yao."
Daktari Ellie Cannon anasema dalili za onyo za madhara ya kucheza kamari ni pamoja na:
- -kuweka kamari zaidi ya unavyoweza kumudu
- -kukopa ili kucheza kamari
- -kupoteza uwezo wa kufuatialia wakati
- -kuhisi wasiwasi au hatia kwa sababu yake
- -kutunza siri yako ya kamari kutoka kwa wale walio karibu nawe
Msemaji wa Tume ya Kamari, shirika la serikali linalodhibiti uchezaji kamari nchini Uingereza, anasema: "Kampeni kama hizi ni muhimu sana katika kukuza ufahamu wa hatari za madhara ya kucheza kamari.
"Tunaunga mkono mpango wowote unaotoa usaidizi na ushauri ili kuwasaidia wale wanaocheza kamari kufanya hivyo kwa njia salama. Pamoja na mahitaji yetu madhubuti ya udhibiti kwenye kampuni za kamari, ina jukumu muhimu katika kuzuia na kupunguza madhara yanayohusiana na kamari."












