Ipi tofauti ya Sunni na Shia na nafasi zao katika migogoro ya Mashariki ya Kati?

sdxc

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kiongozi wa kidini wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei (kushoto), na Mwana Mfalme wa Saudi Arabia, Mohamed bin Salman

Madhehebu makubwa katika ulimwengu wa Kiislamu ni Sunni na Shia. Tofauti kati ya matawi hayo mawili ya Uislamu ni ukumbusho wa wazi juu ya uhusiano tata kati ya wapinzani wawili wa Mashariki ya Kati; Saudi Arabia na Iran .

Nchi hizo ziko katika mapambano ya utawala wa kikanda na mivutano ya wawili hao kwa miongo kadhaa inachochewa na mgawanyiko wa kidini.

Iran ina idadi kubwa ya Waislamu wa Shia, wakati Saudi Arabia ni Waislamu wa Sunni.

Katika mgawanyiko wa Sunni na Shia, Hamas ni kundi la ki-Sunni lakini ni mshirika wa Iran kwa miongo kadhaa, ikitoa msaada wa kifedha na kijeshi kwa kundi hilo ili kupambana na Israel adui wa Iran.

Tangu kuanza kwa vita vinavyoendelea Gaza, makundi mengine ya Mashariki ya Kati yaliofanya mashambulizi dhidi ya Israel na yanayounga mkono Hamas ni kundi la Lebanon la Hezbollah na Houthis wa Yemen, makundi haya mawili ya Kishia - pia ni washirika wa Tehran..

Saudia imekuwa na mazungumzo ya kuwa na uhusiano bora na Israel na mmoja wa wanachama wa nyumba ya kifalme ya Saudi Arabia, Prince Turki al Faisal, ameikosoa Israel na Hamas kwa mashambulizi dhidi ya raia.

Historia ya Sunni na Shia

AS

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Wafuasi wa itikadi kali wa Kisunni, kama vile Taliban - nchini Pakistan na Afghanistan, walishambulia mara nyingi maeneo ya ibada ya Mashia

Mgawanyiko kati ya Sunni na Shia ulianza mwaka 632 baada ya kifo cha Mtume Muhammad, ambacho kilisababisha mvutano kuhusu mwenye haki ya kuwaongoza Waislamu – mvutano ambao unaendelea hadi leo.

Ingawa madhehebu yote mawili yameishi pamoja kwa karne nyingi, yanafanana mambo mengi katika imani na desturi. Lakini pia yana tofauti katika masuala ya mafundisho, ibada, sharia na uongozi.

Kutoka Syria hadi Lebanon, kupitia Iraq na Pakistan, migogoro mingi ya hivi karibuni imezidisha mgawanyiko katika madhebu hayo.

Sunni ni nani?

asx

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mwana Mfalme wa Saudi Arabia, Mohamed bin Salman.

Wasunni ndio wengi kati ya Waislamu - inakadiriwa kuwa takribani 90% ya Waislamu ni Sunni. Jina la Sunni linatokana na neno ‘Ahl al-Sunna,’ watu wa suna.

Suna ni matendo na mafundisho yanayotokana na Mtume Muhammad na maswahaba zake. Sunni wanawaheshimu manabii wote waliotajwa katika Quran, hasa Mtume Muhammad, ambaye wanaamini ndiye Nabii wa mwisho.

Katika historia ya Mashariki ya Kati wanazuoni na viongozi wa kisuni wamekuwa wakidhibitiwa na serikali.

Na mafundisho ya wanazuoni wa Sunni, ambayo ni mengi nchini Saudi Arabia, chini ya mfumo wa sheria za Kiislamu, hutokana na wanazuoni wakubwa wanne wa kisuni.

Shia ni nani?

sxc

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Idadi kubwa ya Mashia wako katika nchi ya Iran
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mashia walianza kama kundi la kisiasa "Shiat Ali" au kundi la Ali.

Ali alikuwa ni mkwe wa Mtume Muhammad na Mashia wanadai haki yake, na ya kizazi chake, kuwaongoza Waislamu.

Ali aliuawa kutokana na fitina, vurugu na vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo viliukumba ukhalifa wake.

Na wanawe, Hassan na Hussein, walinyimwa kile kinachoonekana na Washia haki yao ya kumrithi.

Hassan inaaminika alilishwa sumu na Mu'awiyah - kiongozi wa Waislamu wa nasaba ya Umayya, wakati kaka yake Hussein alikufa, pamoja na watu kadhaa wa familia yake, kwenye uwanja wa vita.

Matukio haya ndio msingi wa imani ya Mashia kuhusu kifo cha kishahidi na mila zao za maombolezo.

Mashia wana daraja la maulama wanaotekeleza tafsiri ya maandiko ya Kiislamu. Inakadiriwa kwamba Mashia kwa sasa wanafikia wafuasi kati ya milioni 120 a 170, mmoja kati ya Waislamu kumi ni mshia.

Idadi kubwa ya Mashia iko nchini Iran, Iraq, Bahrain, Azerbaijan na kwa uchache nchini Yemen.

Lakini pia kuna jumuiya kubwa za Mashia nchini Afghanistan, India, Kuwait, Lebanon, Pakistan, Qatar, Syria, Uturuki, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu.

Madhehebu haya na migogoro ya kisiasa

w

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Baadhi ya migogoro ya Mashariki ya Kati iko katika sura ya Sunni na Shia

Katika baadhi ya nchi zenye viongozi Massuni, Mashia wanajiona kama wahanga wa ukandamizaji na ubaguzi. Na baadhi ya Wasunni wenye msimamo mkali hufikia hatua ya kuhubiri chuki dhidi ya Mashia.

Mfano kwa miaka mingi wafuasi wa itikadi kali wa Kisunni, kama vile Taliban - nchini Pakistan na Afghanistan, walishambulia mara nyingi maeneo ya ibada ya Kishia.

Mapinduzi ya Iran ya 1979, yalizindua ajenda ya Uislamu wa mwelekeo wa Kishia – mapinduzi hayo yametoa changamoto kwa serikali za kihafidhina za Kisunni, haswa katika Ghuba ya Uajemi.

Na sera ya Tehran ya kuviunga mkono vyama na wanamgambo wa Kishia nje ya mipaka yake - inapingwa na mataifa ya Ghuba yenye Waislamu wengi wa Kisunni.

Wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Lebanon, Washia walipata umaarufu kutokana na shughuli za kijeshi za Hezbollah .

Mizozo ya nchini Iraq na Syria pia ilichukua sura ya madhehebu. Vijana wengi wa Kisunni walijiunga na vikundi vya waasi kupigana na Marekani hadi kuzaliwa dola la kiislamu, kundi la ki-Sunni.

Nchini Syria makundi ya kishia yanapigana upande wa serikali ya nchi hiyo ili kumuunga mkono Bashar Al Asad ambaye ni Mshia. Na makundi hayo yamesaidia pakubwa utawala wake kuendelea kuwa madarakani.

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Seif Abdalla