Je, ni makundi gani tiifu kwa Iran nchini Iraq na Syria?

Chanzo cha picha, REUTERS
Siku ya Ijumaa, Marekani ilifanya mashambulizi ya anga kwenye kambi mbili zinazotumiwa na jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran kuhifadhi silaha katika mji wa Albukamal mashariki mwa Syria.
Haya yanajiri baada ya vikosi vya Marekani na vikosi vya muungano wa kimataifa kukabiliwa na mashambulizi yasiyopungua 12 nchini Iraq na mashambulizi manne nchini Syria tangu kuzuka kwa vita kati ya Israel na Hamas.
Makundi ya Kishia hufanya mashambulizi dhidi ya vikosi vya muungano wa kimataifa vinayoongozwa na Marekani, kwa maslahi ya serikali ya Syria na Iran.
Kikosi cha Quds

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Kikosi cha Quds kipo chini ya jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran, na kinafanya kazi nyeti nje ya Iran, kwa kutoa silaha na mafunzo kwa vikundi vilivyo karibu na Iran, kama vile Hizbullah ya Lebanon na vikundi vya Kishia huko Iraq ambavyo vimeibuka tangu uvamizi wa Marekani nchini Iraq mwaka 2003.
Kikosi hiki kilianzishwa na kamanda wake marehemu, Qassem Soleimani (aliyeuawa katika shambulizi la droni ya Marekani karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad - Januari 2020)"
Soleimani alijenga mtandao mpana wa mahusiano katika eneo hilo kuanzia Yemen hadi Syria, Iraq na nchi nyingine, na akawa kiungo muhimu cha ushawishi wa Iran katika nchi hizi.
Quds ililipigana vita pamoja na wapiganaji wa Kishia nchini Syria na Iraq dhidi ya Dola la Kiislamu na dhidi ya makundi ya upinzani nchini Syria.
Hizbullah ya Lebanon

Chanzo cha picha, ALAMY
Hezbollah ni taasisi ya kisiasa, kijeshi, na kijamii ambayo ina ushawishi mkubwa miongoni mwa jamii ya shia nchini Lebanon.
Inaungwa mkono na Iran na iliibuka wakati Israel ilipokalia kwa mabavu kusini mwa Lebanon mwaka 1982. Hizbullah haifichi ukaribu wake na Iran.
Baada ya jeshi la Israel kuondoka kusini mwa Lebanon mwaka 2000, Hezbullah ilikataa kusalimisha silaha zake, na iliendelea kuimarisha tawi lake la kijeshi. Uwezo wake wa kijeshi unazidi Jeshi la Lebanon.
Vita viliposhika kasi nchini Syria, maelfu ya wanachama wa Hezbollah walipigana pamoja na jeshi la Syria, na wanamgambo hao walifanya kazi kubwa ya kurejesha ardhi ambazo zilidhibitiwa na makundi ya upinzani.
Hizbullah ya Iraq
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kundi hili la "Hezbollah" lilihusishwa na Hezbollah ya Lebanon, lakini kuna kundi jingine liliibuka zaidi ya miongo miwili baada ya 1982 ambalo ni Brigedi ya Hezbollah ya Iraq lakini ni kundi tofauti na lile la Lebanon.
Kundi hili lilianzishwa mwaka 2007, katika mji wa Amara, kusini mwa Iraq. Vikosi vyake viliundwa kutokana na vikundi kadhaa vya Washia wenye silaha.
Baadhi ya vikundi hivyo viliibuka baada ya uvamizi wa Marekani huko Iraq 2003. Kundi hili linaundwa na makundi ya Abu al-Fadl al-Abbas, Karbala, Zaid bin Ali, Ali al-Akbar, na al-Sajjad.
Makundi ya Hizbullah Iraq yanasema yanafanya kazi ya kukwamisha kile wanachokiita mradi wa Marekani na Israel katika Mashariki ya Kati, na wanachama wao walikuwa miongoni mwa wanamgambo wa kwanza kupigana nchini Syria pamoja na vikosi vya serikali baada ya wimbi la maandamano ya wananchi yaliyoikumba nchi hiyo mwaka 2011.
Hezbollah haina muundo wa kiserikali unaojulikana, kama ilivyo kwa makundi mengine makubwa ya kishia nchini Iraq. Hakuna Mkuu wa Hezbollah aliyetangazwa ila kuna uteuzi wa wasemaji kwa niaba ya kundi kwa upande wa kijeshi na kiraia.
Idadi ya wanamgambo wake inakadiriwa kufikia elfu saba, kulingana na takwimu zisizo rasmi. Mafunzo yake yanasimamiwa na a Iran na makundi ya Lebanon, haswa Imad Mughniyeh, aliyeuawa Syria 2015.
Brigedi zake zinatajwa na Marekani kuwa ni za kigaidi, zilifanya operesheni nyingi dhidi ya wanajeshi wa Marekani nchini Iraq.
Ripoti pia zinaeleza kuwa Brigedi hizo zilikuwa sehemu ya kutekwa nyara kwa timu ya wavuvi wa Qatar Disemba 2015 kusini mwa Iraq, wakapokea dola bilioni moja za kikombozi zilizolipwa na Qatar. Lakini Qatar ilisema ililipa pesa hizo kwa serikali ya Iraq.
Harakati ya Al-Nujaba

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Harakati hiyo ilishirikiana na Brigedi za Hizbullah katika vita vya Syria hasa katika mji wa Aleppo mwaka 2015, na kuna maelezo kwamba kundi hilo lina mfungamano na Kikosi cha Quds.
Ushahidi unaonyesha Iran ndiyo inayoipatia fedha na silaha, taarifa za kijasusi, na kuisaidia kuchagua viongozi wake. Harakati hiyo ina uhusiano wa karibu na vikundi vinavyounga mkono Iran.
Mwanzilishi wa vuguvugu hilo, Akram al-Kaabi, alikuwa kamanda mashuhuri katika "Jeshi la Mahdi" la kiongozi wa kidini wa Kishia wa Iraq, Muqtada al-Sadr kabla ya kuondoka.
Al-Kaabi alijiunga na Asaib Ahl al-Haq, kundi lililoanzishwa na Kikosi cha Quds 2008. 2019 Marekani ilimuweka Al-Kaabi kwenye orodha ya "magaidi wa kimataifa."
Novemba 4, 2015, Al-Kaabi aliiambia idhaa moja ya Iraq "ataitikia amri yoyote itayotolewa na Kiongozi Mkuu wa Iran Ali Khamenei, ikiwa ni pamoja na kupindua serikali ya Iraq au kupigana katika vita vyovyote."
Mapema mwezi Machi 2017, kundi hilo lilitangaza kupitia shirika la habari la Iran la Tasnim liko katika mchakato wa kuunda kikosi cha Ukombozi wa Golan, ili kuikomboa kutoka udhibiti wa Israel.
Kundi la Asaib Ahl al-Haq

Chanzo cha picha, REUTERS
Kundi la Asaib Ahl al-Haq, liliibuka kupinga uvamizi wa Marekani, na walidai kuhusika na mashambulizi mengi dhidi ya majeshi ya Marekani na Iraq.
Kiongozi mashuhuri wa Asaib ni Qais Khazali, alijitoa katika Jeshi la Mahdi mwaka 2004, mwaka mmoja baada ya uvamizi wa Marekani - baada ya Jeshi la Mahdi kusaini makubaliano ya kusitisha mapigano na serikali ya Iraq na jeshi la Marekani.
Harakati hiyo inayoungwa mkono na Kikosi cha Quds na kupewa mafunzo na uungaji mkono kutoka Iran, imepanuka na kuijumuisha Syria, ambako imewatuma wanachama wake kupigana.
Mbali na makundi hayo kuna makundi mengine ya wana mgambo nchini Iraq kama vile Brigedi za Abu al-Fadl al-Abbas, Brigedia ya Badr, na wanamgambo wengine wanaofadhiliwa na serikali ya Iraq kupitia muungao wa Popular Mobilization Forces. Wengine ni wanamgambo wa kishia wa Fatemiyoun kutoka Afghanistan na Zainabiyoun wa Pakistan.
Makadirio kuhusiana na idadi ya wanamgambo wanaoiunga mkono Iran waliotumwa nchini Syria, wanakadiriwa idadi kuwa kati ya wapiganaji elfu 25 na 40. Idadi hii inaweza kuongezeka au kupungua kulingana na mahitaji.














