Je, Hezbollah itajiunga na vita vya Hamas dhidi ya Israel?

w

Chanzo cha picha, Getty Images

Kundi la Hezbollah la Lebanon, linaloungwa mkono na Iran, ni tishio kwa Israel kwenye mpaka wake wa kaskazini. Kundi hili la Kishia linavichachafya vikosi vya IDF juu ya operesheni ya ardhini huko Gaza dhidi ya Hamas. Israel hakika haihitaji vita vipya na Hezbollah, lakini hali inaweza kushindwa kudhibitiwa wakati wowote.

Zaidi ya wiki mbili zimepita tangu shambulio la umwagaji damu lililofanywa na wanamgambo wa Kiislamu wa Hamas dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba.

Iran ni wafadhili wakuu wa Hamas na Hezbollah, na wanaunganishwa na wazo la pamoja la kuangamiza Israel.

Je, Hezbollah itaingia vitani?

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Hezbollah ina wapiganaji takribani elfu 60

Tangu Oktoba 7, wanamgambo hao wamekuwa wakirushiana makombora na Israel - lakini kiwango cha mapigano yao ni kidogo.

Hali iliendelea kuwa mbaya wiki iliyopita. Siku ya Ijumaa, Israel iliamuru kuhamishwa kwa watu kutoka mji wa Kiryat Shmona, karibu na mpaka na Lebanon.

Siku ya Jumamosi, Hezbollah ilishambulia maeneo kadhaa ya kijeshi ya Israel, na ndege za Israel na vikosi vya ardhini vilijibu kwa mashambulizi dhidi ya maeneo ya Hezbollah. Jumapili. Walebanoni pia waliamua kuondoka katika maeneo ya mpaka.

Hamas, walipoishambulia Israel, walitegemea msaada wa makundi mengine yenye itikadi kali katika eneo hilo, na sasa wanahisi kutelekezwa, gazeti la L'Orient-Le Jour linasema.

Mwanzilishi mwenza wa Hamas Khaled Meshal wiki iliyopita aliishukuru Hezbollah kwa kila inachofanya, lakini akaongeza kuwa "haitoshi."

Hezbollah, kwa upande wake, ilisema haikuwa na nia ya kushiriki moja kwa moja katika mzozo huo hadi Israel ivuke "mstari mwekundu" bila kutaja huo mstari.

Vyombo vya habari vya Saudia, vikinukuu vyanzo vilivyo karibu na Hezbollah, vilieleza kwamba yafuatayo yanaweza kuchukuliwa kuwa mstari mwekundu; operesheni ya ardhini huko Gaza; idadi ya waathiriwa kuzidi mno, mauaji ya mmoja wa viongozi na kushambulia maeneo ya Hezbollah.

Uamuzi wa kuingia kwenye mzozo au la, utafanywa Tehran, sio Beirut, ambapo viongozi wa Lebanon mara kadhaa wameweka wazi hawahitaji vita vingine. Mgogoro wa kisiasa na kiuchumi umekuwa ukiendelea nchini Lebanon kwa muda mrefu.

Hezbollah ina uwezo wa kuingia vitani bila kibali cha Iran. Lakini Jamhuri ya Kiislamu bado inapendelea kusubiri.

Iran itaisukuma Hezbollah vitani?

d

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Hezbollah wakiwa katika mafunzo Mei 2023
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kwa mujibu wa Raz Zimmt, profesa katika Chuo Kikuu cha Tel Aviv na mtafiti wa Taasisi ya Utafiti wa Usalama wa Taifa ya Israel (INSS), Iran haina machaguo mengi na italazimika kuchagua kati ya maovu mawili.

"Sidhani kama kampeni ya ardhini ya Israeli katika Ukanda wa Gaza itachukuliwa kuwa mstari mwekundu. Badala yake, itachukuliwa hivyo tutakapofika mahali ambapo kuna tishio la kweli kwa uongozi wa kijeshi na kisiasa wa Hamas katika Ukanda wa Gaza.

Iran italazimika kuchagua kati ya chaguzi mbili mbaya. Isipofanya lolote, itaifanya Israel kuendelea kuleta madhara zaidi kwa Hamas na kufichua udhaifu wa Iran. Ikiwa Iran itaitaka Hezbollah kuingia vitani, jibu la Israel litasababisha uharibifu mkubwa kwa kundi hilo," gazeti la Haaretz linamnukuu mtaalamu huyo.

Hezbollah ilipigana mara ya mwisho na Israel miaka 17 iliyopita, na imejijengea uwezo wake wa kijeshi tangu wakati huo, na sasa inasitasita kujiingiza katika mzozo ambao haiwezi kushinda.

Iran na ushawishi wa kikanda

D

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Bando lenye picha ya kiongozi wa Hezbollah, Hassan Nasrallah

Hezbollah ilipigana mara ya mwisho na Israel mwaka 2006. Baada ya siku 34 za mapigano, zaidi ya Waisraeli 160 na zaidi ya Walebanon 1,200 waliuawa. Mzozo huo ulimalizika kwa kupitishwa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na pande zote mbili zikatangaza ushindi.

Firas Maqsad, mwandamizi katika Taasisi ya Mashariki ya Kati mjini Washington, anasema vita vya mwaka 2006 vilikuwa na gharama kubwa kwa Israel na Hezbollah, na pande hizo mbili zilifanya kazi kubwa ili kuepusha vita vingine katika miaka ijayo.

Tangu wakati huo, makubaliano ambayo hayajasemwa yalianzishwa kati ya Israeli na Hezbollah; wanamgambo hawaishambuli Israeli, na Israeli haishambuli Lebanon.

Baada ya miaka 17 - hali ya sasa ni tishio, na mivutano inaongezeka.

Tangu vita vya 2006, Hezbollah imeongeza kwa kiasi kikubwa silaha zake za makombora, na wapiganaji wake wamepata uzoefu wa kijeshi katika vita vya Syria lakini jeshi la Israel ni bora kuliko uwezo wa wanamgambo hao.

Hata kama Iran haikuhusika moja kwa moja katika shambulio la Hamas, inatazamwa kuwa ndio mhimili wa upinzani - huko Yemen, Iraq, Syria, Lebanon na Ukanda wa Gaza.

''Iran inahusika kwa ukosefu wa utulivu katika eneo hilo, lakini jamhuri hiyo haitaki makabiliano ya moja kwa moja ambayo hatimaye yanaweza kuhusisha Marekani.''

"Swali ni iwapo Iran iko tayari kutoa muhanga manufaa ya Hezbollah nchini Lebanon kwa kupunguza nguvu zake za kijeshi. Haiwezekani iko tayari na hilo - isipokuwa vita vigeuke kuwa mzozo kwa utawala wa Iran,'' anasema Hanin Ghaddar.

Mbinu za kuzuia

k

Chanzo cha picha, EPA

Afisa wa zamani wa Mossad na naibu mkurugenzi wa Baraza la Usalama la Kitaifa la Israeli Sima Shine, ambaye sasa anafanya kazi katika Taasisi ya Israeli ya Mafunzo ya Usalama wa Kitaifa (INSS), anasema.

"Wao [Hezbollah] kuvuruga mawazo yetu. Lengo lao kuu ni kufanya kila linalowezekana kutuzuia kuingia Gaza. Katika hatua hii, hii haipaswi kusababisha vita vya wazi."

"Iwapo vita vitazuka Lebanon, Hezbollah itashindwa na Iran itapoteza kitisho chake," Nicholas Blanford, mtaalam wa Taasisi ya Marekani ya Atlantic Council, akizungumza na Al jazeera.

Hezbollah ni nani?

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Bendera za Israel zikichomwa moto katika maandamano huko Tehran, Iran

Hezbollah iliibuka kwa msaada wa kifedha kutoka Iran na usaidizi wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Irani 1982 katika kukabiliana na uvamizi wa Israeli huko Lebanon.

Hatua kwa hatua, Hezbollah ilibadilika kutoka kundi la wanamgambo na kuwa mshiriki hai katika maisha ya umma nchini Lebanon, na tangu 2005 mrengo huo wa kisiasa umeketi bungeni.

Hezbollah ina hospitali zake, chaneli za televisheni, shule na programu za vijana.

Tangu 2006, Hezbollah imekuwa jeshi kuu la kikanda la Iran. Wapiganaji wa Hezbollah wanatoa mafunzo kwa makundi mengine yenye uhusiano na Iran katika eneo hilo - nchini Syria, Yemen na Iraq. Kikundi hicho kina wapiganaji wapatao elfu 60.

Mrengo wa kijeshi wa Hezbollah unatambuliwa kama shirika la kigaidi katika nchi nyingi duniani - Marekani, Uingereza, Ujerumani, Australia, Misri, Israel, Canada, Uholanzi na baadhi ya nchi mengine.

Urusi haiichukulii Hezbollah kama shirika la kigaidi, ikieleza kwamba harakati hiyo ni nguvu halali ya kijamii na kisiasa yenye uwakilishi katika bunge la Lebanon.

Chini ya mwamvuli wa Iran, Hamas, Hezbollah, Palestinian Islamic Jihad na makundi mengine yaliunda kile kilichoitwa United Front Doctrine miaka kadhaa iliyopita.

Kusudi la umoja huo ni kuidhibiti Israel. Kwa mujibu wa makubaliano yao, ikiwa moja ya kundi linataka kuangamizwa, wengine watajitokeza kuunga mkono.