Viongozi watano duniani waliowahi kurushiwa viatu hadharani

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Yusuph Mazimu
- Akiripoti kutoka, BBC Dar es Salaam
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Mnamo tarehe 4 Mei 2025, Rais wa Kenya, William Samoei Ruto, alikumbwa na tukio lisilo la kawaida alipokuwa akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara, eneo la Kehancha , Kuria Magharibi, Kaunti ya Migori.
Katika hali ya mshangao na taharuki, mtu mmoja kutoka kwenye umati uliokuwepo alirusha kiatu chake kuelekea kwa Rais Ruto, jambo lililosababisha mtafaruku wa muda mfupi kabla ya walinzi kuchukua hatua.
Ingawa kiatu hicho hakikumjeruhi Rais Ruto, tukio hilo limeibua hisia tofauti miongoni mwa Wakenya na watu wa mataifa mengine, likichochea mjadala kuhusu maana ya kurushiwa kiatu, na wengine kujiuliza kama wapo viongozi wengine wameshawahi kufanyiwa hivyo.
Katika tamaduni mbalimbali, hasa zile za Kiarabu na Asia ya Kusini, kurusha kiatu ni ishara ya dharau ya hali ya juu. Inamaanisha kumdhalilisha mtu hadharani, kumpa fedheha isiyofutika. Viatu vinachukuliwa kuwa kichafu kwa sababu ya kugusa ardhi, hivyo kurushiwa mtu kiatu ni kama kumwambia hana thamani au heshima.
Katika maeneo mengine ni kejeli, lakini katika mataifa mengi ya afrika ni ishara ya kisiasa na kutofautiana kwenye itikadi ama masuala fulani fulani yanayoendana na siasa.
Rais Ruto si kiongozi wa kwanza duniani kukumbwa na tukio kama hili. Hapa ni baadhi ya matukio yanayofanana.
1. George W. Bush: Baghdad, Iraq (2008)

Chanzo cha picha, Getty Images
Mnamo tarehe 14 Desemba 2008, Rais wa Marekani wa wakati huo, George W. Bush, alikumbwa na tukio lisilo la kawaida wakati wa mkutano wa pamoja na Waziri Mkuu wa Iraq, Nouri al-Maliki, katika Kasri la Republican, Baghdad. Mkutano huo ulikuwa sehemu ya ziara ya kuaga kabla ya kumaliza muhula wake wa urais.
Wakati wa mkutano huo, mwandishi wa habari wa Iraq, Muntadhar al-Zaidi, alisimama ghafla na kurusha viatu viwili mfululizo kuelekea kwa Rais Bush, akipaza sauti kwa Kiarabu: "Hii ni busu la kukuaga kutoka kwa watu wa Iraq, wewe mbwa!" Bush alifanikiwa kuvikwepa viatu hivyo kwa kuinama na viatu hivyo havikumgusa. Al-Zaidi alikamatwa mara moja na maafisa wa usalama na kuondolewa kwenye eneo hilo.
Baada ya tukio hilo, al-Zaidi alihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela kwa kosa la kumshambulia kiongozi wa kigeni, lakini kifungo hicho kilipunguzwa hadi mwaka mmoja, na aliachiliwa baada ya miezi tisa kutokana na tabia njema aliyoionyesha. Alidai kuwa aliteswa akiwa kizuizini, akipigwa na kuteswa kwa njia mbalimbali. Tukio hilo lilizua mjadala mkubwa duniani na kumfanya al-Zaidi kuwa shujaa kwa baadhi ya watu katika ulimwengu wa Kiarabu. Ingawa kwa jamii nyingine alionekana kama mtu asiyekuwa na heshima mbele ya viongozi.
2. Wen Jiabao: Cambridge, Uingereza (2009)

Chanzo cha picha, getty
Februari 2 2009, Waziri Mkuu wa China, Wen Jiabao, alirushiwa kiatu wakati wa hotuba yake akiwa katika Chuo Kikuu cha Cambridge, Uingereza. Tukio hilo lilitokea wakati Wen alikuwa akihutubia wanafunzi na wahadhiri katika ukumbi wa hotuba wa chuo hicho.
Mwanafunzi wa Ujerumani, Martin Jahnke, ambaye alikuwa mtafiti wa tiba katika chuo hicho, alisimama ghafla, akapiga filimbi, na kumuita Wen "dikteta," akidai kuwa chuo hicho kilikuwa "kimejiuza" kwa kumkaribisha kiongozi huyo.
Kisha alirusha kiatu chake kuelekea jukwaani, lakini hakikumpata Wen. Badaye Jahnke alikamatwa na kufikishwa mahakamani kwa kosa la kusababisha hofu na usumbufu, lakini baadaye aliachiliwa baada ya Mahakama kusema ushahidi haukuwa wa kutosha kuthibitisha kosa hilo.
3. Pervez Musharraf – London, Uingereza (2009)

Chanzo cha picha, Getty Images
Mnamo mwaka 2009, aliyekuwa Rais na Kiongozi wa Kijeshi wa Pakistan, Pervez Musharraf, alirushiwa kiatu wakati wa mkutano na wanadiaspora wa Kipakistani mjini London. Tukio hilo lilitokea wakati Musharraf alikuwa akihutubia umati wa watu waliokusanyika kumsikiliza.
Mwanaume mmoja kutoka umati uliokuwepo alisimama ghafla na kurusha kiatu kuelekea kwa Musharraf, akipinga utawala wake wa kijeshi na sera zake. Kiatu hicho hakikumgusa Musharraf, na mlinzi wake alifanikiwa kumzuia mshambuliaji huyo, ambaye alikamatwa mara moja na kuondolewa kwenye ukumbi huo.
Tukio hilo lilionyesha hasira na upinzani wa baadhi ya wananchi wa Pakistan dhidi ya utawala wa Musharraf.
4. Omar al-Bashir: Addis Ababa, Ethiopia (2010)

Chanzo cha picha, Getty Images
Mnamo mwaka 2010, Rais wa Sudan wa wakati huo, Omar al-Bashir, alirushiwa kiatu wakati wa mkutano wa viongozi wa Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa, Ethiopia. Tukio hilo lilitokea wakati al-Bashir alikuwa akihutubia mkutano huo.
Mwanaume mmoja kutoka umati alisimama ghafla na kurusha kiatu kuelekea kwa al-Bashir, akipinga utawala wake na mashtaka ya uhalifu wa kivita yaliyokuwa yakimkabili katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC). Kiatu hicho hakikumgusa al-Bashir, na mshambuliaji huyo alikamatwa mara moja na maafisa wa usalama.
5. Hillary Clinton – Las Vegas, Marekani (2014)

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mnamo tarehe 10 Aprili 2014, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton, alirushiwa kiatu wakati wa hotuba katika mkutano wa Taasisi ya Usafishaji wa Chuma (Institute of Scrap Recycling Industries) katika hoteli ya Mandalay Bay, Las Vegas.
Mwanamke mmoja alitembea kuelekea jukwaani, akiwa umbali wa kama safu sita kutoka alipokuwa Bi. Clinton, na kurusha kiatu chake kuelekea kwake. Clinton alifanikiwa kukikwepa kiatu hicho, na akaendelea na hotuba yake kwa ucheshi, akisema, "Je, hiyo ilikuwa sehemu ya onyesho la Cirque du Soleil?"
Mshambuliaji huyo alikamatwa mara moja na maafisa wa usalama na kuondolewa kwenye ukumbi huo.
Matukio haya yanaonyesha jinsi kurusha kiatu kwa kiongozi wa kisiasa kunavyochukuliwa kama ishara ya dharau na kwa wengine ni upinzani. Ingawa ni kitendo cha kuonesha hasira, kinahatarisha usalama na heshima ya nafasi ya uongozi. Viongozi wengi wamechagua kujibu kwa ustaarabu, wakionyesha ukomavu wa kisiasa na kujiamini.














