Kombe la Dunia 2022: 'Tulishuhudia Morocco ikiandikisha historia'

Kelele za ajabu zilipigwa katika uwanja wa Al Thumama - mchanganyiko wa furaha na kutoamini, machozi, kukumbatiana na tabasamu.
Mashabiki wa Morocco walikuwa na ndoto ya wakati huu, lakini sio wengi walitarajia kwamba ingetimia.
Timu yao imeandikisha historia, kuwa timu ya kwanza ya Kiarabu na Afrika kutinga nusu fainali ya Kombe la Dunia baada ya kushinda Ureno.
Wakati mkubwa kwa bara na kanda.
Kulikuwa na taharuki uwanjani na kwenye viti. Mashabiki wa Morocco waliimba mwonaji au "songa mbele" kwa Kiarabu, na kushangilia timu yao ilipofunga.
"Huu ni usiku ambao nitawasimulia watoto wangu na wajukuu," Soufiane Megrini aliniambia.
"Morocco ilitufanya tujivunie. Tunajivunia timu yetu na kocha wetu."

Soufiane aliniambia jinsi alivyoguswa na uungwaji mkono mkubwa wa Waarabu kwa timu yake.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Alisema licha ya kupata lahaja ya Morocco kuwa ngumu, baadhi ya watazamaji kutoka nchi nyingine za Kiarabu wametaka kushiriki katika nyimbo hizo, wakiuliza jinsi ya kutamka maneno hayo.
"Walikuwa wamesimama karibu nasi... walikuwa wakiimba nyimbo za Morocco," alisema.
Bendera zinasimulia sehemu muhimu ya hadithi ya Kombe la Dunia la Morocco. Ninapoandika haya, ghorofa ndefu zaidi nje ya dirisha langu inaangaza rangi nyekundu na nyota ya kijani katikati.
Lakini kulikuwa na wengine kando na bendera nyekundu na kijani ya Morocco: Mashabiki walibeba bendera za Saudi Arabia, Iraq, Misri, Palestina, Qatar na Jordan.
Maelfu ya mashabiki wamesafiri kutoka katika ulimwengu wa Kiarabu hadi hapa Doha. Wengi wametuambia wamebadilisha tiketi zao kila mara Morocco iliposhinda.
Huenda wengine wakalazimika kuzibadilisha tena ili kushuhudia mechi nyingine ya kihistoria kwa timu yao.
Zineb Aklikm na mumewe Aziz Benyahya walisafiri hadi Doha kutoka Morocco siku moja kabla ya mechi hiyo. Walimwacha mtoto wao wa miezi miwili kurudi nyumbani.
"Kama mama, nijihisi mkosa," Zineb alisema, "lakini nitamwambia kuhusu usiku wa leo. "Sidhani kama kweli tunatambua kilichotokea. Tulikuwa tukishuhudia historia."

Mohammed Rizki alikuwa mwingi wa tabasamu, pindo za kofia yake ya jadi ya Morocco zikisonga huku akiongea kwa madaha. "Siwezi kuelezea kwa kweli," alisema. "Ni mseto wa hisia. Tuna furaha sana kuhusu ushindi na tunafurahia kile kinachokuja." Huu ni wakati mzuri sana wa michezo kwa Morocco. Ni utendaji bora zaidi katika historia ya timu hii, lakini inakwenda vizuri zaidi ya mpira wa miguu. Huu ni wakati unaohitajika sana wa furaha ya pamoja na fahari kwa eneo zima na bara.
Muhimu zaidi, huu ni wakati ambao umebadilisha jinsi timu za Kiarabu na Kiafrika zinavyotazamwa sio tu katika macho ya vikosi vya Ulaya na Amerika Kusini, lakini machoni pa umati wao wenyewe.
Moja ya video zilizoshirikishwa zaidi baada ya mchezo, mbali na timu ya Morocco kusherehekea, ni ile ya Cristiano Ronaldo akilia - wakati Ureno ilipotimuliwa kwenye mashindano.
Mtazamaji mmoja aliniambia kuwa huu ni wakati wa "kujiamini" - kusimama uso kwa uso na wababe wa mchezo huu na kuwa washindani wa kweli na nguvu kubwa.
"Tunachotaka sasa ni kombe," Mohammed Rizki alisema. Aliongeza: "Hatuko hapa ili tu kuwa kwenye mashindano. Tuko hapa kushinda."














