Uchaguzi DR Congo: Upigaji kura wakumbwa na 'machafuko' na ucheleweshaji wa muda mrefu

TH

Chanzo cha picha, Reuters

Na Emery Makumeno

BBC News, Kinshasa

Upigaji kura katika uchaguzi mkuu wa urais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo umekumbwa na ucheleweshaji wa muda mrefu na madai ya udanganyifu.

Baadhi ya vituo vya kupigia kura havikufunguliwa siku nzima, na hivyo kusababisha mafadhaiko mkubwa. Upigaji kura umeongezwa hadi Alhamisi katika baadhi ya maeneo ambayo wapiga kura hawakuweza kutekeleza shughuli hiyo muhimu au kwa vituo vilivyofunguliwa kwa kuchelewa.

Wagombea wanne wa upinzani wametaka uchaguzi huo kufutwa na kurudiwa upya .

Mmoja wao alielezea uchaguzi huo kama "machafuko kamili", kufuatia ghasia wakati wa kampeni.

Rais Félix Tshisekedi anakabiliwa na wagombea 18 wakati anawania muhula wa pili.

Takriban watu milioni 44 walistahili kupiga kura zao, kufuatia kampeni iliyotawaliwa na mzozo unaozidi kuwa mbaya katika eneo la mashariki lenye utajiri wa madini.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

DR Congo ni takriban mara nne ya ukubwa wa Ufaransa, lakini haina miundombinu ya kimsingi - hata baadhi ya miji yake mikubwa haijaunganishwa na barabara. Takriban theluthi mbili ya wakazi milioni 100 nchini humo wanaishi chini ya umaskini, na kupata $2.15 (£1.7) kwa siku au chini ya hapo.

Umoja wa Mataifa, Misri na nchi jirani ya Kongo-Brazzaville zilisaidia kusafirisha vifaa vya uchaguzi katika maeneo ya mbali.

Kura zilipaswa kufunguliwa saa 06:00 saa za ndani (04:00 GMT mjini Goma; 05:00 GMT mjini Kinshasa), na kufungwa baada ya saa 11. Lakini ucheleweshaji mkubwa uliripotiwa.

Mwanamke mmoja mjini Kinshasa aliambia BBC kuwa alilazimika kupigana ndani ya kituo ili kupiga kura. "Kulikuwa na machafuko," alisema. "Nilikanyagwa chini ya miguu."

Mpiga kura mwingine alisema alirudi nyumbani baada ya kituo cha kupiga kura kukosa kufunguliwa kufikia 18:00 saa za huko, wakati umeme ulipokatika. "Baadhi ya watu wamekuwa hapa tangu 04:00 lakini tuliambiwa kulikuwa na tatizo kwenye mashine," aliambia BBC.

Mgombea urais wa upinzani Martin Fayulu, mshindi wa pili katika uchaguzi wa urais uliozozaniwa wa 2018, alielezea hali hiyo kama "machafuko kamili".

"Ikiwa watu wote hawatapiga kura katika vituo vyote vya kupigia kura vilivyoonyeshwa na Ceni [Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi], hatutakubali uchaguzi huu," alinukuliwa akisema na Reuters baada ya kupiga kura katika mji mkuu.

Shirika hilo la habari liliripoti kwamba mgombea mwingine wa urais, Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel Denis Mukwege, alidai kwamba "udanganyifu wa uchaguzi wa karne [ulikuwa] unafanyika".

Bw Fayulu na Bw Mukwege walijumuika na wagombea wengine wawili katika kutoa wito wa marudio ya uchaguzi huo.

Mfanyabiashara Milionea Moïse Katumbi alisema ni mapema sana kukata kauli lakini kumekuwa na "mapungufu mengi".

Afisa wa Ceni Patricia Nseya alikiri visa vya utovu wa nidhamu miongoni mwa wafanyikazi wake na kuahidi hatua baada ya uchunguzi unaoendelea.

Kulingana na kundi la waangalizi la Symocel, karibu 60% ya vituo vya kupigia kura vilifunguliwa kwa kuchelewa, wakati 30% ya mashine za wapigakura zilikuwa na kasoro.

Mkuu wa uchaguzi Denis Kadima alisema upigaji kura utazidishiwa muda hadi Alhamisi katika maeneo ambayo upigaji kura haukufanyika Jumatano.

Pia alithibitisha kuwa kulikuwa na majaribio 3,244 ya kudukua mifumo ya kompyuta ya taasisi hiyo.

Katika mji wa kaskazini-mashariki wa Bunia, watu ambao hapo awali walikimbia ghasia na hawakuweza kusafiri kurejea vijijini kwao kupiga kura walionyesha hasira yao kwa kushambulia kituo cha kupigia kura na kuharibu mashine za kupigia kura kabla ya polisi kurejesha utulivu.

TH

Chanzo cha picha, CHARLIE OMBA

Kuna baadhi ya maeneo ambapo upigaji kura haufanyiki kabisa kwa sababu ya shughuli za waasi.

Ceni inatarajiwa kutangaza matokeo ya muda tarehe 31 Disemba.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo iko kwenye hifadhi kubwa ya cobalt, ambayo kwa sasa ni sehemu muhimu ya betri nyingi za lithiamu, zinazoonekana kuwa muhimu kwa mustakabali usio wa nishati ya mafuta.

Kwa mara ya kwanza, raia wa Kongo wanaoishi katika nchi nyingine tano - ikiwa ni pamoja na Afrika Kusini na na nchi iliyoitawala DRC Ubelgiji - wakati wa ukoloni wanaweza kupiga kura zao.

Kama hapo awali, mshindi atakuwa mgombea aliye na kura nyingi zaidi, na hakuna duru ya pili ikiwa watashindwa kuvuka alama ya 50%. Idadi kubwa ya wapinzani kwa Bw Tshisekedi inaweza kumnufaisha , kwani inaweza kugawanya uungwaji mkono wa upinzani.

Wapiga kura pia wanachagua wawakilishi wa ubunge, mkoa na manispaa - wenye wagombea wapatao 100,000 kwa jumla - katika nchi hii kubwa, ambayo ina urefu wa kilomita 2,000 (maili 1,400) magharibi hadi mashariki.

Kuna zaidi ya vituo 175,000 vya kupigia kura. Tume ya uchaguzi, kwa usaidizi wa walinda amani wa Umoja wa Mataifa, ilianza kutoa vifaa vya kupigia kura katika maeneo ya mbali takriban miezi miwili iliyopita kwa sababu ya mtandao duni wa usafiri.

Katika eneo la mashariki, ukosefu wa usalama umetawala wakati wa uchaguzi.

Makumi ya makundi yenye silaha yamekuwa yakishindana kudhibiti sehemu za eneo hilo lenye utajiri wa madini.

Kuwepo kwa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa, kikosi cha kanda ya Afrika Mashariki na wanajeshi wa Kongo hakujazima ghasia hizo, ambazo zimesababisha takriban watu milioni saba kulazimishwa kuondoka makwao. Wengi wa wale hawajaweza kujiandikisha kupiga kura, katika kile ambacho wengine walikishutumu kama mchakato wa usajili wenye machafuko.

Vurugu za kisiasa katika maandalizi ya uchaguzi pia zilikuwa chanzo cha wasiwasi.

Katika siku ya mkesha wa upigaji kura, Umoja wa Ulaya ulisema una wasiwasi kuhusu "hotuba za chuki, ghasia na matukio ambayo yameshuhudiwa siku chache zilizopita". Kumekuwa na visa vya vifo, na kusababisha Bw Katumbi kusimamisha kampeni yake kwa muda mfupi.

Imetafsiriwa na Yusuf Jumah na kuhaririwa na Ambia Hirsi