Uchaguzi wa DRC 2023: "Tusifikirie kuwa kazi ya makanisa ni kupinga utawala uliopo" - Mchungaji Eric Senga

Chanzo cha picha, Getty Images
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ni mojawapo ya nchi zilizo na waumini wengi wa Kikatoliki katika eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara, ikikadiriwa kuwa waumini wa kanisa hilo karibu milioni 50 miongoni mwa wakazi wake takriban milioni 100 .
Ingawa serikali ya nchi hiyo sio ya kidini, dini hata hivyo iko kila mahali katika jamii na inaendelea kuwa na ushawishi mkubwa katika maisha ya umma.
Kanisa Katoliki limekuwa moja ya nguzo thabiti za mfumo wa kisiasa na kijamii wa Congo siku zote tangu enzi za ukoloni.
Kwa miongo kadhaa, limekuwa ikitekeleza jukumu lake kama nguvu ya kukabiliana, likijiimarisha kama mshirika muhimu wa serikali , na kuchukua nafasi yake katika maeneo muhimu ya kijamii kama vile elimu, afya na kulinda amani.
Hali inaporuhusu linakuwa mhusika wa kisiasa ili kulinda demokrasia na kuhakikisha kuwa nafasi ya kisiasa ni ya amani na nafasi yake hiyo huheshimiwa na wadau wote.
Majukumu hayo yamelipatia kanisa hilo ushawishi mkubwa na kulipa uhalali wa kihistoria na umaarufu.
Katika mkesha wa uchaguzi wa urais wa Disemba 20, 2023, Kanisa Katoliki kwa kawaida linataka kutumia ushawishi wake na kuhakikisha kunakuwa na uwazi wa mchakato wa uchaguzi na kutekelezwaa matakwa ya watu katika uchaguzi huo.

Chanzo cha picha, PRESIDENCY OF THE REPUBLIC OF THE DRC
Jukumu la kihistoria la Kanisa nchini DRC
DRC ni nchi ambayo dini ipo katika makundi yote ya jamii na maisha ya umma. Kulingana na makadirio ya Vatcan, nchi hiyo ina takriban 49% ya Wakatoliki , 35% ya Waprotestanti na waaminifu wanaoshirikiana na makanisa ya uamsho, 10% ya Kimbanguists (Kanisa la Kikristo lililozaliwa Congo) na Waislamu wachache (10% ).
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Ili kuelewa ushawishi wa Kanisa Katoliki katika maisha ya kijamii ya Congo kwa ujumla na katika nafasi yake ya kisiasa, licha ya kuibuka kwa makanisa ya kiinjilisti, lazima turejelee katika nyakati za mwanzo za historia yake.
Kanisa Katoliki lilianzishwa nchini DRC na wamisionari wa Ubelgiji katika karne ya 19. Tangu wakati huo, limekua kama taasisi yenye ushawishi, na kuwa na nafasi kubwa ya kijamii.
Kanisa ni mshirika mkuu wa Serikali katika nyanja za elimu na afya, llikiziba pengo la ukosefu wa huduma za umma kupitia mtandao wake wa hospitali, vituo vya kijamii na shule mashuhuri, ambazo zimetoa mafunzo kwa viongozi wengi wa Congo.
Kwa mujibu wa Baraza la Maaskofu la Kitaifa la Kongo (Cenco) , Kanisa Katoliki leo linasimamia shule 18,638 kwa jumla zikiwemo shule za msingi 12,616, shule za chekechea 724, na shule za sekondari 5,298 zinazopokea zaidi ya wanafunzi milioni 4.3 wanaofundishwa na waalimu 161,337.
Ushawishi huu pia unaonekana kuingia hadi kwenye uwanja wa kisiasa.
Kuingia kwa Kanisa katika nyanja za kisiasa kulianza tangu kipindi cha mwanzo cha uhuru wa taifa hilo mnamo mwaka 1960. Ushawishi huu ulidumu hadi wakati wa mzozo mkubwa katika miaka ya 1990. Uzito wa Kanisa Katoliki ulijidhihirisha katika maamuzi yaliyochukuliwa wakat iwa mazungumzo ya kisiasa ambayo yalifungua njia ya kuelekea katika mfumo wa vyama vingi.
Askofu Laurent Monsengwo, ambaye wakati huo alikuwa askofu mkuu wa Kisangani (kaskazini-mashariki), alihusika binafsi katika kuanzisha tena mkondo wa mazungumzo ya kisiasa na kuwezesha kufikiwa kwa makubaliano ambayo yalikuwa magumu kufikiwa.

Chanzo cha picha, Getty Images
Miongo kadhaa ya mapambano ya demokrasia
Katika miongo mitatu iliyopita, CENCO imeendelea kufuatilia kwa karibu hali ya kijamii na kisiasa ya ndani ya nchi. Askofu Laurent Monsengwo, huonekana sana katika nyakati ngumu, mara nyingi akijitokeza kukemea majanga yaliyopo kisiasa na kiutawala nchini Congo kama vile rushwa, utawala mbaya na unyanyasaji unaofanywa na mamlaka.
CENCO imejijengea sifa dhabiti na haiba inayotambuliwa na wahusika wote wa kisiasa, ambayo imeiruhusu mara kadhaa kuchukua jukumu la upatanishi katika migogoro iliyofuata mwisho wa utawala wa Mobutu.
Kanisa Katoliki lilishiriki katika kuandaa uchaguzi wa kitaifa na waangalizi wake, na kusisitiza juu ya haja ya kuhakikisha uhuru kamili wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (CENI) unalindwa ili kuepuka maandamano ambayo mara kwa mara yalifuata kila duru ya uchaguzi.

Chanzo cha picha, VATICAN NEWS
Kardinali Laurent Monsengwo Pasinya, aliyefariki dunia mwaka 2021, alikuwa mmoja wa viongozi wa Kanisa Katoliki nchini DRC.
Wakongo wengi wanamkumbuka kama mtetezi wa haki za binadamu na mkosoaji mkali wa serikali mbalimbali za baada ya uhuru tangu 1960.
Matokeo ya mapambano ya Laurent Monsengwo Pasinya yalianza kuonekana wakati wa utawala wa Rais wa zamani Mobutu Sese Seko miaka ya 1990.
Mwaka huo huo, alianzisha hati ya kuomba uhuru zaidi kutoka kwa Marshal Mobutu, ambaye alikuwa madarakani kwa miaka 30 chini ya utawala wa chama kimoja.
Kwa hivyo, anachukuliwa na baadhi ya Wacongo kama mmoja wa watu waliosaidia kusukuma nchi kuelekea hatua zake za kwanza za kidemokrasia.
Baada ya Mobutu, Kardinali alikosoa mamlaka ya Joseph Kabila.
Mnamo Januari 2018, Laurent Monsengwo, wakati huo askofu mkuu wa Kinshasa, aliacha alama yake na hukumu yake maarufu iliyoelekezwa kwa viongozi wa wakati huo siku moja baada ya ukandamizaji wa kikatili wa polisi wa maandamano ya Desemba 31, 2017: 'Wacha watu wa hadhi ya chini watoke!
ENCO pia imehimiza utekelezaji wa mipango madhubuti ya kuwaelimisha raia wa Congo kuhusu maadili ya amani na demokrasia, na kuwahimiza waamini walei kushiriki kikamilifu katika maisha ya kisiasa ya kitaifa.
Mnamo 2006, katika uchaguzi wa kwanza wa urais wa kidemokrasia nchini Congo, Kanisa liliongoza tume huru ya kitaifa ya uchaguzi na kufanya uchunguzi wa awali wa uchaguzi.
Miaka kumi baadaye, mnamo 2016, mwishoni mwa muhula wa pili wa Rais wa zamani Joseph Kabila (2001-2018), ni Kanisa tena ambalo liliandamana na raia kudai kuheshimiwa kwa muda wa mwisho wa kuandaa uchaguzi mpya, kulingana na katiba.
Kanisa lenye ushawishi mkubwa

Chanzo cha picha, Getty Images

Chanzo cha picha, Getty Images
Kanisa Katoliki lenye ushawishi mkubwa lina historia ndefu ya kukuza demokrasia na kufuatilia chaguzi nchini.
Mwaka huu, kwa mara ya kwanza, Baraza la Kitaifa la Maaskofu wa Congo (CENCO) liliungana na Kanisa la Kristo la Congo (ECC) , muungano wa madhehebu 64 ya Kiprotestanti na kiinjili ili kuhakikisha kunakuwa na uendeshaji mzuri wa shughuli za uchaguzi.
Kwa jumla, waangalizi elfu sitini watasambazwa kote nchini. Kulingana na Mchungaji Eric Senga, Katibu Mkuu na msemaji wa Kanisa la Kristo nchini Congo, hii ni kuhakikisha kuwa uchaguzi unakuwa wa uwazi, kuaminika na wa kidemokrasia.
"Kwetu sisi, uchaguzi wa uwazi, unaoaminika na wa kidemokrasia ni uchaguzi ambazo shughuli zake zinatii viwango vya kisheria na kikatiba kwa upande mmoja, na vitendo vinavyotambulika ulimwenguni kote kama vitendo vyema katika demokrasia (...) Uwazi kwetu ni ukweli wa kuweka taarifa hadharani ili wananchi au raia wahakikishe kuwa kinachofanyika ni kielelezo cha utashi wao. Hivyo kwetu sisi dhana za uwazi zinahusu uwezo wa kuweka habari hadharani ili kila mtu awe na kiwango sawa cha habari, kila mtu anahakikisha haki yake imeheshimiwa.
Haki ya kuandikwa jina langu kwa usahihi, haki ya kuonekana kwenye daftari la wapiga kura kwa sababu nimeandikishwa kuwa raia, haki ya kupiga kura kwa sababu nimekidhi masharti yote, kwa sababu tunataka hivyo, na hatimaye, matokeo yatakayochapishwa pia yanakubaliwa. Hatutaki tena kushuhudia hadithi, kama vile ukweli wa masanduku ya kura. Hivi ndivyo tunavyotaka matokeo haya yawe ya amani ili pia watu , watakaoshiriki, wasijihusishe na vita vya udini, siasa, ukabila. "

Chanzo cha picha, Éric Nsenga
Kupambana na mamlaka na sio dhidi ya utawala
Kuingilia huku kwa watu wa kidini katika kisiasa si mara zote bila lawama, hasa pale maaskofu wanapotoa hisia ya kuunga mkono chama kimoja dhidi ya kingine. Lakini kwa Mchungaji Eric Senga, kazi ya makanisa ina lengo moja tu: kuhakikisha kwamba mapenzi ya watu yanaheshimiwa.
"Ningependa kusisitiza hili: tusifikiri kwamba kazi ya makanisa ni kupinga utawala uliopo. Kinachotuhusu sisi ni uwazi na hatimaye, matokeo yaliyopatikana" masanduku ya kura lazima yaakisi usemi wa nia ya watu,” anasema Mchungaji Éric Nsenga, msemaji wa Kanisa la Kristo nchini Congo.
"Hapana, hatuko hapa kusema nani awe rais, nani asiwe. Sio sisi tunaotathmini uamuzi wowote thamani au umuhimu wa wagombea. Hiyo, ni haki ya mtu, ni watu ndio wanaamua, jukumu letu ni kuhakikisha taratibu zinazotumiwa na CENI zinazingatia sheria na matokeo yake yanaakisi matakwa ya wananchi, mgombea bora akishinda huo ndio ushindi wa demokrasia.
Tunapigania kuokoa demokrasia, kuokoa haki, kuokoa ukweli na pia, zaidi ya yote, kuokoa umoja wa kitaifa na kutoa uhalali kwa taasisi za nchi yetu kwa heshima fulani ", anaendelea kusema mwakilishi wa Kanisa la Kiprotestanti.

Chanzo cha picha, CEN
Kando na Kongamano la Kitaifa la Maaskofu la Kongo lenye ushawishi mkubwa, miungano mengine na makanisa ya kiinjili wanatekeleza jukumu lao katika kuleta demokrasia na amani.
Kanisa la Uamsho la Congo lina nia ya kutekeleza ahadi hii kupitia miundo yake mbalimbali ambayo ni hai sana katika masuala ya utetezi, lakini pia kuongeza ufahamu na uchunguzi wa uchaguzi, kulingana na Askofu Mkuu Evariste Ejiba Yamapia , rais na mwakilishi wa kisheria wa Kanisa la Uamsho la Kongo.

Chanzo cha picha, ARCHBISHOP EVARISTE EJIBA YA MAPIA
"Ndio, sisi kama Kanisa la Uamsho la Congo tunashughulikia mambo tofauti. Kwanza ni ufahamu wa wapiga kura kwa sababu uzoefu unatuonyesha kwamba kulikuwa na shauku mwaka 2006 na watu wengi walikuwa na kiu ya kupiga kura.
Na kisha shauku hii ikaendelea kuwepo mwaka 2011, lakini ikapungua kidogo na kisha, ilipofika 2018 naamini kwamba takwimu hazitanipinga, kulikuwa na kushuka kwa shauku kwa sababu kwa wengine, walidhani kuwa watakaoshinda tayari wanajulikana, kwa nini niende kupiga kura?.
Namba mbili tunasema kunatakiwa ya uwajibikaji, yaani kura ambayo haitokani na ukabila au kumthamini mtu bila kujua anachoweza kuliletea taifa.
Pia tunasema kwamba uchaguzi wa uwajibikaji ambao unawashirikisha wananchi kwa njia hii ya kujihusisha kwa kufanya kile tunachokiita ufuatiliaji wa uchaguzi. Ufuatiliaji huu ni njia ya kuonyesha vipengele tofauti vinavyohusishwa na mchakato wa uchaguzi. "

Chanzo cha picha, Getty Images
Kuanzia Mkutano Mkuu wa Kitaifa wa 1992 hadi maandamano kuhusu mchakato wa uchaguzi kati ya 2016 na 2019, Kanisa Katoliki, kupitia CENCO, limekuwa na jukumu muhimu katika kupigania demokrasia nchini DRC.
Huku likisalia ndani ya mipaka ya majukumu yao, Makanisa nchini DRC yanajieleza mara kwa mara kuhusu nyanja zote za maisha ya kijamii, kiuchumi na kisiasa ya nchi.
Katika miaka ya hivi karibuni, Maaskofu wa Congo wamesisitiza wito wao wa amani katika majimbo ya mashariki yanayokumbwa na vita, wakisikitishwa na uwepo wa vikosi vya kigeni vinavyoendelea kuyumbisha eneo hilo kupitia ghasia na kunyonya madini yake mengi, ambayo mengine ni muhimu kwa utengenezaji wa vifaa vya kielektroniki.
Kwa miaka mingi, Kanisa Katoliki limejiimarisha kama taasisi inayoheshimika na yenye ushawishi mkubwa katika jamii ya Congo, ambapo linaendelea kuaminiwa kwa jukumu lake kama mtetezi muhimu katika vita kati ya mamlaka na upinzani.
Kuibuka kwa makanisa ya kiinjili kunathibitisha uzito huu wa kihistoria na ushawishi ambao dini inaendelea kuwa nao katika maendeleo ya jamii ya Congo.
Mkutano muhimu wa uchaguzi wa 2023 sio ubaguzi kwa sheria kwa kanisa la Kikatoliki linalochukuliwa kama "Kanisa Katoliki kubwa zaidi barani Afrika".
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi na kuhaririwa na Yusuf Jumah












