Uchaguzi wa DRC 2023: Unachohitaji kujua

Denis Mukwege ni mmoja wa wagombea 22 wa urais

Chanzo cha picha, AFP

Takribani wapiga kura milioni 40 wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo watapiga uchaguzi ujao wa rais tarehe 20 Desemba huku Rais Félix Tshisekedi akitafuta muhula wa pili na wa mwisho wa miaka mitano madarakani.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ni nchi kubwa zaidi katika Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara. Ikichukua eneo lenye ukubwa wa Ulaya Magharibi yenye idadi ya watu wanaokadiriwa kuwa zaidi ya milioni 100, nchi hiyo ina utajiri mkubwa wa maliasili.

Licha ya baadhi ya wito wa kutaka uchaguzi uahirishwe, mkuu wa tume ya uchaguzi ana imani kuwa kila kitu kitakuwa tayari kwa wakati.

Kwa nini uchaguzi huu una umuhimu?

Ina 70% ya akiba ya dunia ya coltan, madini ya thamani sana ambayo hutumiwa kutengeneza simu za mkononi, pamoja na 30% ya almasi duniani na kiasi kikubwa cha cobalt, shaba na bauxite.

Ingawa utajiri wake mkubwa wa madini na idadi kubwa ya watu inawakilisha rasilimali kubwa ya kiuchumi, maisha nchini DR Congo hayajaboreka kwa watu wengi kwa sababu kadhaa, kama vile migogoro, rushwa na miongo mingi ya utawala mbovu tangu enzi za ukoloni.

Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, sehemu kubwa ya utajiri wa madini, imekumbwa na vita kwa miongo mitatu.

Haijafahamika ni watu wangapi wamepoteza maisha, utafiti wa mwaka 2008 uliofanywa na Kamati ya Kimataifa ya Uokoaji ilikadiria kuwa takribani watu milioni 5.4 wanaweza kuwa wamekufa, wengi wao kutokana na njaa na magonjwa, na kuifanya kuwa mbaya zaidi tangu Vita vya Pili vya Dunia. Hatahivyo, tafiti nyingine zimetia shaka juu ya usahihi wa takwimu hizi.

Baada ya miaka mingi ya misukosuko ya kisiasa na mapinduzi ya serikali, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inaandaa uchaguzi kwa mara ya kwanza tangu kukabidhiwa madaraka kwa amani kati ya Rais wa zamani Joseph Kabila na Bw.Tshisekedi mnamo 2019.

Wagombea ni nani?

Kufuatia kujiondoa kwa wagombea wanne, akiwemo Waziri Mkuu wa zamani Augustin Matata Ponyo, sasa kuna wagombea 22 wa urais, akiwemo Bw Tshisekedi.

Wapinzani wake wakuu ni:

  • Martin Fayulu, anayeaminika na waangalizi wengi kuwa ndiye mshindi halali wa uchaguzi wa urais wa 2018, ingawa aliibuka wa pili kwa mujibu wa matokeo rasmi.
  • Moïse Katumbi, mfanyabiashara tajiri na gavana wa zamani wa jimbo la Katanga, na pia mmiliki wa timu ya soka ya TP Mazembe.
  • Dkt.Denis Mukwege, mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel 2018 kwa kazi yake na walionusurika ubakaji.

Wagombea wanne ambao wamejiondoa wote wamemuunga mkono Bw.Katumbi na chama chake cha ''Together for the Republic".

Bado wamo Waziri Mkuu mwingine wa zamani, Adolphe Muzito, Mbunge Delly Sesanga, mwanaharakati Floribert Anzuluni na Constant Mutamba.

 Rais Félix Tshisekedi alizindua kampeni yake katika uwanja mkuu wa mpira wa miguu wa Kinshasa

Chanzo cha picha, AFP

Kuna wanawake wawili pekee katika kinyang'anyiro hicho: Marie-Josée Ifoku Mputa, mgombea urais mnamo Desemba 2018, na Joëlle Bile, ambaye anajieleza kuwa mgombea anayewakilisha matumaini kwa wanawake na vijana.

Kugombea uchaguzi sio rahisi.

Wagombea wote walilazimika kulipa faranga za Congo milioni 160 ($60,000; £47,000) ikiwa ada za maombi zisizoweza kurejeshwa.

Hata hivyo, kiasi hiki ni chini ukilinganisha na uchaguzi uliopita, wakati ada ilipokuwa $100,000.

Mfumo wa kupiga kura

Mgombea yeyote atakayepata kura nyingi zaidi katika duru ya kwanza anakuwa rais ajaye, akiwa na zaidi ya 50%. Kwa hivyo hakuna duru ya pili.

 Wafuasi wa Martin Fayulu wanaamini aliibiwa ushindi mwaka wa 2018

Chanzo cha picha, AFP

Mshindi atakuwa katika nafasi hiyo kwa muhula wa miaka mitano.

Upigaji kura unafanyika siku 90 kabla ya kumalizika kwa muhula wa rais wa sasa.

Mwaka huu, uchaguzi wa urais utaunganishwa na uchaguzi wa wabunge wa kitaifa na majimbo na madiwani wa mitaa.

Uchaguzi wa mwaka huu unafanyika kukiwa na mzozo wa mashariki, mzozo wa kiuchumi na kijamii na ukosefu wa uaminifu kati ya serikali na upinzani.

Vyama vya upinzani vinashuku serikali kupanga udanganyifu katika uchaguzi, vikishutumu kwa kuzuia uhuru na nafasi ya kidemokrasia. Serikali inakana tuhuma hizi.

Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuna milima na maziwa mazuri, pamoja na utajiri mkubwa wa madini. Huu ni muonekano wa mji wa Bukavu

Chanzo cha picha, AFP

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Uhakikisho uliotolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (Ceni) haujaondoa wasiwasi wa upinzani.

Maaskofu wa Kanisa Katoliki lenye ushawishi mkubwa nchini DR Congo, na viongozi wa Kanisa la Kristo nchini humo (ECC) hivi karibuni walisema wana wasiwasi kama ilivyo kwa upinzani.

Pia kuna mgogoro wa gharama ya maisha. Madhara ya janga la Covid-19 na vita nchini Ukraine bado vinakumba mifuko ya watu wa kawaida wa Congo.

Mfumuko wa bei umepunguza uwezo wa wananchi wa kawaida kununua, ambapo sasa wanapaswa kulipia zaidi mahitaji yao ya msingi, kama vile chakula.

Thamani ya faranga ya Congo imeshuka kwa 15-20% dhidi ya dola ya Marekani tangu kuanza kwa mwaka huu, kulingana na takwimu rasmi.

Theluthi mbili ya wakazi wa DR Congo sasa wanaishi chini ya mstari wa umaskini, na kupata $2.15 kwa siku au chini ya hapo.

Rais Tshisekedi amezindua mipango kadhaa ya kujaribu kukabiliana na masuala haya ikiwa ni pamoja na elimu ya bure ya shule ya msingi na huduma za afya bila malipo kwa wanawake wanaojifungua katika vituo vya matibabu vya umma.

Hata hivyo, maoni yanasalia kuwa tofauti kuhusu jinsi hatua hizi zimekuwa na ufanisi kote nchini.

Mgogoro mashariki

Serikali imeweka hali ya kuzingirwa katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Ituri kwa karibu mwaka mmoja lakini mzozo unaendelea kupamba moto.

Makundi ya waasi kama vile M23, Allied Democratic Forces (ADF) na Codeco yanaendelea kufanya mashambulizi dhidi ya watu wa kawaida na walengwa wa kijeshi.

Wanajeshi wa Kenya walitumwa DR Congo mwaka jana kusaidia kukabiliana na makundi ya waasi lakini serikali imewaamuru kuondoka

Chanzo cha picha, AFP

Kutokana na ghasia hizo, DR Congo ni miongoni mwa nchi zenye idadi kubwa zaidi ya wakimbizi wa ndani duniani.

Takribani watu milioni 6.9 wanadhaniwa kulazimika kuyahama makazi yao tangu Machi 2022.

Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa 28% ya watu wamelazimika kuyahama makazi yao Kivu Kaskazini na 39% Ituri.

Maeneo makubwa mengine yameibuka kutokana na migogoro baina ya jamii, hasa katika jimbo la Tshopo, kaskazini mashariki, na Maï-Ndombe, kusini-magharibi mwa nchi.

Ukosefu wa usalama huenda ukatatiza upigaji kura katika baadhi ya maeneo ya nchi. Mnamo Novemba, tume ya uchaguzi ilisema ilipoteza takribani mawakala 30 kwa kufa maji na kushambuliwa na vikundi vilivyojihami wakati wa usajili wa wapiga kura.

Hivi karibuni serikali ya Congo ilidai kuondoka kwa wanajeshi kutoka nchi za Afrika Mashariki ifikapo mwishoni mwa mwaka huu, ikizishutumu kwa kushindwa kuzuia mashambulizi kutoka kwa makundi yenye silaha chini ya mwaka mmoja baada ya kutumwa huko.

Kuangalia kura

Tume ya uchaguzi inapaswa kuwa chombo kinachojitawala, cha kudumu na kisichoegemea upande wowote kinachotawaliwa na sheria za umma, na kilichopewa mamlaka ya kisheria.

Inaundwa na wanachama 15, dhamira yake ni "kuhakikisha uchaguzi huru na wa kidemokrasia".

Moise Katumbi ni mmiliki wa timu kubwa ya soka ya TP Mazembe

Chanzo cha picha, AFP

Hata hivyo, imeshutumiwa na wakosoaji wanaomtuhumu rais wake, Denis Kadima, kuwa karibu sana na serikali. Wanahofia ukweli kwamba anatoka katika kabila moja na rais anaweza kuathiri uhalisia wa matokeo.

Kwa upande wake, Bw Kadima amerudia kusema kuwa taasisi yake imejitolea kufanya uchaguzi wa uwazi unaoheshimu kanuni za kidemokrasia.

Ujumbe wa waangalizi wa Umoja wa Ulaya umejiondoa katika uchaguzi huo, baada ya kushindwa kuafikiana na serikali ya Congo kuhusu uingizaji wa vifaa vya mawasiliano walivyohitaji kutumia. Watakuwa wakipeleka wataalamu wanane lakini katika mji mkuu wa Kinshasa pekee.

Katika siku za nyuma, Umoja wa Afrika, madhehebu ya kidini na mashirika ya kiraia yalituma waangalizi kufuatilia kwa karibu upigaji kura.

Matokeo tutayapata lini ?

Kwa mujibu wa kalenda ya uchaguzi, matokeo ya awali yanatarajiwa tarehe 31 Desemba.

Ikiwa matokeo yatakuwa tayari kabla ya hapo, yanaweza kutolewa mapema.

Lakini katika chaguzi zilizopita, Ceni haikutangaza matokeo yoyote, ilisubiri mpaka kura zote zihesabiwe kote kabla ya kutangaza mshindi.

Rais ajaye ataapishwa rasmi tarehe 20 Januari.

Imetafsiriwa na Lizzy Masinga