Uchaguzi wa Urais DRC: mwongozo kamili wa kuuelewa uchaguzi wa Disemba 2023
Ousmane Badiane
BBC Afrika

Chanzo cha picha, Getty Images
Takriban wapiga kura milioni 40 wa Congo wametolewa wito wa kupiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa rais mnamo Desemba 20, 2023.
, Rais Félix Tshisekedi ambaye aliyechaguliwa mwaka wa 2018 anawania muhula wa pili wa miaka mitano.
BBC Africa inakupa mwongozo wa kujua kila kitu kuhusu uchaguzi wa urais wa Disemba 2023 katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Kwa nini uchaguzi huu ni muhimu na unafuatiliwa?
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ndiyo nchi kubwa zaidi katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara. Ikiwa na idadi ya watu inayokadiriwa kuwa zaidi ya wakazi milioni 100, nchi hii yenye ukubwa wa Ulaya Magharibi imejaa maliasili nyingi sana.
Ina 70% ya akiba ya ulimwengu ya coltan, madini ambayo yanathaminiwa sana kwa utengenezaji wa simu za rununu, 30% ya almasi pamoja na kiasi kikubwa cha dhahabu na shaba.
Ingawa uwezo wake wa kidemografia unawakilisha njia muhimu, maendeleo ya DRC yanatatizwa na mambo kadhaa ikiwa ni pamoja na vita katika sehemu yake ya mashariki ambavyo vimesababisha vifo vya zaidi ya watu milioni 8 katika kipindi cha miongo miwili. Ni moja ya mapigano mabaya zaidi ya kivita tangu Vita vya Pili vya Dunia.

Chanzo cha picha, Getty Images
Wagombea wa urais

Chanzo cha picha, Getty Images
Mnamo Oktoba 20, Tume Huru ya Kitaifa ya Uchaguzi (CENI) ilichapisha orodha ya muda ya wagombea 24 wa uchaguzi wa urais wa tarehe Disemba 20.
Orodha ambayo hatimaye iliongezeka hadi wagombea 26 baada ya Mahakama ya Katiba kuongeza, maombi mawili Jumatatu Oktoba 30 ambayo hayakukubaliwa na CENI.
Orodha hii bado ni ya muda kwa sababu ni lazima ichunguzwe na Mahakama ya Kikatiba kabla ya kuchapishwa kwa orodha ya mwisho.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Miongoni mwa wagombea 26 waliosajiliwa, ni rais anayemaliza muda wake, Félix Tshisekedi, aliye madarakani tangu Januari 2019 na mgombea anayewania kuchaguliwa tena.
Wapinzani wake wakuu watakuwa viongozi kadhaa wa upinzani kama vile Martin Fayulu, mgombea ambaye hakufanikiwa katika uchaguzi wa urais wa 2018, mfanyabiashara tajiri Moïse Katumbi, gavana wa zamani wa Katanga (kusini-mashariki) na Dkt Denis Mukwege, mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel 2018 ambaye alipata tuzo hiyo kwa kitendo chake cha kuwahudumia na kuwatetea wanawake waliobakwa.
Pia kuna Mawaziri Wakuu wa zamani Adolphe Muzito na Augustin Matata Ponyo, Mbunge Delly Sesanga, mwanaharakati Floribert Anzuluni na Constant Mutamba ambaye yuko karibu na kambi ya Kabila.
Wanawake wawili tu ndio waliamua kuingia kwenye mbio hizo. Hawa ni Marie-Josée Ifoku Mputa, ambaye alikuwa mgombea katika uchaguzi wa urais wa Disemba 2018, na Joëlle Bile. Anajinadi kama mgombea ambaye anataka kutoa matumaini kwa wanawake na vijana.
Wagombea wote walipaswa kuwasilisha kwa CENI risiti ya malipo ya faranga za Kongo milioni 160, sawa na zaidi ya dola 60,000 kama ada zisizorejeshwa za kutuma maombi.
Wakati wa uchaguzi uliopita, wagombea walipaswa kulipa kiasi cha USD 100,000.
Hii hapa orodha kamili ya wagombea 26
- Felix Tshisekedi
- Moise Katumbi
- Martin Fayulu
- Denis Mukwege
- Marie-Josée Ifoku
- Noel Tshiani
- Seth Kikuni
- Radjabho Tebabho Soborabo
- Theodore Ngoy
- Augustin Matata Ponyo
- Adolphe Muzito
- Tony Bolamba
- Jean-Claude Baende
- Delly Sesanga
- Franck Diongo
- Constant Mutamba
- Justin Mudekereza
- Georges Buse Falay
- Rex Kazadi
- Abraham Ngalasi
- Nkema Liloo Bokonzi
- Floribert Anzuluni
- Patrice Mwamba
- Andre Masalu
- Joëlle Bile
- Enoch Ngila
Mbinu ya kupiga kura
Tangu kubadilishwa kwa ibara ya 71 ya Katiba inayohusiana na mbinu ya upigaji kura wa urais na kupitishwa kwa sheria mpya kabla ya uchaguzi wa urais wa 2011, Rais wa Jamhuri sasa anachaguliwa kwa kura nyingi zilizopigwa.
Muhula ni wa miaka miaka mitano ambao anaweza kuupata kwa kupata kura zaidi na sio lazima apate wingi wa kura kamili katika awamu ya pili.
Uchaguzi hufanyika siku tisini kabla ya kumalizika kwa mamlaka ya Rais wa sasa.
Mwaka huu, uchaguzi wa urais katika duru moja utaambatana na uchaguzi wa manaibu wa kitaifa na mikoa pamoja na ule wa madiwani wa manispaa.

Masuala makuu ya uchaguzi huu wa urais

Chanzo cha picha, AFP
Vyama vya upinzani vinaishuku serikali kwa kutaka kupanga udanganyifu katika uchaguzi. Wanaishutumu serikali kwa kuzuia uhuru na nafasi ya kidemokrasia; tuhuma ambazo wale waliopo madarakani wanazikana.
Hakikisho la mara kwa mara kutoka kwa Tume Huru ya Kitaifa ya Uchaguzi (CENI) halijafaulu kuondoa wasiwasi wa upinzani.
Maaskofu wa Kanisa Katoliki waliokusanyika katika Baraza la Kitaifa la Maaskofu wa Congo (CENCO) na viongozi wa Kanisa la Kristo nchini Congo (ECC) hivi karibuni walisema wana wasiwasi swa na wa upinzani.
Katika kiwango cha kijamii, athari za janga la Covid 19 na vita nchini Ukraine vinaendelea kuleta athari kwa familia. Mfumuko wa bei umepunguza uwezo wa kununua kwa wananchi wa kawaida ambao sasa wanapaswa kulipia zaidi mahitaji ya kimsingi.
Kulingana na takwimu rasmi, faranga ya Congo imeshuka thamani kwa karibu 15% hadi 20% dhidi ya dola tangu mwanzo wa mwaka.
Nchini DRC, theluthi mbili ya takriban wakazi milioni 100 wanaishi chini ya mstari wa umaskini, uliowekwa kuwa dola 2.15 kwa siku na Benki ya Dunia.
Rais anayemaliza muda wake Felix Tshisekedi amezindua mipango kadhaa kwa lengo la kuwaondolea watu mateso.
Mpango wa elimu ya msingi bila malipo na huduma za afya bila malipo kwa wanawake wanaojifungua katika vituo vya umma ni sehemu ya mipango hii.
Hata hivyo, maoni yanasalia kugawanyika kuhusu ufanisi wa mipango hii kote DRC.
Mgogoro wa usalama unaoendelea mashariki mwa nchi

Chanzo cha picha, Getty Images

Chanzo cha picha, AFP
Licha ya majimbo ya Kivu Kaskazini na Ituri kuzingirwa kwa karibu mwaka mmoja, hali ya usalama inasalia kuwa ya wasiwasi katika eneo hili la nchi.
Makundi ya waasi kama vile March 23 Movement (M23) (M23), Allied Democratic Forces (ADF) na CODECO yanaendelea kufanya mashambulizi dhidi ya maeneo ya raia na ya kijeshi.
Matokeo: DRC ni miongoni mwa nchi zenye idadi kubwa zaidi ya wakimbizi wa ndani duniani, ikiwa na karibu watu milioni 6.3 kulingana na ripoti ya Umoja wa Mataifa ya mwezi Machi 2022. Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa kiwango cha watu walio katika hali ya kulazimishwa kuhama kinaongezeka, wanafunzi kati yao wakiwa ni 28% katika jimbo la Kivu Kaskazini na 39% katika jimbo la Ituri.
Vyanzo vingine vya mvutano vimeibuka kutokana na migogoro baina ya jamii, hasa katika jimbo la Tshopo, Kaskazini-Mashariki, na katika jimbo la Maï-Ndombe, Kusini-Magharibi mwa nchi.
Ukosefu wa usalama unahatarisha kutatiza upigaji kura katika sehemu fulani za eneo la kitaifa.
Mnamo Novemba 2023, tume ya uchaguzi ilitangaza kuwa imepoteza takriban mawakala thelathini kwa waliokufa maji na kushambuliwa na vikundi vilivyojihami wakati wa usajili wa wapigakura.
Je, MONUSCO imeshindwa?
Hivi majuzi serikali ya Kongo ilidai kuondoka kwa wanajeshi kutoka nchi za Afrika Mashariki ifikapo mwisho wa mwaka, ikizishutumu kwa kushindwa kukomesha harakati za makundi yenye silaha chini ya 'mwaka mmoja baada ya kupelekwa katika nchi hiyo.
Kwa sasa, DRC iko katika mazungumzo kamili na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika, SADC, kwa uwezekano wa kupeleka vikosi vya kijeshi vya nchi za kanda hiyo.
Wakati huo huo, jeshi la Congo na walinda amani wa Umoja wa Mataifa wanaendelea na operesheni za kijeshi katika maeneo yanayokumbwa na ukosefu wa usalama katika jaribio la kurejesha mamlaka ya serikali.
Shirika na uchunguzi wa mchakato wa uchaguzi

Chanzo cha picha, CENI
Tume Huru ya Kitaifa ya Uchaguzi (CENI) ni taasisi inayounga mkono demokrasia. Ni chombo cha sheria za umma, kinachojiendesha, cha kudumu, kisichoegemea upande wowote na kilichopewa mamlaka ya kisheria.
Inaundwa na wanachama 21, jukumu lake ni "kuhakikisha uchaguzi huru na wa kidemokrasia".
CENI hivi majuzi imekuwa ikikashifiwa na wakosoaji wanaomtuhumu rais wake kwa kile wanachoelezea kama "ukaribu" na mamlaka iliyopo madarakani.
Wanasema wanahofia kuwa Mwenyekiti wake Denis Kadima anatoka katika kabila moja na rais anayeondoka, Félix Tshisekedi, kutaathiri uadilifu wa matokeo ya urais.
Kwa upande wake, Bw. Kadima amerudia mara kwa mara kuwa taasisi yake ina nia ya kuandaa uchaguzi kwa uwazi kabisa, huku ikiheshimu misingi ya kidemokrasia.
Katika siku za nyuma, Umoja wa Afrika, madhehebu ya kidini na mashirika ya kiraia wamelazimika kupeleka waangalizi kufuatilia kwa karibu maendeleo ya kura nchini DRC.
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi
Uhariri na Seif Dzungu












