Uchaguzi wa DRC 2023: Félix Tshisekedi, mwanafikra aliyetaka kuibadilisha DRC kuwa nchi ya ndoto

Chanzo cha picha, Getty Images
Cherif Ousman MBARDOUNKA
Mwandishi wa habari -BBC Africa
Kuingia mamlakani kwa Rais Tschisekedi mwaka 2019 kuliibua matumaini makubwa kwani yalikuwa ni makabidhiano ya kwanza ya amani ya madaraka kuwahi kushuhudiwa nchini DRC baada ya uhuru.
Sababu nyingine ya matumaini haya ya watu wa Congo, ni kwamba rais wa 5 alikuwa ni mtoto wa "mpinzani wa kihistoria" na mwanzilishi mashuhuri wa chama cha Union for Democracy and Social Progress (UDPS) , Étienne Tshisekedi wa Mulumba.
Kwa mujibu wa mtaalamu wa siasa katika Chuo Kikuu cha Katoliki cha Graben, Gaucher Kizito "mwanasiasa huyu alifaidika na bado anafaidika na umaarufu wa baba yake."
Kama jibu kwa matarajio ya raia, Félix Tshisekedi alitoa ahadi kadhaa kuanzia kupunguza ukosefu wa ajira hadi vita dhidi ya ukosefu wa usalama wa mara kwa mara mashariki mwa nchi, ikiwa ni pamoja na vita dhidi ya ufisadi.
Miaka mitano baadaye, tunashauri upitie upya miradi mikubwa ya Rais Tshisekedi, katika kuwania muhula wa pili.
Mapambano dhidi ya makundi yenye silaha

Chanzo cha picha, Getty Images
Januari 24, 2019, Félix Tshisekedi aliapishwa kuwa rais wa tano wa DRC.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Katika hotuba yake kwa ajili ya tukio hilo, aliahidi kurejesha mamlaka ya Serikali, kupambana na kufanya kila liwezekanalo ili kuleta usalama wa kitaifa.
Miaka mitano baadaye, Rais Tshisekedi alitoa hotuba nyingine, wakati huu, kuhusu hali ya taifa.
Alirejea katika tathmini yake, pamoja na mambo mengine, suala la ukosefu wa usalama mashariki mwa nchi.
Katika jaribio la kuyalazimisha makundi yenye silaha yanayoendesha harakati zao mashariki mwa nchi hiyo kuweka chini silaha, Rais Félix Tshisekedi alitangaza hali kuzingirwa katika majimbo ya mashariki ya Ituri na Kivu Kaskazini mwaka 2021.
Tangu wakati huo, jeshi lilifanya mabadiliko ya viongozi katika maeneo husika, ili kuwa na nguvu zaidi ya kukabiliana vyema wanamgambo.
Alipokabiliwa na wabunge mnamo Novemba 14, rais-mgombea alikadiria kuwa hali ya kuzingirwa iliruhusu mamlaka kuwafurusha washirika wa makundi yenye silaha na kuzuia vyanzo vyao vya fedha.
"Utawala huu wa kipekee umewezesha uboreshaji wa hali ya usalama katika baadhi ya maeneo ya mikoa miwili inayohusika, hasa kupunguza uporaji wa madini na ambao unachochea migogoro, kupunguza mvutano wa jamii na utulivu kwa kuanzishwa tena kwa mamlaka ya serikali katika maeneo haya," alisema.
Hata hivyo, vyama vya upinzani pamoja na asasi za kiraia vimekosoa vikali ufanisi wa hatua hiyo. Kivu Security Barometer (KST, Kivu Security Tracker) ni jukwaa la kufuatilia ghasia katika mikoa ya Ituri na Kivu Kaskazini.
Jukwaa hilo lilidai kuwa limeshuhudia matukio ya vurugu yaliyofanywa na vikosi vya usalama vya serikali na makundi yenye silaha katika majimbo yaliyo chini ya hali ya kuzingirwa.
Na siku hiyo hiyo ya hotuba ya Rais Tshisekedi kwa wabunge, shirika la habari la AFP lilitangaza kunyakuliwa tena kwa kijiji cha Kishishe na waasi wa M23 ambao walituhumiwa kufanya mauaji mwishoni mwa mwezi Novemba 2022 yaliyosababisha vifo vya watu 170 kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.
Waasi hawa, ambao wanadaiwa kusaidiwa na Rwanda, madai ambayo yanakanushwa na serikali ya Kigali, walijiondoa katika kijiji hicho mwanzoni mwa mwezi Aprili, wakati walipokuwa wakiondoka maeneo mengine katika mkoa wa Kivu Kaskazini ambao walikuwa wameuteka mwaka uliopita.
Baada ya miezi sita ya utulivu, mapigano yalianza tena mwanzoni mwa mwezi Oktoba katika Kivu Kaskazini kati ya waasi wa M23 na jeshi la Congo (FARDC) linaloshirikiana na makundi yenye silaha yanayojitambulisha kama "patriots". Ghasia hizi mpya zimesababisha watu 200,000 kuyakimbia makazi yao kwa mujibu wa makadirio ya Umoja wa Mataifa.
Upande wa kaskazini kidogo, katika eneo la Beni, jeshi la Congo na vikosi vya Uganda vinaendelea kuwasaka waasi wa ADF. Muungano kati ya jeshi la nchi hizo mbili ulifanikiwa kuwasukuma waasi mbali na vituo vya idadi ya watu na kuwaachia huru mamia ya mateka. Ingawa mashambulizi ya vikosi vya Allied Democratic Forces, ADF, hayajatokomezwa kabisa, uwezo wao wa kusababisha madhara umepungua kwa kiasi kikubwa.
Katika ngazi ya kidiplomasia, michakato mbalimbali ya amani inayoungwa mkono na nchi za kikanda bado inajitahidi kutoa matokeo yaliyotarajiwa.
Elimu ya msingi na kujifungua bure
Katika sekta ya kijamii na kiuchumi, Félix Tshisekedi anaweza kujivunia kuwa ameanzisha utoaji wa elimu ya msingi ya bure mnamo Septemba 2019. Kwa kweli lilikuwa moja ya mambo muhimu ya mpango wake kwa kijamii.
Kwa mujibu wake, idadi ya wanafunzi walioandikishwa kwenda shule imeongezeka kwa zaidi ya milioni 5 kutokana nautoaji wa elimu ya msingi bila malipo.
"Katika juhudi za kuboresha elimu na utekelezaji wa elimu ya msingi bila malipo, shule 1,230 zilijengwa kama sehemu ya Mpango wa Maendeleo ya Mitaa katika wilaya 145," alisema.
Félix Tshisekedi pia meafiki uzinduzi wa mpango wa msaada wa elimu bure unaoitwa: "Sio shule bila benchi."
Bw shisekedi alielezea kuwa serikali yake imeongeza bajeti iliyotengwa kwa ajili ya elimu kwa asilimia 9.1 kutoka 2021 hadi 2022 na kwa mwaka 2022 hadi 2023, kwa asilimia 23.9 ili kusaidia utoaji wa elimu bila malipo.
"Kwa kipindi hiki cha miaka mitano, wastani wa mshahara wa mwalimu uliongezeka kutoka 159,662.67 FC hadi 408,689.67 FC," aliongeza.
Hata hivyo, baadhi ya wadau katika sekta ya elimu wana mashaka kuhusu mpango huu, wakitaja msongamano wa madarasa katika baadhi ya maeneo na ugumu wa shule kuendelea kuwapa motisha walimu wengine.
Mwaka 2020, uchunguzi uliofanywa na Mkaguzi mkuu wa Fedha, chombo cha kupambana na rushwa kilichowekwa chini ya mamlaka ya moja kwa moja ya rais, kililaani udanganyifu katika sekta ya elimu. Hatua hiyo ilisababisha kukamatwa na kushtakiwa kwa maafisa wa ngazi za juu.
"Tulionyesha kwamba kulikuwa na shule za gushi, kwamba kulikuwa na wafanyakazi wa hewa, na ninaamini kwamba kazi hii ilikamilika, mamlaka za sekta ya elimu zilihojiwa na mahakama na baadhi yao walihukumiwa kifungo cha miaka 20 jela. Bado wako gerezani," anaeleza Jules Alingete, Mkaguzi Mkuu wa Fedha katika mahojiano na BBC.
Kwa mtaalamu wa masuala ya siasa Gaucher Kizito, utoaji wa elimu msingi bure ni jambo ambalo mkuu wa nchi anaweza kulitumia kujinadi na kuweza kushinda kiti cha urais. Aliongeza kuwa mamia ya vijana pia wananufaika kwa mpango wa udhamini elimu unaofahamika kama Excellentia ulioanzishwa na mke wa rais Denise Nyakeru Tshisekedi.
Kutokana na udhamini huo, vijana takribani mia moja wanasoma katika shule mbalimbali nchini huku wengine kadhaa wakipelekwa kuendelea na masomo yao nje ya nchi.
Mnamo Septemba 2023, Rais Felix Tshisekedi alizindua mpango wa kujifungua bila malipo katika hospitali za umma. Katika nchi ambayo wanawake kadhaa mara nyingi hushikiliwa hospitalini na watoto wao kwa kushindwa kulipia garama ya matibabu , hatua hii ilileta ahueni kwa wanawake.
Kila mwaka, Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu, UNFPA, hutoa zaidi ya dola milioni 7 kusaidia serikali katika uzazi wa mpango pamoja na dawa za kuokoa maisha kwa wanawake na watoto wachanga.
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa linabainisha kuwa bado kuna haja ya kuimarisha mfumo wa afya wa nchi na mitandao ya huduma za dharura za uzazi na watoto wachanga pamoja na kupelekwa kwa wafanyikazi wenye ujuzi na wenye uwezo katika maeneo yote ya nchi.
"Ni muhimu kuhamasisha rasilimali kubwa za kifedha, vifaa na rasilimali watu ili kusaidia huduma hii ya bure. Ni kwa sababu hii ambapo UNFPA inatetea uimarishaji wa rasilimali kwa ajili ya afya ya mama, mtoto mchanga kote DRC," inaeleza taarifa kutoka shirika la Umoja wa Mataifa.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa upande wa sekta ya uchumi, wakati Wakongo wakilalamika juu ya kuporomoka kwa faranga ya Congo ambayo ina athari kubwa katika maisha yao ya kila siku, Rais Tshisekedi hivi karibuni alielezea kuimarika upya kwa uchumi wa taifa.
"Niwahakikishie kuwa uchumi wetu wa mwaka 2023 uko katika hali nzuri.
Tumepitia kipindi kigumu mwaka 2020, kukabiliana na changamoto zinazosababishwa na janga hili kufikia viwango vya ukuaji wa uchumi unaoashiria
Hata kama anatambua kwamba juhudi bado zinahitajika kufanywa katika kuimarisha haki na uhuru, mrithi huyo wa Joseph Kabila katika Palais de la Nation anaomba kura katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika tarehe 20 Disemba.
"Kwa hivyo tuna chaguo kati ya kuanzia mwanzo au kuimarisha mafanikio ya kasi hii ya maendeleo kwa kusonga mbele, na maono ya wazi, kuelekea siku zijazo ambapo Wakongo wote watapata fursa ya kufanikiwa. " ilieleza Ahadi mpya au kauli mbiu ambayo ilizindua kampeni yake.
Washirika wakuu wa Tshisekedi ni akina nani?
Katika uchaguzi wa rais utakaofanyika Desemba 20, Félix Tshisekedi atategemea uungwaji mkono wa Jean-Pierre Bemba, Naibu Waziri Mkuu wa sasa anayesimamia masuala ya ulinzi na Vital Kamerhe, Naibu Waziri Mkuu anayesimamia masuala ya uchumi.

Chanzo cha picha, Getty Images
Mbabe wa zamani wa kivita Jean-Pierre Bemba pia ameahidi "kufanya kila linalowezekana ili kufanikisha ushindi wa rais anayeondoka.
Chama chake, Chama cha Ukombozi wa Kongo (MLC) ni sehemu ya muungano wa vyama vya kisiasa vinavyounga mkono mgombea wa Rais Félix Tshisekedi.
Ni wakati wa mkutano mkuu wa chama chake cha siasa uliofanyika Jumamosi Septemba 30, 2023 ambapo Jean-Pierre Bemba alifichua kumuunga mkono Félix Tshisekedi.
"MLC kinathibitisha uanachama wake katika Umoja Mtakatifu wa Taifa, kama shahidi wa upendeleo wake kwa Mkuu wa Nchi Félix Tshisekedi kubadilisha sana jamii yetu kuongoza nchi yetu kuelekea maendeleo, kuhakikisha usalama wake na kuweka amani ndani ya mipaka yetu, ndio maana niliamua kutogombea ili kumuunga mkono ndugu yetu Félix-Antoine Tshisekedi Tshilombo, Jean-Pierre Bemba Gombo, rais wa chama cha MLC.
Vital Kamerhe

Chanzo cha picha, Getty Images
Sawa na Jean-Pierre Bemba, Vital Kamerhe pia ni mshirika mkubwa wa Rais Tshisekedi.
Mwezi Agosti mwaka jana, Muungano wa Vital Kamerhe kwa ajili ya Taifa la Congo (UNC) uliamua kuunga mkono azma ya Félix Tshisekedi kuwania urais katika uchaguzi wa urais mwezi Desemba 2023.
Kwa wanachama wa UNC, ni muhimu kukamilisha vitendo vyote vya mpango wa pamoja iliyoundwa na UDPS. Hata hivyo, mnamo 2018, pande hizo mbili zili[kamilisha makubaliano jijini Nairobi kulingana mbapo kwa mujibu wake Félix Tshisekedi angegombea 2018 na Kamerhe mnamo 2023.
Mbele ya waandishi wa habari wakati wa mkutano wa Agosti 19, Vital Kamerhe alielezea kuwa ni "chaguo la moyo na mantiki, kwa sababu uwezo wetu mkubwa wa kubadilisha mambo unategemea imani yetu katika siku zijazo.
"Tunafahamu kazi kubwa inayomsubiri Rais wa Jamhuri. Lakini tunajua kwamba tunaweza kutegemea uamuzi wake wa kubeba mwenge wa matarajio yetu ya kitaifa hata zaidi," aliongeza.
Hata hivyo, mchambuzi Gaucher Kizito anaamini kuwa suala la msingi la muungano kati ya Bemba, Kamerhe na Tshisekedi ni "kugawana nafasi na majukumu, hasa katika ngazi ya serikali" wakati atakapopata ushindi. Hii itategemea, kulingana na yeye, "uzito ambao kila chama cha siasa kitawakilisha kwa idadi ya manaibu na meya.
Wakati wa mkutano wa tarehe 1 Oktoba, UDPS, chama tawala na vyama vingine wanachama wa "Umoja Mtakatifu wa Taifa" walimtangaza rais anayeondoka kama mgombea wao.
Hata hivyo, Félix Tshisekedi amesajiliwa kama mgombea huru katika orodha iliyochapishwa na Ceni.
Ataondoka kwa muda katika uwanja wa kampeni kuiwakilisha DRC katika mkutano wa COP28. Wakati atakapoondoka washirika wa Muungano Mtakatifu wataendelea kufanya kampeni katika majimbo mbalimbali ya DRC kwa matumaini ya kushinda muhula wa pili.
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi












