Iran yasema inaweza kutengeneza silaha za nyuklia lakini haina mpango wa kufanya hivyo

Iran imekuwa ikisisitiza kuwa mpango wake wa nyuklia ni kwa madhumuni salama

Chanzo cha picha, Reuters

Mkuu wa nishati ya atomiki nchini Iran anasema kuwa nchi hiyo ina uwezo wa kutengeneza silaha za nyuklia lakini haina mpango wa kufanya hivyo, shirika la habari la Iran linaripoti.

Maoni ya Mohammad Eslami yanaangazia kauli kama hiyo ya hivi majuzi ya mshauri mkuu wa kiongozi mkuu wa Iran.

Madai kama haya ya umma ya maafisa wakuu ni nadra na yana uwezekano wa kuzidisha wasiwasi kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.

Imeendeleza shughuli zake za nyuklia tangu makubaliano ya kuziwekea vikwazo kudorora.

Makubaliano ya mwaka 2015 yalianza kusambaratika wakati Marekani ilipojiondoa na kurejesha vikwazo vya kiuchumi vilivyokuwa vimedhoofisha.

Iran imekuwa ikidai mara kwa mara mpango wake wa nyuklia ni kwa madhumuni ya amani tu lakini mataifa yenye nguvu ya Magharibi na shirika la kimataifa la uangalizi wa nyuklia wanasema hawajashawishika.

Maafisa wa nchi za Magharibi wameonya kuwa muda unazidi kuyoyoma kurejesha mapatano hayo kabla ya mpango wa Iran kufikia hatua ambayo hauwezi kutenguliwa.

Mpango wa nyuklia wa Iran: Picha ya Setilaiti inayoonesha shughuli za nyuklia nchini Iran
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Katika matamshi yake yaliyoripotiwa Jumatatu na shirika la habari la Fars, Bw Eslami alisisitiza maoni yaliyotolewa na mshauri mkuu, Kamal Kharrazi.

"Kama Bw Kharrazi alivyotaja, Iran ina uwezo wa kiufundi wa kutengeneza bomu la atomiki, lakini mpango kama huo hauko kwenye ajenda," Bw Eslami alisema.

Katika hotuba yake mwenyewe aliyoitoa kwa kituo cha habari cha Al Jazeera tarehe 17 Julai, Bw Kharrazi alisema: "Iran ina mbinu za kiufundi za kuzalisha bomu la nyuklia lakini hakujawa na uamuzi wa Iran wa kulijenga."

Kumekuwa na wasiwasi juu ya muda ambao itachukua Iran kukusanya uranium iliyorutubishwa ya kutosha kwa silaha ya nyuklia.

Mwezi Juni, mkuu wa wakala wa kimataifa wa nishati ya atomiki, Rafael Grossi, alisema Iran inaweza kupata kiasi hicho katika muda wa wiki chache.

Marekani iliweka muda wa takriban mwaka mmoja katika kipindi ambacho makubaliano ya nyuklia yalikuwa sawa.

Hata hivyo Bw Grossi alisema kuwa na nyenzo za kutosha haimaanishi kuwa Iran inaweza kutengeneza bomu la nyuklia.

Katika ripoti yake ya hivi punde mwezi Mei, IAEA ilisema Iran ilikuwa na kilo 43.1 (lb 95) za uranium iliyorutubishwa hadi asilimia 60 . Takriban kilo 25 za uranium iliyorutubishwa hadi 90% inahitajika kwa ajili ya silaha ya nyuklia.

Madai kutoka Iran kwamba ina ujuzi wa kiufundi wa kutengeneza bomu yamekuja wakati Iran na mataifa yenye nguvu duniani yanazozana kuhusu kufufua mkataba wa mwaka 2015.

Mazungumzo ya muda wa miezi kadhaa mjini Vienna yamekwama, na mazungumzo nadra yasiyo ya moja kwa moja kati ya Marekani na Iran kuhusu suala hilo yaliyofanyika Qatar mwezi Juni yalimalizika bila makubaliano.

Urutubishaji wa madini uranium ni nini?

Madini ya Uranium yaliorutubishwa hutengenezwa kwa kuweka gesi ya uranium hexafluoride ndani ya mashine ya kuzunguka ijulikanayo kama centrifuges kwa lengo la kutenganisha viini muhimu vya kutengeneza nyuklia vijulikanavyo kama U-235.

Chini ya mkataba huo makubaliano ya nyuklia , Iran inaruhusiwa kutengeneza kiwango kidogo cha madini yaliorutubishwa ya uranium yalio na asilimia kati ya 3- 4 ya U-235, na yanaweza kutumika kutengeneza nishati kwa vinu vya nyuklia.

Viwango vya kutengeneza silaha-ni 90% ya uranium iliyorutubishwa au zaidi.

Makubaliano hayo pia yanaizuia Iran kuweka akiba inayozidi 300kg ya madini hayo yaliyorutubishwa kwa kiwango kidogo.

Iran imekuwa ikikana inarutubisha madini hayo kwa minajili ya kujenga zana za nyuklia.

Kwanini kuna umuhimu wa kuwa na ukomo wa urutubishaji madini ya uranium?

Mwaka 2015,Iran iliingia kwenye makubaliano kuhusu mradi wa nyukilia sambamba na mataifa yenye nguvu duniani-Marekani,Uingereza, Ufaransa,China,Urusi na Ujerumani.

Chanzo cha picha, AFP

Waangalizi wanasema kuwa urutubishaji wa madini ya uranium kunaweza kufupisha muda unaohitajika kutengeneza bomu la nyuklia.Iran inasisitiza kuwa mpango wake wa nyuklia ni wa amani.

Hata hivyo, mashaka ya kuwa Iran huenda inatengeneza bomu la nyuklia kisiri yalifanya Umoja wa Ulaya, Marekani na Umoja wa Mataifa kuiwekea Iran vikwazo mwaka 2010.

Makubaliano ya mwaka 2015 yaliyotiwa saini na China, Ufaransa, Ujerumani, Urusi Uingereza na Marekani yalifikiwa ili kusitisha mpango huo kwa mabadilishano ya Iran nayo iondolewe vikwazo.