Daktari aliyepoteza kumbukumbu ya miaka 12 ya maisha yake baada ya ajali

c

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Baada ya ajali mbaya, akili ya Dk Pier Piccioni iliganda miaka 12 nyuma.
    • Author, Jo Fidgen & Edgar Maddicott
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Dk. Pierdante (Pier) Piccioni, alizinduka Mei 31, 2013, katika kitanda cha hospitali kaskazini mwa Italia. Pier alikuwa mkuu wa chumba cha dharura, lakini siku hiyo aliamka kama mgonjwa, saa chache baada ya ajali mbaya ya gari.

"Nilikosa fahamu kwa muda wa saa sita, nilipozinduka, wenzangu wakaniuliza, 'unaitwa nani?' Nilijaribu kujibu kwa tabu.

"Na walipouliza: Leo ni siku gani? Nilifikiria kwa sekunde 5-6 na kujibu, 'Oktoba 25, 2001.”

"Wakaniuliza: 'Ni siku gani katika wiki?

"Nilijibu: 'Alhamisi.'

Madaktari walikagua na kuthibitisha Oktoba 25, 2001, ilikuwa ni Alhamisi.

"Ilikuwa ajabu kwao kwamba nilikumbuka siku katika wiki kutoka miaka 12 iliyopita."

Kwa Pier, Alhamisi hiyo miaka 12 iliyopita ilikuwa sasa. Madaktari wake walishangaa, lakini hawakumwambia chochote kwa wakati huo. Walichokifanya ni kumuuliza kama anataka kumuona mkewe.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

"Mwanamke aliyeingia alikuwa kama mke wangu, lakini ana mikunjo mingi, nywele tofauti, miwani... alikuwa tofauti kabisa.

"Kisha watoto wangu wakaingia - ambao katika akili yangu walikuwa na umri wa miaka 8 na 11 – lakini waliingia wakiwa watu wazima wawili, wa miaka 20 na 23!"

"Mmoja wa madaktari wawili alikuwa rafiki yangu, nilimkumbuka akiwa kwa nywele zake, lakini hakuwa nazo tena.

"Sikuelewa nini kimetokea, kwa nini ulimwengu umebadilika sana. Lakini ukweli ni kwamba ni mimi ndiye niyebadilika: nimepoteza kumbukumbu ya miaka 12 ya maisha yangu."

Pier aligundua pale siku iliyofuata, alipoona picha yake kwenye ukurasa wa mbele wa makala ya gazeti la ndani kuhusu ajali mbaya iliyohusisha mkuu wa chumba cha dharura.

"Tarehe ni Juni 1, 2013.

"Nilijisemea, 'Huu si mzaha, ni jeraha la ubongo, na haya ndiyo matokeo yake.'

"Simu niliyokumbuka iliniruhusu kupiga simu na kutuma ujumbe mfupi, lakini mitandao yote ya kijamii kama Instagram na Messenger, na simu ya kisasa, yalikuwa mambo mapya."

Mashimo kwenye ubongo

d

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mbali na kurejea kazini kwake kama daktari, Pier ameandika vitabu kadhaa tangu kupona kwake.

Mkewe Maria Assunta Zanetti, wanawe Filippo na Tommaso, marafiki zake na wafanyakazi wenzake. Hakukumbuka jinsi alivyokuwa mkuu wa Idara ya Dharura.

"Miezi kadhaa baadaye, baada ya vipimo, tuliona athari ya ajali: kulikuwa na mashimo kwenye ubongo wangu. Maeneo ambayo kuna mashimo labda ndio huhifadhi kumbukumbu ya muda mrefu.”

Pier alifanyiwa kila mtihani na utaratibu wa kujaribu kurejesha kumbukumbu zake. Alijaribu vidonge na tiba, hata matibabu ya kuushitua ubongo, lakini hakuna kilichofanya kazi.

"Kwa nini uendelee kuishi? Nilifikiria kujiua."

Kwa bahati nzuri, mkewe alikuwa pamoja naye wakati wote akijaribu kumsaidia. "Ilikuwa vigumu sana mwanzoni. Alijaribu kunieleza mambo mengi yaliyotokea, lakini hizo zilikuwa kumbukumbu zake, si zangu."

Lakini alikumbuka kwamba alimpenda au alisahau hisia hizo pia?

Pier anakiri kwamba mara ya kwanza mkewe alipomtembelea hospitalini, aliposhtushwa na kupita kwa miaka usoni mwake. Lakini kuna kitu kilitokea alipokuwa akiondoka.

"Aligeuka na nikamwona nyuma na nikasema, 'Wow, ni mrembo!'

"Nilimpenda, alikuwa kama mtu mwingine na nilipenda tena..!"

"Watoto wangu walianza kunipenda. Ilikuwa rahisi kwao kwa sababu walikuwa na kumbukumbu zao zote."

"Ilinichukua miaka mitatu ya maisha yangu baada ya tukio hilo kuelewa jinsi ya kubadilisha hasira kuwa fursa.

"Haikuwa rahisi, lakini nilifanya juhudi kurudi kusomea taaluma yangu na kusikiliza familia na marafiki zangu."

Nilikuwa nani?

c

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kilichomtokea Pier kimerikodiwa katika tamthilia. Mwigizaji Pierpaolo Spollon, akiwa ameshikilia picha ya mwigizaji anayeigiza kama Pier, Luca Argentero.

Swali ambalo Pierre alikuwa nalo kwa familia yake, marafiki na wafanyakazi wenzake lilikuwa yeye ni mtu wa aina gani. "Alikuwa mtu mzuri au mbaya?

"Wafanyakazi wenzangu waliniambia nilipokuwa mkuu wao, nikisimamia watu wapatao 230, jina langu la utani lilikuwa The Bastard Prince."

Ni kwa sababu "alikuwa muungwana katika matusi yake." "Kwamba nilikuwa kama almasi: mwenye nguvu sana, sahihi sana, lakini mkali sana kwa watu wengine."

Alichokifanya Pier ni kupekuwa barua pepe zote alizokuwa ameandika katika miaka ambayo hakuweza kukumbuka.

"Nilisoma barua pepe zote, zaidi ya 76,000, kujaribu kuelewa nilikuwa nani.

"Katika baadhi ya barua pepe, nilipata uthibitisho kwamba nilikuwa bosi na nilikuwa mkali, na nilihuzunika."

Miaka miwili baadaye, Pier anasema, mfanyakazi mwenzake alimwambia: "Ikiwa tungejua kwamba pigo la kichwa lingekufanya kuwa mtu bora, tungekupiga mapema."

Kurejesha kilichopotea

f

Chanzo cha picha, Getty Images

Miaka kumi na miwili baada ya ajali hiyo, Pier hajapoteza matumaini ya kurejesha kumbukumbu zake zilizopotea, lakini anasema, "nimejifunza jambo moja muhimu: ikiwa unataka kuishi, huwezi kuendelea kufikiria juu ya siku za nyuma, fikiria kuhusu siku zijazo."

Akiwa amesahau sehemu ya maisha yake ya zamani; “ilinibidi nianze kujenga upya maisha yangu, si kwa kumbukumbu zangu, bali na za mke wangu, marafiki zangu, watoto wangu.

"Wakati mmoja nilionyeshwa picha ya mtu mrefu mweusi, na nilipoambiwa ni Rais wa Marekani, nilifikiri haiwezekani."

Ilikuwa, bila shaka, Barack Obama. Pier hakukumbuka uchaguzi wake.

"Ulimwengu mpya umekuwa bora zaidi kuliko ule wa zamani.

"Ninajivunia kuishi katika aina tofauti ya ulimwengu, ulimwengu ambao, wanawake katika taaluma yangu wanafikia viwango vya juu zaidi kuliko hapo awali, na hiyo ni muhimu sana."

Ilimchukua miaka miwili na nusu, kabla ya kurudi kuwa daktari tena, licha ya kuwa na jeraha kama hilo la ubongo.

"Ilinibidi kupitia vipimo zaidi ya 63 vya kiufundi, kisaikolojia na mazingira ili kudhibitisha kuwa niko sawa kuwa daktari tena.

Ufunguo mwingine wa mabadiliko yake, anasema, ilikuwa ni "kutunza kijarida. Niliandika kile nilichoona ni muhimu kwangu au mambo ya kijinga kuhusu siku yangu, kuhusu maisha yangu."

Shajara hiyo ya safari yake kati ya maisha ilikuwa msingi wa kumbukumbu katika kitabu kilichochapishwa kwa Kiitaliano chini ya kichwa " Meno Dodici " na kitabu hicho kikawa msingi wa mfululizo wa tamthilia ya KiItaliano ya Doc Nelle tue nami.

"Ninapoamka, nahisi umri wangu ni miaka 53; wakati wa mchana nagundua nina miaka 65."

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi