Kufariki dunia pamoja: Kwa nini wanandoa hawa waliamua kukatiza maisha yao

Na, Linda Pressly, BBC News

Jan na Els walikuwa wameoana kwa karibu miongo mitano. Mwanzoni mwa mwezi Juni, walifariki pamoja baada ya kupewa dawa za kuwasaidia kufariki na madaktari wawili. Huko Uholanzi, hii inajulikana kama ‘duo-euthanasia’. Inaruhusiwa kisheria, na ni nadra sana kutokea - lakini kila mwaka, wanandoa zaidi wa Uholanzi huchagua kukatisha maisha yao pamoja kwa njia hii.

Onyo: Baadhi ya watu wanaweza kuona makala hii kuwa yenye kufadhaisha

Siku tatu kabla ya kukatiza maisha yao kwa hiari, Jan na Els wanandoa waliopenda kusafiri waliketi pamoja na mwanahabari wa BBC, eneo la Friesland, kaskazini mwa Uholanzi. Muda mwingi waliishi katika makazi yao yaliotengenezwa kwenye magari, au kwenye boti.

"Tulijaribu wakati mwingine [kuishi] kwenye rundo la mawe – kwa kuifanya kama nyumba," anatania Jan, "lakini haikuwezekana."

Ana umri wa miaka 70, na amekaa katika kiti kinachozunguka cha gari, mguu mmoja ukiwa umeinama chini yake katika mkao pekee unaopunguza maumivu yake ya mgongo aliyonayo. Mkewe, Els, ana umri wa miaka 71 na ana matatizo ya akili. Alikuwa na wakati mgumu kuzungumza maneno yake.

"Hii ni nzuri sana," anasema, akisimama kwa urahisi na kuelekeza mwili wake. "Lakini ni mbaya," anaongeza, akiashiria kichwa chake.

Jan na Els walikutana katika shule ya chekechea – wao ulikuwa ushirikiano wa milele. Alipokuwa mdogo, Jan alicheza mpira wa magongo katika timu ya taifa ya vijana ya Uholanzi, kisha akawa kocha wa michezo. Els alipata mafunzo ya kuwa mwalimu wa shule ya msingi. Lakini ulikuwa upendo wao wa majini, kwenye boti, na usafiri wa baharini ambao ulileta maana kipindi cha miaka yao pamoja.

Kama wanandoa wachanga waliishi kwenye nyumba ya mashua. Baadaye walinunua mashua ya kubeba mizigo na kuanzisha kile kilichojulikana kama biashara ya kusafirisha bidhaa kuzunguka njia za majini za Uholanzi.

Wakati huo huo, Els alijifungua mtoto wao wa pekee wa kiume (ambaye hakutaka kutajwa jina lake). Alisoma katika shule ya bweni ya kila wiki na alitumia wikendi kuwa na wazazi wake. Wakati wa likizo za shule mtoto wao walikuwa naye pia, Jan na Els walitafuta safari za kikazi ambazo zingewapeleka mahali pazuri - kando ya mto Rhine, au visiwa vya Uholanzi.

Kufikia mwaka 1999, biashara ya mizigo ya ndani ilikuwa na ushindani mkubwa. Jan alikuwa akipata maumivu makali ya mgongo kutokana na kazi ngumu aliyokuwa akifanya kwa zaidi ya muongo mmoja. Yeye na Els walihamia nchi kavu, lakini baada ya miaka michache walianza kuishi tena kwenye mashua. Hilo lilipozidi kuwa vigumu kulisimamia, walinunua gari lao waliloligeuza kuwa makazi.

Jan alifanyiwa upasuaji mgongoni mwaka wa 2003, lakini hali yake iliendelea kuwa mbaya. Alikuwa ameacha kutumia dawa za maumivu makali na hakuweza kufanya kazi tena huku Els akiwa bado anajishughulisha na kufundisha.

Wakati mwingine walizungumza kuhusu kusaidiwa kufariki dunia - Jan alielezea familia yake hakutaka kuishi kwa muda mrefu na mapungufu yake ya kimwili. Ilikuwa wakati huu wanandoa hao walijiunga na - shirika la kutetea "haki ya kufariki" la Uholanzi.

"Ikiwa unatumia dawa nyingi, unaishi kama mizimu," Jan anasema. "Kwa maumivu niliyo nayo, na ugonjwa wa Els, nadhani tunapaswa kumalizana na hili."

Wakati Jan anasema "kumalizana na hili", anamaanisha – kukatiza maisha yao.

Mnamo 2018, Els alistaafu kufundisha. Alikuwa akionyesha dalili za mapema za matatizo ya akili lakini alikataa kumuona daktari - labda kwa sababu alishuhudia kifo cha baba yake kutokana na ugonjwa wa Alzheimer. Lakini ilifika wakati dalili zake hazikuweza kupuuzwa tena.

Mnamo Novemba 2022, baada ya kugunduliwa kuwa na matatizo ya akili, Els alitoka nje ya chumba cha mashauriano cha daktari, akiwaacha mumewe na mwanawe.

"Alikuwa na hasira - kama fahali aliyetaka kupigana," anakumbuka Jan.

Ilikuwa baada ya Els kujua hali yake isingeimarika ndipo yeye na Jan, pamoja na mtoto wao wa kiume, walianza kujadili suala la wawili hao kusaidiwa kufariki dunia pamoja.

Nchini Uholanzi, kusaidiwa kufariki au kujiua ni halali ikiwa mtu atatoa ombi la hiari, na mateso wanayopitia - ya kimwili au ya kisaikolojia - yanatathminiwa na madaktari kuwa "hayawezi kuvumilika", bila matarajio ya kuboresheka. Kila mtu anayeomba kusaidiwa kufariki dunia anachunguzwa na madaktari wawili - wa pili akiangalia tathmini iliyofanywa na wa kwanza.

Mnamo 2023, watu 9,068 walisaidiwa kufariki dunia nchini Uholanzi - karibu 5% ya jumla ya idadi ya vifo. Kulikuwa na matukio 33 ya wanandoa kusaidiwa kufariki dunia. Baadhi ya matukio yanayofanya hali hii kuwa ngumu zaidi ni ikiwa mmoja wa washirika ana matatizo ya akili, ambapo kunaweza kuwa na kutokuwa na uhakika kuhusu uwezo wao wa kutoa idhini.

"Madaktari wengi hawataki hata kufikiria kumsaidia mgonjwa kufariki akiwa ana matatizo ya akili," anasema Dk Rosemarijn van Bruchem, daktari wa watoto na mtaalamu wa maadili katika Kituo cha Matibabu cha Erasmus, huko Rotterdam.

Huu ndio ulikuwa msimamo wa Jan na Els. Kati ya maelfu waliofariki dunia mnamo 2023, 336 walikuwa na matatizo ya akili.

Kwa hivyo madaktari hutathmini vipi hitaji la kisheria la "mateso yasiyoweza kuvumilika" kwa wagonjwa walio na matatizo ya akili?

Kwa wengi walio na matatizo ya akili hatua ya mapema, kutokuwa na uhakika juu ya jinsi mambo yanavyoweza kuendelea kunaweza kuwaongoza kufikiria juu ya kukatiza maisha yao, anaelezea Dk van Bruchem.

“Je, sitaweza kufanya mambo ninayoona kuwa muhimu? Je, sitaitambua familia yangu tena? Ikiwa unaweza kueleza hilo sawa sawa, ikiwa inawezekana kuwa na daktari ambaye yuko tayari kukusaidia kufariki, na pia daktari [wa pili] ambaye ni mtaalamu wa uwezo wa matatizo ya kiakili, hofu iliyopo ya kile kitakachokuja inaweza kuwa sababu ya kuzingatiwa katika kusaidiwa kufariki dunia.”

Katika tukio ambapo wanandoa wanataka kukatisha maisha yao pamoja, madaktari lazima wawe na uhakika kwamba mwenzi mmoja hamshawishi mwingine.

Dk Bert Keizer amehudhuria matukio mawili ya wanandoa kutaka kusaidiwa kufariki. Lakini pia anakumbuka alikutana na wanandoa wengine, aliposhuku kuwa mwanamume huyo alikuwa akimlazimisha mkewe. Katika ziara nyingine, Dk Keizer alizungumza na mwanamke peke yake.

"Alisema alikuwa na mipango mingi ...!" Dk Keizer anasema, akieleza kuwa mwanamke huyo alitambua wazi kwamba mumewe alikuwa mgonjwa sana, lakini hakuwa na mpango wa kufariki naye.

Mchakato wa kusaidiwa kufariki ulisitishwa na mwanaume akafariki dunia kutokana na sababu za asili. Mkewe bado yuko hai.

Jan na Els pengine wanaweza kuendelea kuishi kwa muda usiojulikana. Lakini Je, wanahisi wanaweza kufariki mada wowote hivi karibuni kwa njia ya asili?

"Hapana, hapana, hapana – sioni hilo likitokea," anasema Els.

"Nimeishi maisha yangu, sitaki maumivu tena," anasema mume wake. "Maisha ambayo tumeishi, tunazeeka. Tunafikiri lazima yasitishwe."

Na kuna kitu kingine. Els amefanyiwa tathmini na madaktari ambao wanasema bado ana uwezo wa kujiamulia kwamba anataka kufariki - lakini hii inaweza kubadilika ikiwa matatizo yake ya akili yataendelea kuongezeka.

Siku moja kabla ya miadi yao na madaktari wa kuwasaidia kufariki dunia, Els, Jan, mwana wao na wajukuu walikuwa pamoja.

Siku ya Jumatatu asubuhi, kila mtu alikusanyika hospitalini. Marafiki wakubwa wa wanandoa hao walikuwepo, kaka za Jan na Els, na binti-mkwe wao pamoja na mtoto wao wa kiume.

"Tulikuwa na saa mbili pamoja, kabla ya madaktari kuja," anasema. "Tulizungumza juu ya kumbukumbu zetu ... na tulisikiliza muziki."

“Nusu saa ya mwisho ilikuwa ngumu,” mwana wao alisema. "Madaktari walifika na kila kitu kilifanyika haraka - wanafuata utaratibu wao, na ni suala la dakika tu."

Els van Leeningen na Jan Faber walipewa dawa za kuwaua na madaktari na walifariki pamoja Juni 3, 2024.

Imetafsiriwa na Asha Juma