Wanajeshi wa Israel wanaendelea kutuma picha za unyanyasaji licha ya kuahidi kuchukua hatua

Chanzo cha picha, Instagram
Wanajeshi wa Israel wanasambaza picha za kukamatwa kwa Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa, licha ya ahadi ya jeshi kuchukua hatua dhidi ya utovu wa nidhamu wa hapo awali uliofichuliwa na BBC.
Wataalamu wa sheria wanasema upigaji picha huo, na uchapishaji wake mtandaoni, unaweza kuwa uhalifu wa kivita.
BBC imetathimini picha na video 45, ambazo ni pamoja na zile za wafungwa waliofunikwa bendera za Israel.
Jeshi la Ulinzi la Israel lilisema wanajeshi wameadhibiwa au kusimamishwa kazi kutokana na "tabia isiyokubalika".
Haikuzungumzia matukio binafsi au askari tuliowabaini.
Sheria ya kimataifa inasema wafungwa hawapaswi kuoneshwa fedheha isiyo ya lazima lakini wataalamu wa haki za binadamu wanasema kuchapishwa kwa picha za kizuizini hufanya hivyo.
Mnamo Februari, BBC Verify iliripoti kuhusu utovu wa nidhamu wa askari wa IDF kwenye mitandao ya kijamii wakati wa vita huko Gaza vilivyoanza baada ya shambulio la Oktoba 7 la Hamas dhidi ya Israel, ambalo liliua takribani watu 1,200.
Zaidi ya wengine 252 walichukuliwa mateka. Zaidi ya watu 34,000 wameuawa na Israel huko Gaza, wizara ya afya ya eneo hilo inayoendeshwa na Hamas inasema.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Wakati wa uchunguzi wetu wa awali, tuligundua na kuanza kuchunguza mtindo sawa wa tabia katika Ukingo wa Magharibi, ambao umekumbwa na ongezeko la vurugu katika kipindi hicho hicho.
Licha ya hapo awali BBC kuripoti kuhusu utovu wa nidhamu wa wanajeshi wa Israel kwenye mitandao ya kijamii, na baadaye jeshi kuahidi kufanyia kazi matokeo tuliyogundua, mwanajeshi wa zamani wa Israel, Ori Givati, anasema hajashtuka kusikia kwamba shughuli hii inaendelea.
Msemaji wa Breaking The Silence, shirika la wanajeshi wa zamani na wanaohudumu wa Israel ambao wanafanya kazi ya kufichua makosa yanayodaiwa kufanywa na Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF), Bw.Givati aliongeza kuwa kwa hakika anaamini kuwa matamshi ya siasa kali za mrengo wa kulia nchini humo yalichochea.
"Hakuna madhara. Wao (askari wa Israel) wanatiwa moyo na kuungwa mkono na mawaziri wakuu wa serikali," alisema.
"Utamaduni katika jeshi, linapokuja suala la Wapalestina, ni walengwa tu. Sio wanadamu. Hivi ndivyo jeshi linavyokufundisha tabia."
Israel imejenga takribani makazi 160 ya Wayahudi 700,000 tangu ilipokalia Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki, ardhi ambayo Wapalestina wanataka kama sehemu ya taifa la baadaye katika vita vya Mashariki ya Kati vya 1967. Wengi wa jumuiya ya kimataifa wanachukulia makazi hayo kuwa haramu chini ya sheria za kimataifa, ingawa Israel inapinga hili.

Chanzo cha picha, Instagram
Uchambuzi wetu uligundua kuwa video na picha 45 za mitandao ya kijamii ambazo tulichunguza zilitumwa na askari 11 wa Brigedi ya Kfir, ambayo ni kikosi kikubwa zaidi cha askari wa miguu katika IDF na hasa kinafanya kazi katika Ukingo wa Magharibi.
Wote 11 walikuwa, wakiwahudumia wanajeshi, na hawakuficha utambulisho wao kwenye mitandao ya kijamii.
Wanne wanatoka katika kikosi cha askari wa akiba cha Kfir Brigade - 9213, ambao eneo lao la operesheni linaonekana kuwa katika sehemu ya kaskazini ya Ukingo wa Magharibi, kulingana na uchambuzi wetu wa video zao za mitandao ya kijamii.
Tuliuliza IDF kuhusu vitendo vya askari mmoja mmoja tuliowataja na kama wameadhibiwa, lakini hawakujibu.
Pia tulijaribu kuwasiliana na askari hawa kwenye anuani zao za mitandao ya kijamii ili kuwaeleza matokeo yetu. Mmoja anaonekana kutuzuia na wengine hawakujibu wakati wa kuandika.
Machapisho mengi zaidi ya askari hawa yalikuwa chini ya jina la Yohai Vazana.
Video zake nyingi zinaonesha kikosi chake kikiingia majumbani usiku na kuwakamata Wapalestina, mara nyingi wakiwafunga mikono na kuwafumba macho. Wanawake wanaonekana wakiwa na hofu huku wakirekodiwa bila hijabu zao.
Amechapisha video na picha 22 kwenye Facebook na TikTok, kutoka kwa kile kinachoonekana kuwa picha za kamera za doria, zinazoonesha kukamatwa kwa Wapalestina.
TikTok ilithibitisha kuwa video mbili tulizoangazia, ambazo hazikuwa zimeshushwa kwenye mtandao, sasa zimeondolewa kwa kukiuka miongozo yake ambayo "inaweka wazi kwamba hatuvumilii maudhui ambayo yanalenga kuwadhalilisha waathiriwa wa mikasa ya vurugu".
Meta, kampuni inayomiliki Facebook, ilieleza kuwa inakagua maudhui na itaondoa video zozote zinazokiuka sera zake.

Chanzo cha picha, Facebook
Picha ya skrini kutoka kwa mojawapo ya video za Yohai Vazana, inaonesha washiriki wa kikosi chake wakiingia kwa nguvu kwenye nyumba na kupiga picha mbele ya mwanamke wa Kipalestina mwenye mtoto.
Mwanajeshi mwenzake Ofer Bobrov anashiriki katika picha kadhaa na Bw Vazana. Manukuu kwenye video zake mara nyingi hujumuisha alama ya reli "9213", ikionesha kuwa anatoka kwenye kikosi cha Bw Vazana.
Video za Bw Bobrov za operesheni zake za kijeshi huchapishwa pamoja na sehemu za wanajeshi wakicheza densi na karamu, wakiwa tayari kwa doria, na utaratibu mwingine wa maisha yao ya kila siku.
Video moja iliyochapishwa tarehe 12 Februari kwenye TikTok inajumuisha picha kadhaa za mfungwa akiwa amefunikwa macho na amefungwa sakafuni huku askari akisimama na bendera ya Israel nyuma yake.
Wapalestina wanaokamatwa mara kwa mara huoneshwa wakiwa wamefunikwa macho , baada ya kulazimishwa ama kulala sakafuni au kuchuchumaa, wakiwa wamefungwa mikono nyuma ya migongo yao.
Katika video moja, Bw Ben, ambaye pia amehudumu na vikosi vya IDF huko Gaza, anawakejeli Wapalestina wawili wanaozuiliwa, akiwaamuru kusema: "Am Yisrael Chai", kumaanisha "Watu wa Israel wanaishi".
Ori Dahbash ni mwanachama mwingine wa kikosi hicho ambaye amechapisha picha za operesheni za kijeshi katika Ukingo wa Magharibi, ikiwa ni pamoja na picha ya mfungwa ambayo pia imeshirikiwa na Bw.Vazana.

Chanzo cha picha, Facebook
Wataalamu walisema picha zilizotumwa na wanajeshi hao zinaweza kukiuka sheria za kimataifa.
Dk Mark Ellis, mwenyekiti wa jopo la ushauri lililoundwa na Umoja wa Mataifa kuhusu mahakama za kimataifa za uhalifu, alitoa wito wa uchunguzi wa matukio katika picha hizo, na IDF kuwatia adabu askari waliohusika.
Mwanasheria wa kimataifa wa haki za binadamu Sir Geoffrey Nice, ambaye alifanya kazi na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Yugoslavia ya Zamani (ICTY) kati ya 1998 na 2006, alikubaliana na Dk Ellis, lakini alikuwa na shaka kwamba mtu yeyote angewajibishwa kwa matendo yao.
Katika kujibu uchunguzi wetu, IDF ilijibu: "IDF inashikilia askari wake ... na inachunguza wakati tabia hii ambayo haiendani na maadili ya IDF. Katika tukio la tabia isiyokubalika, askari waliadhibiwa na hata kusimamishwa kazi.
"Aidha, askari wanaagizwa kuepuka kupakia picha za shughuli za uendeshaji kwenye mitandao ya kijamii."
Jibu la IDF halikukubali kwamba iliahidi kuchukua hatua juu ya matokeo yetu ya awali juu ya utovu wa nidhamu kama huo wa mitandao ya kijamii, huko Gaza.
Bw.Givati, kamanda wa zamani wa Israel katika Ukingo wa Magharibi, alisema alihisi aibu na kuchukizwa na jinsi wanajeshi wa Israel wanavyowatendea wafungwa.
"Tunapaswa kuwatendea kwa heshima ambayo tungependa kutendewa," aliiambia BBC.
Alisema tabia hiyo inaakisi jinsi alivyohisi jamii ya Israel inawatazama Wapalestina, na kutilia shaka madai yake ya kutii sheria za kimataifa.















