Wasiwasi na mawazo ya kujiua: hatari za vinywaji kuongeza nguvu kwa watoto na vijana

Chanzo cha picha, Getty images
Na Philippa Roxby
Mwandishi wa BBC wa taarifa za Afya
Uuzaji wa vinywaji vyote vya kuongeza nguvu kwa vijana na watoto nchini Uingereza unapaswa kupigwa marufuku, kulingana na moja ya tafiti za hivi karibuni juu ya athari za vinywaji hivyo za kiafya.
Utafiti huo unahusisha unywaji wa vinywaji hivi na viwango vikubwa vya hatari kuliko hapo awali, ikiwa ni pamoja na wasiwasi, mafadhaiko na mawazo ya kujiua.
Vinywaji hivi ambavyo kwa kawaida huwa na viwango vya juu vya kafeini na sukari na huuzwa kama "vyanzo vya nishati."
Maduka mengi makubwa ya Uingereza yameanzisha marufuku ya hiari ya uuzaji wa vinywaji vya kuongeza nguvu kwa watoto wa chini ya umri wa miaka 16.
Marufuku ya jumla, ambayo pia yangeyahusu maduka yote madogo, wauzaji reja reja wa mtandaoni na mashine za kuuza, ilipendekezwa nchini Uingereza na Uskochi mnamo mwaka 2019. Mamlaka ya afya ya Kiingereza ilisema itatoa jibu la suala hili "kwa wakati ufaao".
Kufuatia utafiti huo, mashirika 40 ya afya yalituma barua kwa Waziri wa Afya wa Uingereza Victoria Atkins kusisitiza wito wao wa kuzuiwa kwa uuzaji wa vinywaji vya kuongeza nguvu.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
"Vingi kati ya vinywaji hivi vina kiasi kikubwa cha kafeini, wakati mwingine kati ya miligramu 160 na 200 kwa kila kopo. Kiasi hiki ni mara mbili ya kile kilicho katika kikombe cha wastani cha kahawa (karibu 80 mg, kulingana na nguvu) " inaonyesha barua hiyo.
Wasindikaji wa hivi mara nyingi kwenye maelezo yao husema kuwa havifai watoto, lakini wale walio chini ya umri wa miaka 18 wanaweza kununua kwa urahisi katika maduka madogo ya mboga, watafiti na wataalam wanasema.
Vinywaji vya kuongeza nguvu vinauzwa kama vichocheo vya kimwili na kiakili na hutoa nishati zaidi kuliko vinywaji baridi vya kawaida.
Hili ni soko kubwa na linalokua. Nchini Uingereza, hadi theluthi moja ya watoto hutumia aina hii ya vinywaji angalau mara moja kwa wiki.
Amelia Lake, profesa wa lishe ya afya ya umma katika Chuo Kikuu cha Teesside, ambaye aliongoza uhakiki wa tafiti kuhusiana na vinywaji hivi , alichambua tafiti 57 za hivi karibuni kuhusu vinywaji vya kuongeza nguvu na athari zake kwa afya ya vijana. Zaidi ya watoto milioni moja kutoka nchi 21 walijumuishwa katika utafiti huo.
"Ushahidi uko wazi: vinywaji vya kuongeza nguvu ni hatari kwa afya ya akili na ya kimwili kwa watoto na vijana, pamoja na tabia na elimu yao," alisema.
"Lazima tuchukue hatua sasa ili kuwalinda kutokana na hatari hizi.
Utafiti huo uligundua kuwa wavulana walikuwa na uwezekano mkubwa wa kunywa vinywaji vya kuongeza nguvu kuliko wasichana.
Aidha, unywaji wa vinywaji hivi mara kwa mara una uwezekano mkubwa wa kuwachochea vijana kutumia dawa za kulevya, kuwa na wajeuri na kufanya ngono bila kinga.
Matatizo ya usingizi, utendaji duni wa kitaaluma na mlo usio na afya pia unahusishwa kwa karibu na matumizi ya vinywaji vya nishati, utafiti unahitimisha.
Bi Lake alisema kuwa ingawa utafiti wake haukuweza kuthibitisha kwamba vinywaji vya kuongeza nguvu vilisababisha madhara ya moja kwa moja kwa afya - kwa sababu tafiti za lishe daima hutegemea uchunguzi - matokeo ni muhimu na yanaunda ushahidi bora zaidi unaopatikana.
Inawezekana kwamba vinywaji vya kuongeza nguvu vinahusishwa na madhara ya kiafya kwa sababu wale wanaovitumia mara kwa mara wana uwezekano mkubwa wa kupata tabia zingine zisizofaa, kama vile kuvuta sigara au kunywa pombe, kwa mfano.
Tahadhari kuhusu Kafeini
Mapendekezo rasmi yanasema kuwa matumizi ya kafeini haipaswi kuzidi miligramu 3 kwa kilo ya uzito wa mwili.
"Ni rahisi sana kwa kijana kunywa kiasi hicho, huku kafeini ambayo ni sawa na kahawa mbili ikiwa ndani ya kopo kubwa la kinywaji cha kuongeza nguvu’’, asema Bi. Lake.
Kiasi kikubwa cha sukari kinaweza pia kuharibu meno ya watoto na, ikiwa tayari hawajala vizuri, huchangia kunenepa kupita kiasi.
Baadhi ya nchi, kama vile Latvia na Lithuania, tayari zimepiga marufuku uuzaji wa vinywaji vya kuongeza nguvu kwa watoto, lakini ni mapema mno kutathmini athari za hatua hii.
Nchi nyingine, kama vile Finland na Poland, zinaweza kufuata mfano huo.
Uingereza na Uskochi zilifanya mashauriano ya umma kuhusu kupiga marufuku mauzo kwa watoto miaka minne iliyopita, na Wales inazingatia kufanya mashauriano kama hayo mnamo 2022.
Sheria za sasa zinasema kwamba vinywaji vyenye kafeini, kutoka chanzo chochote, katika viwango vya juu ya miligramu 150 kwa lita, lazima viwe na taarifa ifuatayo kwenye lebo: "Kiwango cha juu cha kafeini. Hakipendekezwi kwa watoto na wanawake wajawazito au wanaonyonyesha.
"Tumefanya mashauriano ya umma kuhusu kupiga marufuku uuzaji wa vinywaji vya kuongeza nguvu kwa watoto walio na umri wa chini ya miaka 16 nchini Uingereza na tutawasilisha majibu yetu kamili kwa wakati ufaao," alisema msemaji wa Wizara ya Afya na Huduma za Kibinadamu ya Uingereza.
"Wakati huo huo, maduka mengi na hasa maduka makubwa yamepiga marufuku kwa hiari uuzaji wa vinywaji vya kuongeza nguvu kwa watoto wa chini ya umri wa miaka 16.
Watoto na watu wengine wanaoweza kuathiriwa na kafeini wanapendekezwa kuitumia tu kwa kiasi.
William Roberts, wa Shirika la Kifalme la Afya ya Umma, alisema utafiti huo "unaongeza ushahidi kwamba vinywaji vya kuongeza nguvu vinaweza kudhuru afya ya mwili na akili ya watoto na vijana, kwa muda mfupi na kwa muda mrefu".
"Ndio maana tunahitaji serikali ya Uingereza kuchukua uongozi na kutimiza ahadi yake ya 2019 ya kupiga marufuku uuzaji wa vinywaji vya kuongeza nguvu kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 16."
Imetafsiriwa na Dinah Gahamani












