Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Gregory X: Mfahamu Papa huyu ambaye uchaguzi wake ulichukua miaka mitatu
Kongamano litakalomchagua mrithi wa Papa Francis lilianzisha sheria zake za msingi karne nyingi zilizopita.
Ni Papa Gregory X ambaye alithibitisha kwamba makadinali wanaosimamia kumchagua kiongozi wa Kanisa Katoliki walipaswa kujifungia na kujitenga na ulimwengu wa nje kufanya uamuzi muhimu kama huo.
Ingawa zimefanyiwa marekebisho, sheria alizoanzisha bado zinatumika hadi leo.
Ingawa hakuwa hata kuhani alipochaguliwa, kwani upapa wake ulidumu miaka mitano tu (1271-1276), Gregory X alikuwa mmoja wa mapapa wenye umuhimu zaidi wa kiroho katika historia.
Ili kuelewa maisha yake, lazima uelewe wakati wake.
Kanisa lililogawanyika
Katikati ya karne ya 13, Ukristo uligawanyika sana.
Tangu karne ya 11, maisha ya Ulaya yalikuwa na mapambano kati ya upapa na ufalme ulioundwa na mfalme wa Frankish Charlemagne, haswa katika maeneo ya Ujerumani ya sasa, inayojulikana leo na wanahistoria kama Milki Takatifu ya Kirumi.
"Papa na mfalme wa kile tunachokiita sasa Milki Takatifu ya Kirumi walikuwa wakishiriki katika mapambano ya uongozi wa Jumuiya ya Wakristo," Alejandro Rodríguez de la Peña, profesa wa historia ya zama za kati katika Chuo Kikuu cha CEU San Pablo huko Madrid, aliiambia BBC Mundo.
"Kwa karne kadhaa, watawala walikuwa wakipingana na mapapa hadi kufikia hatua ya makabiliano ya kijeshi, na mfalme mkuu wa mwisho, Frederick II, alikuwa ametengwa."
Nguvu hizi mbili kubwa zilijiunga na Ufaransa mpya iliyounganishwa, ambayo ilikuwa imekamilisha ushindi wake wa kusini mwa Italia ," anasema Rodríguez de la Peña.
Huu ulikuwa ulimwengu wakati Papa Clement IV alikufa mnamo Novemba 29, 1268, huko Viterbo, mji ambao ulikuwa sehemu ya kile kilichokuwa Majimbo ya Papa, ambayo yalienea zaidi ya Vatican ya sasa.
Kwa kufuata utamaduni wapiga kura makardinali, husafiri hadi mahali ambapo papa alifariki kumchagua mrithi wake.
Lakini makardinali wamegawanywa katika kambi mbili zinazoonyesha mvutano wa wakati huu.
Kwa upande mmoja, kikundi cha makadinali wa Italia walijiunga na masilahi ya Dola, inayojulikana kama Ghibellines; na kwa upande mwingine, makadinali wa Ufaransa wanaojulikana kama Guelphs, ambao walipinga nguvu kubwa ya kisiasa, kiuchumi, na kidini ya Kanisa la wakati huo likiwa chini ya udhibiti wa Milki Takatifu ya Kirumi.
Ushindani ulimaanisha kuwa miezi ilipita bila makardinali kufikia makubaliano, na hakuna mgombea aliyefikia wingi unaohitajika, kwa hivyo – kongamano liliendelea.
Lilidumu kwa karibu miaka mitatu na kuwa refu zaidi katika historia ya Kanisa.
Wakiwa wamechoka kusubiri bila suluhisho, madiwani wa jiji la Viterbo waliwafungia makardinali katika jumba la kifalme ambapo walikutana na hata kufikia hatua ya kupunguza milo yao ya kila siku ili kuwalazimisha kufikia makubaliano.
"Mhusika mdogo"
Hatimaye, mteule aliteuliwa kuwa ni Teobaldo Visconti, shemasi mkuu ambaye hata hajatawazwa kuwa padri na ambaye wakati huo alikuwa Mtakatifu Jean d'Acre, katika Syria ya leo, kwenye vita vya msalaba dhidi ya Waislamu.
"Kwanini walichagua mhusika mdogo ambaye pia alikuwa upande wa pili wa ulimwengu ni fumbo ambalo hatuwezi kufunua na vyanzo vinavyopatikana," anasema Rodríguez de la Peña.
Visconti alikuwa Muitaliano ambaye hakuwa amepokea maagizo ya ukuhani, lakini ambaye alikuwa amekutana na kufanya kazi na makadinali wengi wa Ufaransa katika nyadhifa mbali mbali na ambaye alikuwa na uhusiano mzuri sana, "kwa hivyo tunaweza kukisia kwamba anaweza kuwa alichaguliwa kama mgombea wa maelewano," mwanahistoria wa Uhispania anasema.
Kipindi cha mpito katika Kanisa hakikuisha mara moja, kwani ilimchukua Visconti miezi kadhaa kurudi kutoka Nchi Takatifu na ilibidi atawazwe wakfu kuwa kasisi na kuteuliwa kuwa Askofu wa Roma kabla ya kutawazwa kuwa Papa.
Lakini, mara moja kwenye kiti cha enzi cha Mtakatifu Petro, "Gregory X alionyesha kwamba atakuwa papa huru, kwamba hatajiruhusu kushinikizwa, na kuishia kuwa papa mzuri," anasema Rodríguez de la Peña.
Papa mpya atajaribu kuponya majeraha ya ndani ya Kanisa, kutafuta maelewano na Kanisa la Orthodox, na kusisitiza umuhimu wa kukamilisha Vita vya Msalaba na ushindi wa Nchi Takatifu.
Lakini urithi wake muhimu zaidi utakuwa mwingine.
Mfumo mkali zaidi
Gregory X alijaribu kudai uhuru wa Kanisa kutoka kwa "nguvu za kidunia" na njia ya kumchagua Papa - Ubi periculum , iliyotangazwa katika Baraza la Lyon mnamo 1274.
Rodríguez de la Peña anaelezea kuwa "njia ya kumchaguza Papa ililenga kuwatenga wapiga kura Makardinali kutoka kwa ushawishi mbaya wa nje na shinikizo kutoka kwa watawala" wa wakati huo, ambao walikuwa na nia ya kudhibiti taasisi yenye nguvu katika ulimwengu wa zamani kama upapa.
Papa Gregory X alithibitisha kwamba makardinali walipaswa kubaki chini ya ulinzi na bila mawasiliano katika jumba la kifalme alikofia papa na, Kardinali angeweza kuondoka huko tu mara tu mrithi atakapochaguliwa.
Walipaswa kuishi pamoja, wakitenganishwa tu na vitambaa kwa muda wote wa mkutano huo, na kutoka siku ya tatu na kuendelea waliruhusiwa sahani moja tu ya chakula kwa siku.
Kuanzia siku nane na kuendelea wangeweza kula mkate na maji tu.
Masharti hayo yalifanya maisha kuwa magumu kwa makardinali wakati wa mkutano huo katika jaribio dhahiri la Gregory kukuza makubaliano na kuzuia kurudiwa kwa hali ambazo zilisababisha kuchaguliwa kwake mwenyewe.
Ingawa Rodríguez de la Peña pia anaona mwelekeo wa kitheolojia: "Wazo ni kwamba kutengwa na kutokuwepo kwa shinikizo la nje kutoka kwa nguvu za wakati huo huwaruhusu kusikia sauti ya Roho Mtakatifu na kufanya uamuzi mzuri ulioongozwa naye."
Gregory X alikufa mnamo 1278 na alitangazwa mwenye heri mnamo 1713.
Baadhi ya vifungu vyake vikali zaidi vya uchaguzi wa papa mpya vilipunguzwa na mapapa wa baadaye, na vingine vilishindwa kutumika, lakini wazo muhimu la kuwatenga wapiga kura wa makardinali limebaki hadi leo na litasisitizwa katika mkutano ambao utamchagua mrithi wa Papa Francis.
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi