Siri kubwa ya kongamano Makardinali wanapomchagua Papa mpya

Muda wa kusoma: Dakika 6

Kwa zaidi ya miaka 750, sheria kali zimetawala orodha ya makadinali wanaokusanyika kumchagua papa. Kwa mfano, ravioli, napkini na kuku ni vitu ambavyo vimepigwa marufuku kutoka kwa meza ya makadinali kwa karne nyingi, kwani vinaweza kutumika kupitisha ujumbe wa siri.

Hii ni tafsiri iliofanywa na mwandishi wa BBC;

Wiki iliyopita, ukitembea kuizunguka Roma, mara nyingi hungeweza kuona makardinali kwenye mgahawa. Wana haraka ya kufurahia chakula wanachopenda - na haishangazi: kwamba kuanzia Mei 7, makadinali 135 watatengwa na sehemu nyingine ya dunia katika eneo la Sistine Chapel. Watatengwa na ulimwengu hadi kura ya siri iamue nani atakuwa papa mpya..

Mwaka 2013, ilikuwa mara ya mwisho kwa uchaguzi wa Papa kufanyika, vyombo vya habari vya Italia viliripoti kwamba makadinali wengi walikuwa wakitembelea Al Passetto di Borgo, mgahawa wa familia ulio mita 200 tu kutoka Basilica ya St. Kadinali Donald William Wuerl anayejulikana kwa kuagiza lasagne, huku Francesco Coccopalmerio (mojawapo ya makadinali waliopendwa zaidi mwaka 2013) akipendelea ngisi wa kukaanga.

Mikutano ya Papa imekuwa maarufu kwa usiri wao. Makardinali hufungiwa kwenye chumba kimoja, bila mawasiliano na ulimwengu wa nje.

Ishara pekee inayoruhusiwa ni moshi: mweupe una maana kwamba papa amechaguliwa, mweusi unamaanisha kura ya pili inahitajika kwa sababu thuluthi mbili pamoja na kura moja haijaafikiwa.

Ni nini hasa kinatokea ndani ya mkutano huo haijulikani, lakini jambo moja ni wazi: makadinali wanapaswa kula kwa siku au wiki ili kuchagua papa mkuu wa pili wa Kanisa Katoliki la Roma, ambalo lina Wakatoliki bilioni 1.4.

Pia unaweza kusoma

Lakini usiri unaweza kudumishwa vipi na upigaji kura kuhakikishiwa una kinga dhidi ya ushawishi wa nje ikiwa makadinali wataletewa chakula chao na mabaki ya chakula hicho kuondolewa?

Kihistoria, chakula kimekuwa tishio linalowezekana: mpishi anaweza kuficha ujumbe kwa kadinali kwenye ravioli, au kadinali anaweza kupitisha ujumbe kwenye kitambaa kichafu. Milo ya pamoja inaweza pia kuwa tovuti ya mazungumzo ya siri.

Picha hii, ya "utamaduni wa chakula", hutumiwa na tamaduni maarufu ili kuunda mazingira ya mashaka, fitina, na udhibiti.

Katika filamu ya Conclave (2024), karibu hatua zote hufanyika sio katika ukumbi wa kupiga kura, lakini katika chumba cha kulia.

Milo ya kelele inatofautiana na ukimya wa karibu wa mkutano wenyewe, ambapo hakuna mjadala rasmi. Ukimya huo unavunjwa tu na wakati wa hotuba ya kitamaduni, kama vile kiapo kinachochukuliwa na kardinali wakati wa kupiga kura kumchagua papa.

Hata hivyo, karibu na ukimya huu wa sherehe bado kuna mawasiliano mengi, mara nyingi kwa njia ya chakula.

Na ingawa filamu hiyo si onyesho sahihi la kile kinachoendelea nyuma ya milango iliyofungwa, hakuna shaka kwamba katika "utamaduni wa chakula" wa papa, kama ilivyo katika utamaduni mwingine wowote, kile unachokula, jinsi unavyokula, na mtu unayekula naye hutoa ujumbe mkubwa.

Msururu wa sheria za usiri ambazo bado zinatumika hadi leo zilianzia 1274, wakati Papa Gregory X alipochaguliwa kwa kipindi cha karibu miaka mitatu, kutoka 1268 hadi 1271.

Ulikuwa uchaguzi mrefu zaidi wa upapa katika historia. Mwanasheria mkuu wa Kiitaliano Enrico de Segusio, ambaye alishiriki katika mkutano huo, aliandika kwamba wakazi wa jiji hilo walitishia kupunguza mgao wa chakula cha makadinali hao ili kuharakisha mchakato huo.

Hata wakati huo, washiriki wa conclave walipaswa kutengwa. Sheria za chakula cha makardinali zilikuwa kali zaidi: baada ya siku tatu bila makubaliano, makardinali waliruhusiwa chakula kimoja kwa siku, na baada ya siku nane - mkate na maji tu.

Katikati ya karne ya 14, Papa Clement VI alipunguza vikwazo hivi, kuruhusu sahani tatu za chakula kwa siku ambazo zinashirikisha: supu, , nyama au mayai na jibini au matunda). Ingawa sheria kali ya kufunga haikushikamana, udhibiti mkali juu ya mchakato ulisalia.

Historia ya kina zaidi ya milo ya conclave ni ya Bartolomeo Scappi, mpishi maarufu wa ya miaka hiyo. Alimtumikia Papa Pius IV na Pius V, na mnamo 1570 alichapisha kitabu cha upishi, Opera Dell'Arte del Cucinare (Sanaa ya Kupika), ambayo ilimletea umaarufu mkubwa.

Anaelezea jinsi mkutano huo wa makadinali walivyokula wakati wa uchaguzi wa Papa Julius III, na anaandika kuhusu jinsi udhibiti ulivyohakikishwa - na mazoea anayoelezea bado yanatumika hadi leo.

Kama Scappi anavyoandika, milo ya makadinali ilitayarishwa katika jiko la kawaida na wapishi na wahudumu wa chakula, walikuwa sehemu tu ya wafanyikazi wanaohudumia makadinali hao.

Jiko linaweza kuwa mahali pazuri pa ujumbe wa siri, na kwa hivyo walinzi walikuwa wakifanya kazi hapo kila wakati.

Mara mbili kwa siku, watumishi walipeleka chakula kwa sherehe kwenye dirisha. Kwa njia hiyo, chakula kilipitishwa kwa makadinali. Kabla ya hili, sahani zilikaguliwa na watambuzi kwa ujumbe wa siri kwenye chakula. Kila hatua ilisimamiwa na walinzi wa Italia na Uswisi.

Udhibiti wa chakula ulikuwa mkali: hakuna kitu ambacho kinaweza kuficha barua kiliruhusiwa. Hakuna mikate iliyofungwa, hakuna kuku mzima. Mvinyo na maji tu katika vyombo vya uwazi.

Vitambaa vilifunuliwa na kuchunguzwa kwa uangalifu. Hii sio tu kuhakikisha wamba makadinali wanatengwa, lakini pia ilipunguza hatari ya sumu – kwani baada ya yote, Papa amekuwa mtu mwenye ushawishi mkubwa wa kisiasa, na haswa wakati wa enzi za kale.

Licha ya vikwazo, makardinali, kulingana na maelezo ya Scappi, walikula vizuri. Saladi, matunda, nyama baridi, divai na maji safi zilitolewa. Hali ya maisha iliyoelezwa na Scappi ilikuwa nzuri: kila chumba kilikuwa na kitanda, meza, hanga za kutundikia nguo, viti viwili, sufuria na chombo kilicho na kifuniko, pamoja na vitu vingine. Mbali na udhibiti kamili, ushiriki katika conclave wakati wa Renaissance haikuwa jambo gumu.

Wakati wa mkutano huo utakaoanza tarehe 7 Mei, makadinali kama kawaida wataishi katika Casa di Santa Marta, kiambatisho cha Kanisa kuu la Mtakatifu Petro. Watawa watawapikia makadinali. Sahani zitakuwa za kawaida za mkoa wa Lazio, ambapo Vatican iko, na Abruzzo jirani: watakula tambi, kondoo na mboga za kuchemsha. Lengo ni kuboresha hali hali ikilinganiswa na zama za kale na kuhakikisha kuwa mchakato unadhibitiwa madhubuti ili kuzuia uvujaji wa habari.

Katika filamu ya Conclave, moja ya maonyesho ya kwanza jikoni, yanaonyesha watawa wakichemsha kuku mzima kwa mchuzi: chakula cha kawaida, sio cha anasa kabisa. Lakini hilo si jambo la muhimu, ishara ni: Kanisa Katoliki la kisasa - hasa tangu Papa Francis - linajitahidi kuonyesha picha ya kawaida na kiasi. Wasiwasi kuhusu ujumbe wa siri katika kuku ni jambo la zamani.

Vifaa vya kielektroniki sasa vinachukuliwa kuwa tishio kuu, na hii inaonyeshwa mara kwa mara kwenye filamu.

Kwa hiyo wakati Vatikan inakaguliwa kwa vifaa vya elektroniki vilivyofichwa kabla ya mkutano huo, makadinali wanajitayarisha kwa njia tofauti: kutembea karibu na Roma na kufurahia vyakula wanavyopenda. Kwa mmoja wao, moja ya chakula cha jioni kitakuwa mwisho wao kama kardinali.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Seif Abdalla