Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Tunachokijua kuhusu mkataba wa madini wa Ukraine na Marekani
Washington na Kyiv zimetia saini mkataba uliokuwa ukisubiriwa kwa muda mrefu juu ya madini ya Ukraine, baada ya miezi kadhaa ya mazungumzo yenye utata.
Pande zote mbili zimethibitisha kwamba zinaanzisha mfuko wa uwekezaji wa kuchimba madini, na kuunda makubaliano ya kugawana mapato.
Marekani imesema makubaliano hayo ni "ishara kwa Urusi" kwamba utawala wa Trump "umedhamiria kusaka amani, uhuru na ustawi" wa Ukraine.
Makubaliano yamekuja baada ya miezi miwili kupita tangu mkutano kati ya Rais wa Marekani Donald Trump na Zelensky katika Ikulu ya White House kugeuka kuwa mzozano na kuzusha hofu kwamba huenda Marekani ikajiondoa katika uungaji mkono wake kwa Ukraine.
Mkataba huo unasemaje?
Waziri wa Uchumi wa Ukraine, Yulia Svyrydenko alisafiri kwa ndege kuelekea Washington siku ya Jumatano baada ya mazungumzo ya kutia saini makubaliano hayo kufikiwa na Waziri wa Fedha wa Marekani, Scott Bessent.
Baada ya wawili hao kutia Saini, Svyrydenko aliorodhesha masharti ya mkataba huo kwenye mitandao ya kijamii.
Akichapisha kwenye X, mkataba huo utaanzisha mfuko wa uwekezaji ili kusaidia kuvutia uwekezaji wa nchi za Magharibi katika miradi ya madini, mafuta na gesi nchini Ukraine.
Amesema rasilimali zitabaki kuwa mali ya Ukraine, na Kyiv itachagua wapi pa kufanya uchimbaji.
Ushirikiano huo utakuwa wa sawa, kwa misingi ya 50/50, amesema, akiongeza kuwa makubaliano hayo hayatahusisha malipo yoyote ya fedha ambayo Ukraine itatakiwa kuilipa Marekani.
Marekani itawajibika katika kusaidia kuvutia uwekezaji na teknolojia kwa miradi ya Ukraine.
Kama sehemu ya mkataba huo, Marekani itachangia msaada mpya kwa Kyiv, ambao unaweza kujumuisha, kwa mfano, mifumo ya ulinzi wa anga.
Anasema mapato na michango ya mfuko huo haitatozwa kodi na nchi zote mbili.
Svyrydenko amesema mkataba huo lazima uidhinishwe na wabunge wa Ukraine.
Haijulikani ikiwa mpango huo unajumuisha hakikisho la wazi la usalama wa Ukraine kutoka Marekani, jambo ambalo Zelensky amesisitiza katika mazungumzo ya nyuma.
Taarifa ya Idara ya Fedha ya Marekani imesema: "Hakuna serikali au mtu ambaye alifadhili au kupeleka silaha za vita kwa Urusi ataruhusiwa kufaidika na ujenzi mpya wa Ukraine."
Trump, kwa upande wake, amesema mpango huo unawakilisha malipo kwa pesa ambazo Marekani imetumia kwenye vita hivyo hadi sasa.
"Biden aliipa Ukraine dola bilioni 350," Trump amesema kupitia runinga ya NewsNation katika mazungumzo ya simu. Ameongeza: "Tumeingia kwenye makubaliano ambayo yatatupa ya dola bilioni 350 zaidi."
Trump amedai Marekani imetumia karibu dola bilioni 350 (£263 bilioni) kama msaada kwa Ukraine. Lakini uchambuzi wa BBC umegundua kuwa kiasi halisi ni kidogo kuliko hicho.
Alipoulizwa ikiwa uwepo wa Marekani nchini Ukraine unaweza kuzuia vita vya Urusi katika eneo hilo, amesema "inaweza."
Ukraine ina madini gani?
Kyiv inakadiria kuwa karibu 5% ya madini muhimu duniani yako Ukraine. Ikijumuisha tani milioni 19 za madini ya graffiti. Kwa mujibu wa Taasisi ya serikali ya Utafiti wa Jiolojia, inasema Ukraine ni "moja ya nchi tano zinazoongoza" kwa usambazaji wa madini hayo. Grafiti hutumiwa kutengeneza betri za magari ya umeme.
Ukraine pia ina kiwango kikubwa cha madini ya titanium na lithiamu. Inasema ina kiasi kikubwa cha madini adimu duniani – yanayotumiwa kutengeneza silaha, mitambo ya umeme wa upepo, vifaa vya elektroniki na vifaa vingine muhimu katika ulimwengu wa sasa - lakini madai haya hayana uhakika.
Pia, baadhi ya maeneo yenye madini ya nchi hiyo yamekamatwa na Urusi. Kulingana na Svyrydenko, rasilimali zenye thamani ya dola bilioni 350 (£277bn) ziko katika maeneo yanayokaliwa na Urusi.
Kuna onyo pia, kwamba mpango unaoiruhusu Marekani kufaidika na utajiri mkubwa wa madini wa Ukraine hauwezi kutokea, isipokuwa nchi hiyo ishughulikie kwanza tatizo la mabomu ya chini ya ardhi ambayo hayajalipuka.
Robo ya ardhi ya Ukraine inakadiriwa kuwa na mabomu ya ardhini, zaidi katika maeneo yenye vita mashariki mwa nchi hiyo.
Suala jingine ni kwamba, itachukua muda kabla ya mtu yeyote kuona manufaa ya mpango huo.
"Rasilimali hizi haziko kwenye bandari au ghala; lazima zichimbwe," anasema Tymofiy Mylovanov, waziri wa zamani na mkuu wa kitivo ch uchumi katika chuo kikuu cha Kyiv.
Urusi inasemaje?
Urusi bado haijatoa maoni yoyote kuhusu mpango huo, lakini mapema mwaka huu, Vladimir Putin aliiambia TV ya serikali kuwa yuko tayari "kutoa" rasilimali kwa washirika wa Marekani katika miradi ya pamoja, ikiwa ni pamoja na uchimbaji madini katika "maeneo mapya" ya Urusi - akimaanisha maeneo ya mashariki mwa Ukraine inayoyakalia tangu uvamizi wake miaka mitatu iliyopita.
Putin pia alisema, makubaliano kati ya Marekani na Ukraine kuhusu madini si jambo la msingi kwa Urusi. Na akasisitiza kuwa kuwa Urusi ina rasilimali nyingi zaidi za aina hiyo kuliko Ukraine."
"Kuhusu maeneo mapya, tuko tayari kushirikiana na washirika wa kigeni," aliongeza.
Imetafsiriwa na Rashid Abdalla