Ligi Kuu ya China: Kutoka kutaka kumnunua Bale hadi kufilisika na kuuza basi la timu

efdcv

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Hulk alisajiliwa na timu ya Shanghai SIPG
    • Author, Sophie Williams
    • Nafasi, BBC

Juni 2016, mamia ya mashabiki walikusanyika kwenye uwanja wa ndege wa Shanghai, China ili kutazama mmoja wa wanasoka maarufu ulimwenguni akiwasili katika jiji hilo.

Givanildo Vieira de Sousa almaarufu Hulk, mchezaji wa kimataifa wa Brazil akiwa na umri wa miaka 29 wakati huo, alisajiliwa na meneja wa Shanghai SIPG, Sven-Goran Eriksson kwa zaidi ya pauni milioni 46 na mshahara wake wa pauni 320,000 kwa wiki.

Miaka mitatu baadaye, majina mengine makubwa yalisajiliwa kwa vitita vikubwa zaidi.

Nyota wa Chelsea, Oscar aliwasili miezi sita baadaye. Ada ya uhamisho ilikuwa takribani pauni milioni 60. Mshahara wake ukiaminika kuwa pauni 400,000 kwa wiki.

Carlos Tevez, mchezaji aliyeshinda kombe la Ligi Kuu ya Uingereza akiwa na Manchester United na City, inasemekana alisajiliwa kwa pesa nyingi sana.

Nyota wa Paris St-Germain, Ezequiel Lavezzi, wa Liverpool, Alex Teixeira na mshambuliaji wa Colombia, Jackson Martinez pia walisajiliwa kwa pesa nyingi.

Azma ya Rais Xi

rgf

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Sealy mwenye jezi nyeupe akipambana na Oscar katika mechi dhidi Shanghai SIPG mwezi Machi 2017

Kuboreshwa kwa ligi ya China (Super League) kulikuja sambamba na matakwa ya Rais Xi Jinping ya kuigeuza nchi hiyo kuwa taifa la kandanda. 2011 alitangaza mipango ya timu ya taifa ya wanaume kufuzu Kombe la Dunia na China kuwa mwenyeji wa mashindano hayo.

Ligi Kuu ya China ilipoanza kutumia kiasi kikubwa cha pesa, azma yake ya kuligeuza taifa hilo kuwa taifa lenye nguvu katika kandanda ilianza kuonekana kuwa ya kweli.

"Soko la China ni tishio kwa timu zote duniani, si kwa Chelsea pekee," alisema meneja wa wa timu hiyo Antonio Conte wakati huo Oscar akielekea mashariki.

"China inaonekana kuwa na uwezo wa kifedha wa kuhamisha ligi nzima ya Ulaya hadi China," alisema mwenzake wa Arsenal, Arsene Wenger.

Mipango yakwama

gf

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Tevez alisajiliwa na Shanghai Shenhua kutoka Boca Juniors
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Hata hivyo, baada ya mwongo mmoja, azma ya China iko katika mwelekeo tofauti, lengo limeshindwa kufanikiwa na wachezaji wameondoka.

Kufikia 2019, ligi hiyo ilikuwa kubwa kiasi kwamba Gareth Bale wa Real Madrid - wakati fulani mchezaji ghali zaidi duniani - ilielezwa atahamia Jiangsu Suning kwa mkataba wa miaka mitatu, kwa pauni milioni 1 kwa wiki.

Chini ya miaka miwili baadaye, timu ya Jiangsu Suning ilikufa ikiwa na hali mbaya ya kifedha - kufikia hatua ya kulipiga mnada basi la timu hiyo kwa pesa taslimu.

Mambo yaliharibika pale Chama cha Soka cha China (CFA), ambacho awali kilianzisha kodi iliyofanya uhamisho wa pesa nyingi kuwa mgumu na kukataza wafadhili wakubwa kuzipa timu majina yao - kilipotangaza kikomo cha mishahara mnamo Disemba 2020.

Wakati huo, CFA ilisema kuweka kikomo cha mishahara ilitumai ingedhibiti pesa na kutoa uwekezaji kwa timu ya taifa ya China.

Kwa muda mrefu, utawala wa michezo wa China ulikuwa ukihofia matumizi ya ligi. 2017 iliapa kuzuia matumizi na kudhibiti uwekezaji usio na maana, ikivishutumu vilabu kutumia pesa nyingi na kuwalipa wachezaji wa kigeni mishahara mikubwa kupita kiasi.

Kikomo cha mshahara hakika kilikuwa na athari. Kikomo hicho kilimaanisha wachezaji wa nje wangeweza tu kulipwa kitita cha pauni 52,000 kwa wiki, malipo madogo ukilinganisha na mikataba ya wachezaji waliosajiliwa awali.

Baadhi ya timu zilihitaji vizuizi hivyo kutokana na madeni kwa sababu ya matumizi yao makubwa. Idadi kubwa ya matatizo ya vilabu pia yalichochewa na matatizo ya wamiliki wao.

Vilevile wakati wa uviko 19, sera kali za China zilipunguza orodha ya mechi na kuamuru michezo yote ichezwe bila mashabiki kwa zaidi ya miaka miwili. Mapato ya utangazaji na ufadhili yakashuka.

Beki wa Bosnia-Herzegovina, Samir Memisevic alichezea Hebei FC kuanzia Februari 2020 - aliiambia BBC.

"Baada ya miezi michache, matatizo ya kifedha yalianza. Walikuwa na tatizo kubwa na wachezaji wa China - hawakuwalipa kwa miezi mingi na nilikuwa na uhakika kwamba mwisho wa mwaka huo klabu hiyo haitakuwepo tena. "

Memisevic alipokea na kukubali ofa ya kwenda kwa mkopo Beijing Guoan, moja ya vilabu vikubwa kwenye ligi hiyo.

Timu ya Hebei, ambayo ilimsajili Lavezzi na wachezaji wa zamani wa Ligi Kuu ya Uingereza, Javier Mascherano na Gervinho, ilifuta timu zao za vijana kwa nia ya kutaka kunusurika.

Na baadhi ya wafanyikazi walikubali kufanya kazi bila malipo kwa miezi kadhaa, walijitolea kufanya kazi bure kwa ajili ya timu. Licha ya hayo yote, mapema mwaka huu Hebei ilisambaratika.

"Ninaionea huruma sana klabu ya Hebei kwa kilichotokea kwa sababu ilikuwa moja ya timu kubwa zenye majina makubwa na pesa," alisema Memisevic, ambaye sasa anachezea Al-Nasr ya Dubai.

Ufisadi pia ni Tatizo

dvc

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mashabiki wa soka huko China

Kwa shabiki wa soka John Hassett, Ligi Kuu ya China haitakuwa nzuri bila timu anayoipenda, Guangzhou City. Klabu hiyo ilikuwa ikisimamiwa na Eriksson na nyota wa zamani wa Arsenal na Rangers Giovanni van Bronckhorst ilivunjwa mwezi Machi.

"Sehemu ya tatizo ni kwamba vilabu vingi havikuweka mipango ya kutengeneza pesa. Tiketi ni bei nafuu sana. Baadhi ya vikundi vya wanafunzi vilikuwa vinanunua tiketi kwa bei nafuu zaidi. Watu wengi hawanunui shati rasmi za timu, hununua nje ya uwanja kwa dola 3,'' anasema Hassett.

''Mwishoni mwa mwaka jana, wakati hesabu za kufungua mwaka zikianza, swali lilikuwa; pesa zimeenda wapi? Kashfa ya ufisadi ilienea katika ofisi za juu za mchezo huo,'' anasema Hassett.

Kiungo wa kati wa zamani wa Everton na kocha mkuu wa zamani wa timu ya wanaume ya China, Li Tie, alichunguzwa kwa "ukiukaji mkubwa wa sheria," na mashtaka ya hongo yaliletwa mwezi Agosti.

Mwenyekiti wa zamani wa Chama cha Soka cha China, Chen Xuyuan anakabiliwa na shutuma kama hizo. Naye kiungo wa Korea Kusini, Son Jun-ho, aliyeichezea Shandong Taishan, akizuiliwa tangu mwezi Mei kwa tuhuma za kupokea hongo.

Sasa ni idadi ndogo tu ya wachezaji wa kigeni waliobaki kwenye ligi hiyo. Wachezaji wanaocheza nchini China kwa sasa, wa ndani na nje, hawakujibu maombi ya mahojiano kutoka BBC.

Bado kuna matumaini

Lakini pamoja na matatizo ya ligi, bado kuna ushabiki mkubwa wa soka la ndani. Tiketi za mechi ya kwanza ya timu ya Beijing Guoan zilipoanza kuuzwa mwezi Aprili, ziliuzwa ndani ya dakika tano.

Wakala wa soka aliyefanya kazi China na La Liga, Alberto Doldan anasema, "timu nyingi nchini China zimetoweka kutokana na matatizo ya kifedha. Lakini nadhani siku zijazo zitakuwa bora zaidi kwa sababu wamekuwa wakifanya kazi na wachezaji wachanga.''

"China bado ni mahali pazuri. Nadhani kuna mustakabali mzuri huko usoni kwa wachezaji wa ndani. Katika miaka mitano, sita au saba ijayo, tutapata wachezaji wengi wa ndani wenye kiwango cha juu zaidi.''

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah