Jinsi wanyanyasaji wa kingono walivyowalenga wanasoka watoto Gabon

TH

Na Suzanne Vanhooymissen & Tamasin Ford

BBC Africa Eye

Taasisi zinazosimamia soka zinakabiliwa na shutuma za kushindwa kuwalinda vijana waathiriwa wa unyanyasaji wa kingono nchini Gabon. BBC Africa Eye ilizungumza na zaidi ya mashahidi 30 ambao walieleza kuhusu mtandao ambao umeathiri vitengo vyote vya mchezo huo kwa miongo mitatu.

Onyo: Makala haya yana maelezo ambayo baadhi ya wasomaji wanaweza kukasirishwa nayo

Madai ya unyanyasaji wa kingono katika nchi ya Afrika ya kati ya Gabon yalianza mapema miaka ya 1990.

Mwathiriwa mmoja, ambaye hakutaka jina lake litajwe, alielezea kile kilichomtokea akiwa kijana katika kambi ya kandanda ya wachezaji wa chini ya miaka -17. Alisema yeye na rafiki yake wa karibu waliamshwa usiku wa manane na kupelekwa kwenye chumba chenye taa nyekundu, kilichokuwa na mtu aliyekuwa uchi wa mnyama.

“Walianza kunishikashika na rafiki yangu- sikuelewa , nikaanza kuomba, nikataka kutoka lakini mlango ulikuwa umefungwa, wakanishika na kunirusha chini, kulikuwa na walinzi wawili. Ni kana kwamba walikuwa wamejiandaa," alisema.

"Niliona jinsi walivyoanza kumbaka rafiki yangu. Nilimtazama machoni, naye akanitazama tena kana kwamba kuniambia : 'Hebu tuvumulie ili tumalizane nayo.' Nililia na kupiga kelele .

"Waliniambia sitachaguliwa kucheza tena na kwamba ikiwa nitathubutu kuzungumza na mtu yeyote kuhusu kile kilichotokea, familia yangu ingeuawa."

Hakuwahi kuichezea tena Gabon.

TH
Maelezo ya picha, Mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Gabon, Parfait Ndong, pichani hapa katika chuo chake, anasema alipuuzwa alipopaza sauti kuhusu dhulma hizo
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

BBC Africa Eye ilisikia kuwa kulikuwa na majaribio kadhaa ya kutahadharisha mamlaka kuhusu kile kilichokuwa kikifanyika kwa miaka mingi.

Mnamo 2019, mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Gabon Parfait Ndong alirudi nyumbani kuanzisha chuo chake cha mafunzo ya soka Jardin de football au Gabon. Baada ya kuichezea Gabon mechi 45 na kucheza soka barani Ulaya, ni mtu anayeheshimika katika soka ya Gabon. Alipojua kinachoendelea, alisema alitoa taarifa kwa mamlaka.

"Nilichukua hatua zote nilizoweza," aliambia BBC, na kuongeza kuwa alizungumza na rais wa ligi hiyo, rais wa shirikisho la soka la taifa, linalojulikana kama Fegafoot, na waziri wa michezo wakati huo.

Alisema baada ya juhudi hizi kupuuzwa, aligeukia vyombo vya habari vya ndani: "Hakuna aliyetaka kusikia nilichotaka kusema."

Haikuwa hadi gazeti la Guardian la Uingereza liliporipoti unyanyasaji huo mnamo Desemba 2021 , ambapo makocha wanne walikamatwa. Watatu kati yao wanasalia gerezani.

Katikati ya madai mabaya zaidi alikuwa Patrick Assoumou Eyi, anayejulikana sana kama "Capello". Kwa miongo kadhaa, alikuwa kocha mkuu wa timu za taifa za vijana za Gabon. Muhimu zaidi, Capello alikuwa na uwezo wa kuamua nani ataichezea Gabon katika kiwango hicho.

"Kimsingi alishikilia nafasi kama ya 'Mungu'kwa sababu kila mtu alimuabudu kama sanamu. Wale wanaosimamia vituo vya mafunzo, vyuo," alisema Ndong.

Mnamo Desemba 2021, kamati huru ya maadili ya Fifa ilianza taratibu za uchunguzi wa awali kuhusu ripoti za unyanyasaji wa kingono unaodaiwa kufanywa na Capello, na kumsimamisha kwa shughuli zote zinazohusiana na soka. Uchunguzi huu uliongozwa na kamati mpya ya maadili ya Fegafoot, na Mei 2022 chumba cha uchunguzi cha Fifa kilirasimisha uchunguzi wa awali.

TH
Maelezo ya picha, Mashahidi wanakadiria kwamba maelfu ya wavulana walitendwa vibaya

Kwa Loïc Alves, mshauri mkuu wa kisheria katika Fifpro - muungano wa kimataifa wa wachezaji wa kulipwa wa kandanda, kuruhusu Fegafoot kuongoza uchunguzi huo kulijumuisha "mgogoro wa kimaslahi katika kila ngazi".

"Muathiriwa anawezaje kuamini taasisi ile ile ambayo imewanyanyasa?" Aliuliza.

Capello alikiri mashtaka ya kubaka, kuwatayarisha na kuwanyanyasa wachezaji wachanga na bado yuko gerezani akisubiri hukumu. Makocha wengine waliokamatwa wanakanusha tuhuma zilizotolewa dhidi yao.

Maswali yameibuliwa kuhusu mamlaka zipi zilifahamu na lini.

Alexis, ambaye jina lake limebadilishwa ili kulinda utambulisho wake, alipanda safu ya vijana nchini Gabon na kwenda kucheza Ulaya. Aliambia BBC sababu pekee iliyomfanya aweze kuzungumza waziwazi ni kwa sababu hayupo tena nchini. Kama angekuwa, alisema, maisha yake yangekuwa hatarini.

"Kwa hiyo, walimkamata Capello lakini wamejua kwa muda gani na hawajafanya chochote kuhusu hilo? Walisimama kwa kiwango cha chini kabisa. Inakwenda hadi juu, lakini watafanya chochote ili kuifunika. Capello ametolewa kama kafara. Ni vichwa vilivyo juu ambavyo vinapaswa kuangushwa.."

Mwanasoka mwingine, ambaye tutamwita Julien, aliambia BBC kwamba yeye pia alidhulumiwa kuanzia umri wa miaka 14. Aliichezea timu ya taifa ya Gabon kwa miaka kadhaa na anaamini idadi ya wavulana walioathiriwa ni ngumu kufahamu.

"Sijui ni makocha wangapi walikuwa wakiwadhulumu wavulana, lakini kwa muda tumuangalie Capello peke yake, ndiye anayejulikana zaidi na amekuwa akifanya hivi kwa miaka 25 au 30. Kila mwaka amekuwa akifanya hivyo. kwa angalau wavulana 50, ikiwa sio zaidi," alisema.

"Sasa hebu tufikirie ni wangapi wengine walikuwa sehemu ya mtandao huo. Tunazungumza kuhusu maelfu ya wavulana."

Licha ya wito wa kumtaka mkuu wa Fegafoot Pierre-Alain Mounguengui kujiuzulu, alisalia madarakani na alichaguliwa tena Aprili 2022.

Bw Alves anaamini kuwa alipaswa kusimamishwa kazi: "Uzito wa madai ya kuficha mambo ulipaswa kusababisha kusimamishwa moja kwa moja, kusimamishwa kwa muda kabla ya uchaguzi."

Kama mkuu wa Fegafoot, Bw Mounguengui anaweza kuchukuliwa kuwa hafai kwa kutojua kinachoendelea au hatia ya kuficha unyanyasaji wa miaka mingi, alisema.

Wiki tatu baada ya kuchaguliwa tena, Bw Mounguengui alikamatwa na kushutumiwa kwa "kukosa kuripoti uhalifu wa dhulma za kingono dhidi ya watoto". Tofauti na Capello, Fifa haikumsimamisha kazi, na aliendelea kusimamia Fegafoot kutoka gerezani.

Sera ya Fifa ya kuwalinda watoto inasema: "Kumsimamisha kazi mfanyakazi wake wakati uchunguzi wa nje unafanyika na inapaswa kuwa jambo la kawaida."

Mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Gabon Rémy Ebanega, ambaye alianzisha muungano wa kwanza wa wachezaji wa kulipwa nchini humo mwaka 2014, ni - kama Ndong - mmoja wa watu wachache katika soka ya Gabon ambaye anahisi anaweza kuzungumza kwa uwazi. Yeye mwenyewe hakunyanyaswa lakini alisema ana marafiki kadhaa ambao walidhulumiwa.

"Mfumo wa haki nchini humo umemfunga rais wa shirikisho hilo, na Fifa haikufanya lolote. Kwa nini pia hakusimamishwa kazi huku uchunguzi ukiendelea kama walivyofanya na Capello?" alisema.

"Aliendelea kusimamia shirikisho hilo akiwa gerezani. Sidhani kama hilo halijawahi kutokea mahali pengine."

Mnamo Mei 2022, Fifa ilimsimamisha rasmi Capello, makocha wengine wawili na mkuu wa ligi ya kandanda, lakini haikumuwekea vikwazo Bw Mounguengui.

Wakati huo huo, Shirikisho la Soka barani Afrika (Caf) lilisema Bw Mounguengui alichukuliwa kuwa hana hatia hadi itakapothibitishwa na alimwandikia Waziri wa Michezo wa Gabon wakati huo Franck Nguema mnamo Aprili 2022 kuhoji kuzuiliwa kwake. Rais wa Caf Patrice Motsepe kisha alimtembelea bosi huyo wa Fegafoot jela miezi minne baadaye.

Baada ya takriban miezi sita gerezani, Bw Mounguengui aliachiliwa kwa muda. Wiki tatu baadaye, katika ufunguzi wa Kombe la Dunia la Fifa 2022 nchini Qatar, alipigwa picha akimkumbatia rais wa Caf.

TH
Maelezo ya picha, Bosi wa Fegafoot Pierre-Alain Mounguengui (kulia) akilakiwa kwa furaha na mkuu wa Caf kwenye sherehe za ufunguzi wa Kombe la Dunia tarehe 20 Novemba 2022.

Kwa Ebanega, mwaliko wa kwenda Qatar na bosi wa Fifa Gianni Infantino ulifanya ionekane kama shirikisho la soka duniani liliridhishwa na utendakazi wa Fegafoot: "Je, hiyo ndiyo unayoita kazi iliyofanywa vizuri? Kwa shirikisho kutoshughulikia unyanyasaji wa kingono?"

Miezi mitatu iliyopita, Bw Mounguengui alichaguliwa tena kwa nafasi ya juu zaidi ya Caf kama mwanachama wa kamati yake kuu. Wiki iliyopita, alipigwa picha pamoja na wasimamizi wa Caf mjini Cairo kwa ajili ya tangazo la waandalizi wa mashindani ya ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika.

Takriban miaka miwili baada ya madai hayo kufichuliwa katika vyombo vya habari vya kimataifa, viongozi wengi waandamizi huko Fegafoot wanasalia madarakani.

"Ninaamini mfumo huo uliweza kuendelea na kwamba bado unaweza kuendelea kwa sababu hakuna kilichobadilika," Ebanega alisema.

Kuna hofu ya kweli miongoni mwa watu wengi waliozungumza na BBC kuhusu madai ya unyanyasaji kuwa watoto bado wako hatarini.

"Nina hakika unyanyasaji bado unaendelea," Julien alisema.

Tuliyawasilisha madai hayo katika filamu ya BBC Africa Eye kwa Fegafoot, Caf na Fifa. Pande zote zililaani unyanyasaji wa watoto kwa namna yoyote ile kwa maneno makali zaidi.

Fegafoot na Bw Mounguengui walikanusha madai yote yaliyotolewa dhidi yao na kusema hatua mwafaka zilichukuliwa punde tu madai yoyote ya unyanyasaji wa kingono katika soka ya Gabon yaliwekwa wazi.

Walisema hawatambui ukosoaji wowote wa uchunguzi ulioanzishwa na kamati ya maadili ya Fegafoot Desemba 2021 tangu ilipoundwa kwa mujibu wa kanuni za shirikisho hilo.

Fifa na Caf zilikanusha tuhuma zote zilizotolewa dhidi yao, na kusema uchunguzi wa Fifa uliorasimishwa Mei 2022 bado unaendelea.

Vyombo vyote viwili vilisisitiza uchunguzi wao wote ulishughulikiwa kwa mujibu wa mahitaji yaliyotolewa na Kanuni za Maadili za Fifa, Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo, Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu na sheria ya Uswizi.

Caf ilisema kuwa Bw Motsepe alitembelea Gabon hasa ili kusisitiza kutovumilia kabisa kwa shirika hilo unyanyasaji wa kingono na kuunga mkono mamlaka za uchunguzi.

Aidha ilieleza kuwa Bw Mounguengui alikuwa mgeni katika Kombe la Dunia alipolakiwa na Bw Motsepe na hakuwa na mashtaka yoyote yanayomkabili.

Bw Nguema, ambaye si waziri wa michezo tena kufuatia mapinduzi ya mwezi uliopita, alikanusha vikali kufahamishwa na mtu yeyote kuhusu madai ya unyanyasaji wa kingono kabla ya kutangazwa hadharani.

Unaweza kutazama filamu kamili ya BBC Africa Eye Predators on the Pitch: Ndani ya Kashfa Kubwa Zaidi ya Soka barani Afrika kwenye chaneli ya YouTube ya BBC Africa .