Nini kilikuwepo angani katika wimbi la mashambulizi ya Iran na yalizuiwa vipi?

.

Chanzo cha picha, EPA

Kwa mara ya kwanza Iran imefanya mashambulizi dhidi ya ardhi ya Israel.

Katikati ya Jumamosi usiku, tahadhari za uvamizi wa anga zilitolewa nchini Israel, wakaazi walihimizwa kutafuta makazi huku milipuko ikisikika na ulinzi wa anga ukiwekwa katika tahadhari.

Vizuizi vilitanda angani usiku katika maeneo kadhaa nchini kote, huku ndege nyingi zisizo na rubani na makombora zikidunguliwa na washirika wa Israel kabla ya kufika katika eneo la Israel.

Takriban nchi tisa zilihusika katika shambulizi hilo la kijeshi - huku makombora yakirushwa kutoka Iran, Iraq, Syria na Yemen na kuangushwa na Israel, Marekani, Ufaransa na Jordan.

Mashambulizi yalihusisha droni, makombora ya cruise na ya balestiki

.

Chanzo cha picha, Reuters

Iran ilirusha zaidi ya ndege zisizo na rubani 300 na makombora kuelekea Israel, jeshi la Israel lilisema Jumapili.

Mashambulizi hayo yalijumuisha ndege zisizo na rubani 170 na makombora 30, ambayo hakuna hata moja lililoingia katika ardhi ya Israel, na makombora 110 ya balistiki ambayo idadi ndogo yao ilifika katika ardhi ya Israel, msemaji wa jeshi la Rear Admiral Daniel Hagari alisema katika taarifa yake kwa njia ya televisheni. BBC haijathibitisha takwimu hizo kwa kujitegemea.

Umbali mfupi zaidi kutoka Iran hadi Israel ni takriban kilomita 1,000 (maili 620) kuvuka Iraq, Syria na Jordan.

Uvamizi ulianzishwa kutoka nchi kadhaa

.

Chanzo cha picha, Reuters

Siku ya Jumamosi usiku Jeshi la Ulinzi la Iran Revolutionary Guards Corps (IRGC) lilisema kuwa limerusha ndege zisizo na rubani na makombora.

Vyanzo vya usalama vya Iraq viliiambia shirika la habari la Reuters kwamba makombora yalionekana yakiruka juu ya anga ya Iraq kuelekea Israel.

IRGC ilisema makombora ya balestiki yalirushwa karibu saa moja baada ya ndege zisizo na rubani zinazosonga polepole ili ziweze kuishambulia Israel kwa takriban wakati mmoja.

Idara ya ulinzi ya Marekani imesema wanajeshi wa Marekani walinasa makumi ya makombora na ndege zisizo na rubani zilizorushwa kutoka Iran, Iraq, Syria na Yemen.

Kundi la Hezbollah nchini Lebanon linaloungwa mkono na Iran pia limesema kuwa limerusha makombora mawili katika kambi ya kijeshi ya Israel katika eneo la Golan Heights linalokaliwa kwa mabavu ambalo Israel imeuteka kutoka Syria katika hatua ambayo haijatambuliwa na wengi wa jumuiya ya kimataifa.

Israel na washirika wake wamezuia idadi kubwa ya ndege zisizo na rubani na makombora

Takriban asilimia 99 ya mashambulizi yaliyokuwa yamerushwa yalinaswa nje ya anga ya Israel au juu nchi yenyewe, Admiral Daniel Hagari alisema.

Zilijumuisha ndege zisizo na rubani na makombora, ambayo hufuata njia bapa, na makombora mengi ya balestiki, ambayo hurushwa kwenye njia ambayo hutumia mvutano kufikia kasi ya juu sana.

Rais wa Marekani Joe Biden alisema majeshi ya Marekani "yaliisaidia Israel kuangusha takriban ndege zote" zisizo na rubani na makombora yaliyorushwa na Iran siku ya Jumapili. Katika taarifa yake, alisema Marekani ilihamisha ndege na meli za kivita katika eneo hilo kabla ya shambulio hilo ambalo halijawahi kutokea.

.

Vikosi vya Marekani vikiendeleza shughuli zake katika kambi zisizojulikana katika eneo hilo vilidungua ndege kadhaa zisizo na rubani za Iran kusini mwa Syria karibu na mpaka na Jordan, duru za usalama ziliambia Reuters.

Ndege za kivita za Uingereza za RAF Typhoon pia zilitumwa kutungua ndege zisizo na rubani. Zilipaa juu ya anga la Iraq na Syria lakini sio juu ya Israel.

Jordan - ambayo ina mkataba wa amani na Israel lakini imekuwa ikikosoa sana jinsi ilivyoendesha vita vyake dhidi ya kundi la Wapalestina la Hamas huko Gaza - pia ilinasa vitu vya kuruka vilivyoingia kwenye anga yake ili kulinda usalama wa raia wake, baraza la mawaziri la Jordan lilisema katika taarifa yake.

Ufaransa ilisaidia kushika doria kwenye anga lakini haikufahamika iwapo walidungua ndege zisizo na rubani au makombora, jeshi la Israel lilisema.

Ni makombora mangapi yalipita hadi ndani ya ardhi ya Israel na yalisababisha uharibifu gani?

Huko Jerusalem waandishi wa BBC waliripoti kusikia ving'ora na kuona mfumo wa ulinzi wa makombora wa Iron Dome wa Israel ukifanya kazi, ambao unatumia rada kufuatilia roketi na unaweza kutofautisha kati ya zile ambazo zina uwezekano wa kugonga maeneo yaliyojengwa na yale ambayo sio.

Makombora ya kuzuia yanarushwa tu kwa roketi zinazotarajiwa kushambulia maeneo yenye watu wengi.

Makombora machache ya balestiki yalipita na kushambulia eneo la Israel, Adm Hagari alisema.

Mmoja wao "aligonga kidogo" kambi ya jeshi la anga ya Nevatim katika jangwa la Negev kusini mwa Israel. Adm Hagari alisema kambi ya jeshi huo "bado inafanya kazi".

.

Shirika rasmi la habari la IRNA la Iran limesema shambulio hilo lilikuwa "pigo kubwa" kwa kituo cha jeshi la anga.

Kwa ujumla, takriban watu 12 walijeruhiwa upande wa Israel, Adm Hagari alisema.

Walijumuisha msichana wa miaka saba kutoka jamii ya Waarabu wa Bedouin karibu na mji wa kusini wa Arad, ambaye aliripotiwa kujeruhiwa na milipuko baada ya ndege isiyo na rubani ya Iran kunaswa angani. Alikuwa katika uangalizi maalum.

Jordan pia alisema kuwa baadhi ya vipande vilianguka kwenye eneo lake "bila kusababisha uharibifu wowote au majeraha yoyote kwa raia".

Nini kinafuata?

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kituo cha runinga cha Israel cha Channel 12 kilimnukuu afisa mmoja wa Israel ambaye hakutajwa jina akisema Israel itachukua hatua kwa "kujibu" shambulio hilo.

Anga ya Israel imefunguliwa tena kama ilivyo kwa nchi jirani, lakini Waziri wa Ulinzi Yoav Gallant alisema makabiliano na Iran "bado hayajaisha".

Wakati huo huo Iran imeionya Israel na kusema ikiwa Israel italipiza kisasi dhidi ya Iran, nayo "itatekeleza shambulizi kubwa zaidi kuliko hatua ya kijeshi ya leo usiku", mkuu wa majeshi Meja Jenerali Mohammad Bagheri aliiambia TV ya serikali.

Kamanda wa IRGC Hossein Salami pia alisema Iran italipiza kisasi dhidi ya shambulio lolote la Israel dhidi ya maslahi yake, maafisa au raia.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kukutana karibu 20:00 GMT kujadili mzozo wa hivi karibuni.

Bw Biden alisema pia atawakutanisha viongozi wa kundi la G7 la mataifa tajiri siku ya Jumapili ili kuratibu namna ya "kujibu kwa njia ya kidiplomasia" shambulio "baya" la Iran.