Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Majengo ya kihistoria ya Mosul yanavyojengwa tena baada ya uharibifu uliosababishwa na IS
Majengo ya kihistoria mjini Mosul, yakiwemo makanisa na misikiti, yanafunguliwa tena kufuatia uharibifu wa miaka mingi uliotokana na kutekwa kwa mji huo wa Iraq na kundi la Islamic State (IS).
Mradi huo ulioandaliwa na kufadhiliwa na Unesco, ulianza mwaka mmoja baada ya IS kushindwa na kufurushwa nje ya jiji hilo, kaskazini mwa Iraq, mwaka 2017.
Mkurugenzi mkuu wa Unesco Audrey Azoulay anahudhuria sherehe siku ya Jumatano kuashiria kufunguliwa tena.
Mafundi katika mji huo, wakazi na wawakilishi wa jumuiya zote za kidini za Mosul pia watakuwepo.
Mnamo 2014, IS ilidhibiti Mosul, ambayo kwa karne nyingi ilionekana kama ishara ya ustahimilivu na kuishi pamoja kati ya jamii tofauti za kidini na kikabila huko Iraqi.
Kundi hilo liliweka itikadi zake kali kwa jiji hilo, likiwalenga walio wachache na kuwaua wapinzani.
Miaka mitatu baadaye, muungano unaoungwa mkono na Marekani kwa ushirikiano na jeshi la Iraq na wanamgambo wenye uhusiano na serikali walipanga mashambulizi makali ya ardhini na angani ili kuuteka mji huo kutoka kwenye udhibiti wa IS.
Vita vya umwagaji damu zaidi vililenga Jiji la Kale, ambapo wapiganaji wa kundi hilo walipambana hadi tone la mwisho.
Mpiga picha wa Mosul Ali al-Baroodi anakumbuka hali ya kutisha iliyomkumba alipoingia eneo hilo kwa mara ya kwanza muda mfupi baada ya vita vya mtaa kwa mtaa kumalizika majira ya kiangazi ya 2017.
Aliona mnara uliovutia wa al-Hadba, unaojulikana kama "nembo", ya Mosul kwa mamia ya miaka, ikiwa gofu.
"Ilikuwa kama mji wa mauti," anasema. "Miili ya watu waliokufa imetapakaa pande zote, harufu mbaya na matukio ya kutisha katika anga hilo.
"Halikuwa jiji ambalo tulilifahamu - lilikuwa na mabadiliko - ambayo hatukuwahi kufikiria hata katika ndoto zetu mbaya zaidi tulizowahi kuota. Nilinyamaza baada ya hapo kwa siku kadhaa. Nilipoteza sauti yangu. Sikutambua tena.
Asilimia 80 ya Mji Mkongwe wa Mosul, kwenye ukingo wa magharibi wa Tigris, uliharibiwa wakati wa uvamizi wa IS kwa miaka mitatu.
Haikuwa tu makanisa, misikiti na nyumba kongwe ambazo zilihitaji kurekebishwa, lakini pia maisha ya kijamii ya wale ambao walikuwa wameishi huko kwa muda mrefu kwa uwiano kati ya dini na makabila.
Kazi kubwa ya kujenga upya ilianza chini ya ufadhili wa Unesco kwa bajeti ya $115m (£93m) ambayo shirika hilo lilifanikiwa kuitayarisha, nyingi kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu na Umoja wa Ulaya.
Padre Olivier Poquillon - kasisi wa Dominica - alirudi Mosul kusaidia kusimamia urejeshaji wa moja ya majengo muhimu, nyumba ya watawa ya Notre-Dame de l'Heure, inayojulikana kama Al-Saa'a, ambayo ilianzishwa karibu miaka 200 iliyopita.
"Tulianza kwa kujaribu kwanza kukusanya timu - timu inayoundwa na watu kutoka Old Mosul kutoka madhehebu tofauti - Wakristo, Waislamu wanaofanya kazi pamoja," anasema.
Padre Poquillon anasema kuwa kuzikutanisha jumuiya hizo ilikuwa ni changamoto kubwa na mafanikio makubwa zaidi.
"Kama unataka kujenga upya majengo kwanza ni kujenga upya uaminifu - ikiwa hutajenga upya uaminifu, hakuna maana kujenga upya kuta za majengo hayo kwa sababu yatalengwa kushambuliwa na jumuiya nyingine."
Msimamizi wa mradi mzima - uliojumuisha urejeshaji wa nyumba 124 kuukuu na majumba mawili ya kifahari - amekuwa mbunifu mkuu Maria Rita Acetoso, ambaye alikuja Mosul moja kwa moja kutoka kwenye kazi ya ukarabati wa Unesco nchini Afghanistan.
"Mradi huu unaonyesha kuwa utamaduni pia unaweza kutengeneza ajira, unaweza kuhimiza maendeleo ya ujuzi na kwa kuongeza unaweza kuwafanya wale wanaohusika kujisikia kuhusika na wenye thamani," anasema.
Anatumai ujenzi huo unaweza kurejesha tumaini na kuwezesha urejesho wa utambulisho wa kitamaduni wa watu na kumbukumbu yao.
"Nadhani hii ni muhimu hasa kwa vizazi vinavyokua katika hali ya migogoro na ukosefu wa utulivu wa kisiasa," anaongeza.
Unesco inasema kuwa zaidi ya vijana 1,300 wa eneo hilo wamefunzwa ujuzi wa kitamaduni, wakati ajira mpya 6,000 zimetolewa.
Zaidi ya madarasa 100 yalifanyiwa ukarabati mjini Mosul. Maelfu ya vipande vya mabaki ya kihistoria vilipatikana na kuorodheshwa kutoka kwenye vifusi.
Kati ya wahandisi wengi waliohusika katika ujenzi huo, 30% walikuwa wanawake.
Miaka minane kuendelea, kengele zinalia tena kote Mosul kutoka Kanisa la al-Tahera, ambalo paa lake liliporomoka baada ya uharibifu mkubwa chini ya IS mwaka 2017.
Alama nyingine kuu za Mosul pia zimerejeshwa - mnara ule unaotamba wa al-Hadba, Kituo cha watawa cha Dominica al-Saa'a na msikiti mkubwa wa Al-Nouri.
Na watu wameweza kurejea kwenye nyumba ambazo zimekuwa makazi ya familia zao kwa karne nyingi.
Mkazi mmoja, Mustafa, alisema: "Nyumba yangu ilijengwa mwaka wa 1864 - kwa bahati mbaya iliharibiwa kwa sehemu wakati wa ukombozi wa Mosul na haikufaa kuishi hapo, hasa na watoto wangu.
"Kwa hiyo niliamua kuhamia nyumbani kwa wazazi wangu. Nilifurahishwa na kuguswa sana kuona nyumba yangu ikijengwa upya."
Familia ya Abdullah pia imeishi katika nyumba iliyoko Jiji la Kale tangu Karne ya 19 wakati eneo hilo lilikuwa kitovu cha biashara ya pamba - ndiyo maana anasema nyumba yao ni ya thamani sana kwao.
"Baada ya Unesco kunijengea nyumba yangu, nilirudi," anasema. "Siwezi kuelezea hisia niliyokuwa nayo kwa sababu baada ya kuona uharibifu wote uliotokea huko, nilifikiri sitaweza kurudi na kuishi huko tena."
Makovu ya kile watu wa Mosul walivumilia bado hayajapona - sawa na vile sehemu kubwa ya Iraq inavyosalia katika hali tete.
Lakini kuzaliwa upya kwa Jiji la Kale kutoka kwenye vifusi kunawakilisha matumaini ya mustakabali mwema - huku Ali al-Baroodi akiendelea kuhifadhi mabadiliko ya nyumba yake anayoipenda siku baada ya siku.
"Kwa kweli ni kama kuona mtu aliyekufa akifufuka kwa njia nzuri sana - hiyo ndiyo hakika na kweli jiji kufufuliwa," anasema.