Simulizi ya Binti wa miaka 19 mkimbizi kutoka DR Congo alivyotekwa na kundi la MaiMai

w
Maelezo ya picha, Noella alipata ujauzito wa kiongozi wa kundi la Mai mai baada ya kutekwa nyara
    • Author, Peter Mwangangi
    • Nafasi, BBC News

Ikiwa ni siku chache tu tangu siku ya wakimbizi Duniani kuadhimishwa, BBC inaangazia simulizi ya Noella Jeanne, msichana wa umri wa miaka 19 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambaye sasa anaishi nchini Kenya. Alitekwa na kundi la Maimai na kupewa ujauzito akiwa na miaka 13 tu.

Kutekwa na kundi la Maimai

Akiwa na miaka 13 Kijiji cha Noella kilivamiwa na kundi la waasi, katika harakati za kukimbia akaanguka mikononi kwa waasi hao na kupelekwa katika makazi ya kundi hili eneo la msituni.

Baaada ya kuchukuliwa na kundi hilo, kiongozi wake akaamua kuwa Noella atakua kama mke wake.

‘’Mkubwa wao akawaambia mimi nitakua bibi yake, na mimi nilikua mtoto mdogo. Baada ya mizei mitatu nikapata mimba, wakanipeleka katika hospitali yao, nikahudumiwa nikajifungua salama’’ Anasimulia Noella.

Noella alijifungua salama, anasema kuwa baada ya mtoto wake kufikisha miezi miwili ulinzi ukapungua, kundi hilo la Mai mai likaona kuwa sasa amekuwa miongoni mwa jumuiya yao.

Ndio akaanza harakati yake ya kujinasua katika kundi hilo yeye na mtoto wake mchanga.

w
Maelezo ya picha, Noella sasa amehifadhiwa na shirika la RefuSHE nchini Kenya.

Kutoroka na kulala porini na mtoto wa miezi miwili

Maelezo ya video, Wakati kijiji chao kiliposhambuliwa mnamo mwaka 2016, Noella alikimbilia usalama lakini badala yake akajikuta mikononi mwa waasi wa MaiMai.

Baada ya Noella kuona kuwa ulinzi wake umepungua siku moja akafanya maandalizi ya kutoroka.

‘’Mtoto alipofikisha miezi miwili wakasema huyu amezoa hakuna haja tena ya kumlinda, nikaanza kutayarisha vitu nitakavyotoroka navyo, nikachukua maziwa, nguo ya kumfunika mtoto na sukari, ilikua asubuhi walivyoondoka tu na mimi nikaanza kuondoka.

Noella anasimulia kuwa usiku ulipoingia akiwa na mtoto wake alitafuta sehemu ambayo haiku na miti mingi ili kuepuka Wanyama wakali, wakalal hapo na mtoto wake hadi asubuhi.

Alilala kwa siku mbili katika msitu kisha kukutana na watu wazuri waliomsaidia hadi kufika mpaka wa Kenya.

w
Maelezo ya picha, Noella pamoja na wasichana wengine wakimbizi wakishona nguo

Maisha yake ya sasa

Noella kwa sasa anaishi nchini Kenya na anapatiwa usaidizi na kundi la RefuSHE e linaloshughulikia wanawake na wasichana wakimbizi

Kwa mujibu wa mkuu wa programu wa shirika la RefuSHE Rose Kanana, anasema kuwa shirika huwapokea wakimbizi hao kisha kuwaelekeza katika huduma mbalimbali.

Kama kutengeneza nguo ambazo huuzwa maeneo mbalimbali Duniani.

Anajishughulisha na kushona na kuandaa mitindo ya nguo nchini Kenya, Noella ana ndoto ya kuwa mwanamitindo mkubwa na kujulikana maeneo mbalimbali Duniani.

w
Maelezo ya picha, Nguo hizi hutengenezwa na wasichana na wanawake wenye simulizi kama ya Noella.

Kundi la Mai mai au Mayi mayi ni kundi la aina gani?

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Vikundi vya sasa vya Mai-Mai vina mizizi yao ya moja kwa moja kati ya vikundi vilivyojihami vilivyotokea mapema miaka ya 1990. Kipindi hiki kiliadhimishwa na mchakato changa wa demokrasia ambao ulianzisha ghiliba za kisiasa za migogoro ya ardhi, mamlaka za mitaa na upatikanaji wa rasilimali mashariki mwa nchi wakati huo ikijulikana kama Zaire. Mingi ya migogoro hii ilikua nje ya kipindi cha ukoloni, wakati wakoloni waliyapa makundi fulani milki za kimila lakini wakawatenga wengine, na kuandaa uhamiaji mkubwa wa Wanyarwanda kwenda Kongo kufanya kazi kwenye mashamba na migodini.

Baada ya muda Vikundi vya Mai-Mai vilizidi kutenganishwa na jamii walizotoka na kuanza kufuata ajenda zao. Makundi kadhaa yalishirikiana na vuguvugu kubwa la kisiasa-kijeshi, ambalo wakati mwingine pia lilitoa mafunzo ya kijeshi. Wengi walinaswa katika ushindani wa upatikanaji wa maliasili, kama vile dhahabu na mbao.

Katika majimbo ya Kivu pekee kwa sasa kuna zaidi ya vikundi 130 vilivyo na silaha. Mengi ya makundi haya yanajiita "Mai-Mai"-neno mwavuli kwa makundi yenye silaha yanayodai kujihusisha na "kujilinda" dhidi ya "wageni".

Kulingana na ripoti ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2001, wapinajai wa Mai-Mai 20,000 hadi 30,000 walikuwa katika majimbo mawili ya Kivu.

Kiongozi mwingine wa Mai-Mai, Kanali Mayele, alikamatwa na vikosi vya Umoja wa Mataifa mnamo Oktoba 2010, akidaiwa kuwa kiongozi wa matukio ya ubakaji mkubwa katika eneo la Walikale katika jimbo la Kivu Kaskazini.

Katika kipindi chote cha mzozo wa kivita, Mai-Mai walikuwa miongoni mwa wapiganaji waliohusika na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu ikiwa ni pamoja na mauaji haramu, ubakaji na utesaji na matumizi ya askari watoto.

Wasichana katika Mai-Mai mara nyingi hutekwa nyara, kubakwa na kutumiwa kwa madhumuni ya ngono. Ubakaji wa wanawake na watoto wa kiraia uliofanywa na Mai-Mai wakati na baada ya mapigano ya kivita pia umethibitishwa vyema na Umoja wa Mataifa na mashirika ya haki za binadamu.