Kwa nini Nicaragua inawafukuza viongozi wa Kikristo?

5tgfvb

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Mapema mwaka jana, serikali ya Nicaragua iliwakamata viongozi kadhaa wa Kikatoliki, akiwemo Askofu wa Kanisa Katoliki nchini humo Rolando Alvarez, na kuwafunga katika jela la La Modela - kilomita 12 kutoka mji mkuu wa Nicaragua, Managua.

Askofu Rolando alihukumiwa kifungo cha miaka 26 jela - kwenye gereza lenye wadudu na lina wafungwa wengi kuliko uwezo wake - kwa kukosoa ukatili wa Rais Daniel Ortega.

Katika kesi hiyo, viongozi wa Kanisa Katoliki la Roma mjini Vatican na Marekani walishinikiza kwa takribani siku 500 kuachiliwa Askofu huyo na wenzake waliokuwa wamefungwa katika gereza moja.

Pia unaweza kusoma

Ukandamizaji wa upinzani

gfv

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Rais wa Nicaragua Daniel Ortega na Rais wa Cuba Miguel Diaz.

Daniel Ortega, rais wa Nicaragua aliingia madarakani mwaka 2007. Mwaka 2018, maandamano yalianza kote Nicaragua dhidi ya serikali ya Ortega.

Ndiposa, Daniel Ortega alipoanza kukandamiza maandamano hayo. Kufikia mwisho wa mwaka, vikosi vya usalama vya serikali vilikuwa vimewaua na kuwakamata mamia ya watu.

Bianca Jagger, rais wa shirika la kutetea haki za binadamu la Bianca Jagger Foundation for Human Rights, akizungumza na BBC, alisema, “tulipokuwa tukiandamana, vikosi vya usalama vilianza kuwafyatulia risasi waandamanaji. Watu 19 waliuawa na 180 kujeruhiwa siku hiyo."

Alisema Rais Daniel Ortega na Makamu wa Rais Rosario Morello walitayarisha orodha ya wale ambao wanapingana na serikali, ambayo ni pamoja na majina ya wawakilishi wengi wa kidini.

“Orodha hiyo pia ilikuwa na majina ya viongozi wa Kanisa Katoliki waliojaribu kuwatetea wanafunzi wa vyuo vikuu waliouawa na vikosi vya usalama. Viongozi hawa walikosoa serikali,” anasema Bianca Jagger.

Mwaka uliofuata, wengi walioipinga serikali walifungwa au kuuawa. Ikijumuisha viongozi wengi wa kidini.

Ukandamizaji zaidi

GF

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Bianca Jagger anasema, viongozi wa kidini wasiopungua 200 walifungwa jela au kulazimishwa kukimbia nchi. Wengi wao walinyang'anywa uraia wao.

''Daniel Ortega na Rosario Morello wanaharibu Kanisa Katoliki nchini humo na hakutakuwa na kasisi wala kiongozi atakayesalia,'' anasema Bianca Jagger.

Bianca Jagger anaeleza, “Askofu Alvarez, alihudhuria mazungumzo kati ya Ortega, upinzani na viongozi wa wanafunzi, alisema nchi hii inataka mabadiliko. Lakini Ortega hakuafiki hilo. Hivyo alimfanya Askofu Alvarez kuwajibika kwa maneno yake.”

Mwezi Februari 2023, serikali iliwapeleka zaidi ya wafungwa 200 wa kisiasa kutoka Nicaragua hadi Marekani.

Ilijumuisha wanahabari wengi, viongozi wa wanafunzi na viongozi wa upinzani. Lakini Askofu Alvarez alipatikana na hatia ya uhaini na kuhukumiwa kifungo cha miaka 26 jela.

Kanisa linasemaje?

FVC

Chanzo cha picha, USCIRF

Maelezo ya picha, Askofu Rolando
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kulingana na baadhi ya ripoti, Papa Francis amelinganisha vitendo vya Ortega na utawala wa Nazi. Hilo lilmkasirisha Ortega. Alifunga mlango wa mazungumzo na Kanisa na kumrudisha balozi wa Vatican kurudi Roma.

Akizungumza na wafuasi wa Kikristo katika Siku ya Mwaka Mpya wa 2024, Papa Francis alisema ana wasiwasi kuhusu hali ya huko na viongozi wa kidini wa Kikristo wa Nicaragua wamenyimwa uhuru wao.

Tulizungumza na Andrea Cagliarducci, mtaalamu wa masuala ya Vatican katika shirika la habari la Kikatoliki huko Roma, na kuuliza kwa nini mwitikio wa Vatican dhidi ya ukandamizaji wa Nicaragua haujakuwa mkubwa.

Alijibu kwa kusema, “Maaskofu na viongozi wengine wa kidini nchini Nicaragua wamefungwa kwa kosa la uhaini. Vikundi vya wapiganaji vinawalenga viongozi wa kidini pia. Hali nchini Nicaragua ni tofauti.”

''Papa anashughulikia suala hilo kwa tahadhari, akizingatia tishio kwa maisha ya watu muhimu wa Kikatoliki wanaoishi Nicaragua. Lakini kuna sababu zingine,'' anasema Andrea.

Kukata uhusiano wa Vatican kwa nchi yenye Wakatoliki wengi kama Nicaragua kunaweza kusababisha matatizo kama ya China na Korea Kaskazini, ambazo tayari zinazozana na Vatican.

Marekani inafanya nini?

FD

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Daniel Ortega akihutubia wafuasi wake

"Hakuna mahali pengine ambapo mateso ya Wakatoliki na viongozi wa upinzani ni makubwa kama Nicaragua," anasema Ryan Berg, mkurugenzi wa Mafunzo ya Kimkakati na Kimataifa katika Kituo chenye makao yake makuu mjini Washington.

Kutokana na ukweli kwamba ukiukwaji wa haki za binadamu ni jambo la kawaida katika nchi hiyo, ukandamizaji unaoendelea katika nchi hii bado haujulikani kwa kiasi kikubwa.

"Hakuna mtu aliyewahi kuzungumza kuhusu ukandamizaji unaoendelea Nicaragua kwa sababu eneo hilo lina matatizo yake ya ndani,” anasema.

Ryan Berg, anasema ''Marekani iliacha kuifuatilia Nicaragua baada ya Vita Baridi, na kwa sasa inapambana na shida zingine ulimwenguni.''

"Tumetoka kuiangalia Nicaragua kwa mtazamo wa demokrasia na haki za binadamu hadi tatizo la madawa ya kulevya na uhamiaji haramu na udikteta.''

''Hali imebadilika sana tangu Vita Baridi. Sasa tunaona Nicaragua ikiendeleza uhusiano na Urusi, China na Iran. Marekani inapaswa kuunda mkakati katika suala hili," anasema.

Je, Vatican inaweza kukomesha mateso?

v

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Papa Francis

Viongozi wakuu wa kidini wa Nicaragua wamekuwa wakikosoa waziwazi ukandamizaji ulioanzishwa na Ortega dhidi ya viongozi wa upinzani na viongozi wa Kikristo.

Ortega amejibu kwa kuwakamata, kuwafukuza kutoka nchini na kukata uhusiano na Vatican.

Mwaka huu Papa ameeleza hadharani wasiwasi wake kuhusu kuteswa kwa viongozi wa Kikatoliki nchini Nicaragua.

Baada ya kuachiliwa kutoka Nicaragua, Askofu Alvarez alirudi Roma.

Swali, ni nini kingine ambacho Vatican inaweza kufanya kuhusu hilo? Katika historia ya Vatican, tunaweza kuona imetekeleza maamuzi yake ya kidiplomasia katika miktadha mingi tata kama hii.

Lakini wakati huu, dunia inapaswa kukusanyika pamoja kusaidia Vatican kutatua tatizo hili.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi.