Je, unajua kuna Wakristo hawasherehekei Krismasi?

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Krismasi ni sikukuu inayosherehekewa na Wakristo wengi duniani - wanaamini ni siku ambayo Yesu alikuja ulimwenguni ili kuuokoa kutokana na dhambi.
Tarehe 25 Disemba inakubaliwa na idadi kubwa ya waumini wa Kikristo duniani kote husherehekea Krismasi.
Hata hivyo, baadhi ya wakristo hubisha kwamba Biblia, kitabu kitakatifu cha Wakristo, haisemi kwamba Yesu alizaliwa Disemba 25.
"Ni vigumu kukubali Yesu alizaliwa Disemba"

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Miongoni mwa makanisa ya Kikristo kama lile la nchini Sri Lanka, The Center Church - ni kanisa ambalo halikubali kwamba Yesu Kristo alizaliwa Disemba. Badala yake wanaamini Yesu alizaliwa kati ya Aprili au Agosti.
"Ni vigumu kukubali Yesu alizaliwa Disemba. Tunaamini alizaliwa Aprili au Agosti. Krismasi inatokana na sherehe nyingine za zamani," anasema mfuasi wa Kanisa la The Center (sio jina lake halisi).
“Sikukuu hii sio sikukuu iliyoanzishwa kusherehekea kuzaliwa kwa Yesu, ilikuwa ni sikukuu iliyokuwepo zamani sana kwa ajili ya kumuenzi Mungu wa Jua, baada ya muda fulani ikawa sikukuu ya Krismasi, kwa hiyo ni makosa kuitumia sikukuu hiyo kusherehekea kuzaliwa kwa Yesu."
Hata hivyo, Wakristo wanaosherehekea Krismasi Disemba 25 wanasema kusherehekea Krismasi siku hiyo si kosa, hata ikiwa kuna sherehe nyinginezo za Desemba 25.
"Tunasherehekea kuzaliwa kwa Yesu na ujumbe alioleta ulimwenguni. Hakuna haja ya kuleta hoja kuhusu tarehe," anasema muumini wa kanisa la Methodist.
Sera ya Kanisa la The Center ya kukataa Krismasi imelegezwa kwa kiasi fulani. Wafuasi wa kanisa hilo wanasema ingawa hawakuwahi kusherehekea Krismasi hapo awali, wamepanga kusherehekea mara hii – licha ya ukweli kwamba hawakubali kuwa Yesu alizaliwa Disemba 25.

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Madhehebu mengine maarufu ni Waadventista Wasabato – wafuasi wake huabudu siku ya Jumamosi, siku ya Sabato ya Kiyahudi. Waadventista Wasabato hawaitambui Disemba 25 kama siku rasmi ya kusherehekea kuzaliwa Yesu.
Mashahidi wa Yehova Jehova Witness) ni mojawapo ya kundi kubwa la Wakristo ambao hawasherehekei Krismasi. Hapo zamani Mashahidi wa Yehova walikuwa wakisherehekea Krismasi hadi 1928, baada ya utafiti wao.
Waliacha kusherehekea Krisimas walipogundua inatokana na sherehe ya kipagani na Bibilia haijasema kuhusu kusherehekea kuzaliwa Yesu. Hata hivyo, hawawazuii wengine kuheshimu siku hiyo.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi












