Hassassin: Kundi la wauaji lililoangamiza wakuu wengi wa Kiislamu na Kikristo

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
- Author, Juan Francisco Alonso
- Nafasi, BBC
Katika kitabu cha msafiri wa Italia, Marco Polo kiitwacho Book of Wonders, kinaeleza juu ya kundi la Waislamu walioleta hofu Mashariki ya Kati miongoni mwa Wakristo na wafuasi wa Mtume Muhammad; wakiitwa hassassin au hashshashin.
Neno hilo ndilo asili ya neno la Kiingereza assassin (muuaji), ambalo linatumika hadi leo.
Moja ya tukio linalohusishwa na kundi hilo lilitokea Aprili 28, 1192 katika jiji la Tiro (Lebanon ya sasa). Mmoja wa viongozi wa Vita vya Tatu vya Msalaba (Mtaliano), alikuwa akijiandaa kusheherekea kuchaguliwa kwake kuwa mfalme wa Jerusalem.
Hata hivyo, sherehe haikwenda kama ilivyopangwa. Kwa mujibu wa wanahistoria, wajumbe wawili walipeleka barua kwa mtukufu huyo na wakati anaisoma walitoa majambia na kumchoma.
Ingawa utambulisho wa washambuliaji haujawahi kuwekwa hadharani, lakini imethibitishwa walikuwa wanachama wa kikundi cha Hassassin (assassin), ambacho kwa miaka mingi kimechochea waandishi kuandika riwaya, kutengenezwa filamu na hivi karibuni mchezo wa video wa Assassin's Creed umeundwa.
Zao la mifarakano ya Waislamu

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Profesa wa masomo ya Kiarabu na Kiislamu katika Chuo Kikuu cha Autonomous Madrid, Ignacio Gutiérrez de Terán, anasema chimbuko la kundi hili lilianzia kwenye mgawanyiko wa Waislamu 632 baada ya kifo cha Mtume Muhammad.
Tofauti ikajitokeza juu ya suala la nani angemrithi kama imamu (kiongozi) wa Waislamu, lilisababisha mgawanyiko wa wale tunaowajua leo kama Mashia na Sunni.
Katika karne ya 9, mzozo mpya miongoni mwa Mashia ulizuka juu ya uongozi wa madhehebu hayo na madhehebu mapya ya Kishia yaliyozuka ya Ismaili, kutoka kwa Imam Ismail ibn Ja'far. Madhehebu hayo mapya pia yalikumbwa na mgawanyiko kwa sababu ya mabishano juu ya nani anapaswa kuliongoza.
Sehemu ya madhehebu hayo yalimuunga mkono Nizar, ambaye baada ya kunyakua mamlaka huko Alexandria (Misri), aliuawa na wafuasi wa kaka yake mdogo, aliyetawala huko Cairo.
Wafuasi wa Nizar walihamia Uajemi, ambako walieneza imani yao, ingawa hazikukubaliwa na Wasunni wala Mashia. Nizarides walijumuisha vipengele vya falsafa ya Kigiriki na tafsiri nyingine za siri za Uislamu.
Ili kuepuka manyanyaso, kikundi hicho kilianzisha mtandao wa wamishonari. Mmoja wa wahubiri wao wa karne ya 11, ni kijana Mwajemi aitwaye Hasan-i Sabbah, ambaye alisilimu na pia kuunda jumuiya ya siri ya Hassassins.
"Hassassin walikuwa na itikadi kali. Ni vuguvugu la kijamii ambalo lilitumia dini kama kisingizio. Na kabla ya kuangamizwa, walikuwa na mawazo ya kigaidi," anasema Profesa wa masomo ya Kiislamu Emilio González Ferrín kutoka Chuo Kikuu cha Seville.
Katika Milima

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Walijaribu kuunda taifa lao wenyewe, lakini walishindwa. Hasan-i Sabbah alirudi kwenye milima ya Iran na kuteka ngome isiyoweza kushammbuliwa ya Alamut katika safu ya milima ya Elburz (kilomita 100 kaskazini mwa Tehran).
“Ngome hii ilikuwa makao makuu ya mtandao wa ngome zilizoshikiliwa na Wanizari ambazo zilienea hadi Syria na Lebanon ya leo.
Kutoka hapo mwanzilishi wa kundi hilo, ambaye baadaye alijulikana kama Mzee wa Mlima, alitafuta ushawishi wa kisiasa katika mataifa ya Kiislamu," anaelezea Gutiérrez de Terán.
Ili kufikia malengo yake, Hasan-i Sabbah aliunda kikosi cha wanamgambo wenye mafunzo ya hali ya juu, alikitumia kushambulia watu maalum katika maeneo ya Waislamu na Wakristo.
"Kwa vile hawakuruhusiwa kushika madaraka, na hawakuwa na nguvu za kuchukua au kudhibiti nchi, ndipo waliamua kufanya kazi ya mauaji , iwe wanaweza kutoroka au la,” anasema González Ferrín.
Mwanahistoria huyo analielezea vuguvugu lililoongozwa na Hasan-i Sabbah halikuwa maarufu wala halikuwa na watu wengi, bali lilitumia akili sana. Lilikuwa na mwelekeo wa kidini wa itikadi kali.
Vyanzo vya Kiislamu vinawataja watu hao kwa jina lao halisi; fedayeen (wale wanaojitolea kwa ajili ya wengine), kama hashshashin, neno la Kiarabu kwa watumiaji wa hashish.
Kwa nini waliitwa hivyo? “Inasemekana Hasan-i Sabbah, wakati wa mafunzo, alizungumza nao kuhusu pepo, kisha aliwalisha majani ya bangi na kuyatafuna au kuyameza; na kuanzia hapo akawapa kazi ya kufanya mauaji,” Gutiérrez de Terán alieleza.
Lakini González Ferrín anaamini simulizi hiyo sio ya kweli na imeelezwa kwa sababu tu ya ukosefu wa ufahamu wa mbinu zilizokuwa zikitumiwa na kikundi hicho na ni jaribio la kulidharua kundi hilo.
Mbinu zao za Mauaji

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Ununuzi au utekaji nyara wa watoto wadogo ni baadhi ya njia zilizotumiwa na Hasan-i Sabbah na warithi wake ili kuongeza safu ya wanamgambo.
Baada ya kuajiriwa, wanachama wapya walifundishwa sio tu mapigano, pia lugha, utamaduni na desturi za vijiji au miji ambayo walipaswa kwenda kuua.
"Walikuwa kama ninja, wapiganaji waliojua namna ya kuingia katikati ya watu," González Ferrín anasema.
Gutiérrez de Terán anasema, "ni watu waliokuwa na elimu na tamaduni, waliojua mila na hata lahaja na tabia ya wakazi wa maeneo ambayo walikwenda kutekeleza mashambulizi yao."
Uwezo wao wa kujipenyeza, usahihi katika mashambulizi na ukatili wao ndio vimewafanya wawe maarufu na kuogopwa.
Ili wanachama wake wawe tayari kujitolea, Hasan-i Sabbah anawaweka katika mafundisho ya kidini huko Alamut. Ngome hiyo ilikuwa muhimu ili kuwezesha mafundisho haya, kwa mujibu wa Marco Polo.
Kuangamizwa baada ya Karne na Nusu

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Kundi hilo liliweza kuishi kwa miaka 166 hadi adui kutoka kaskazini alipowaangamiza, Wamongolia.
"Wamongolia walikuwa tishio kubwa zaidi kuliko Wapiganaji wa Msalaba, kwa sababu walikuwa makatili. Kwa hiyo Wanizari walijaribu kufanya makubaliano nao, lakini walishindwa," anaeleza Gutiérrez de Terán.
Jeshi la kutisha la Hulagu Khan, mjukuu wa Genghis Khan, lilikwenda kwenye ngome hiyo na kuiharibu yote. Kwa mujibu wa baadhi ya simulizi, Hulagu Khan aliamini kundi hilo lilikuwa limemuua mmoja wa wajomba zake.
Lakini kabla hilo halijatokea, viongozi na wakuu wengi wa Kiislamu na Kikristo waliangamia mikononi mwa kundi hilo.
Walioponea Chupuchupu

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Sultan Saladin, mmoja wa watu muhimu sana katika Uislamu, ambaye aliiteka tena Jerusalem kutoka kwa Wapiganaji wa Msalaba katika karne ya 12, alikuwa mmoja wa walengwa wa Hassassin, lakini aliweza kuokoa maisha yake.
"Saladin aliongoza mfululizo wa kampeni za kuwafukuza Wapiganaji wa Msalaba, lakini alitambua ili kufikia hili alipaswa pia kuondoa majimbo na falme fulani za Kiislamu, zile ambazo zilishirikiana na Wapiganaji wa Msalaba. Wakati wa kampeni hii, alilenga Masyaf, ngome ya Nizarid huko Syria ya sasa,” anasema Gutiérrez de Terán.
Wananizari walijibu haraka, na 1185 walituma wauaji ili wamuue.
"Wauaji hao waliingia ndani ya kambi ya Saladin, wakiwa wamevaa kama askari wake na kujaribu kumuua kwenye hema lake, lakini hawakufanikiwa kwa sababu ya koti zito na kofia la chuma,"anasema Profesa kutoka Chuo Kikuu cha Autonomous cha Madrid.
Mfalme Edward wa Kwanza wa Uingereza, ambaye alishiriki katika Vita vya Msalaba vya 9, pia aliponea chupuchupu kuuawa na mmoja wa wafuasi wa kundi hilo mwaka 1272.
Pia walitoa huduma zao za kuuawa kwa Waislamu na Wakristo na kupewa malipo ya kiasi kikubwa cha fedha. Na kuwa waasisi wa huduma ya kuua ambayo imedumu kwa karne nyingi.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Lizzy Masinga












