Matokeo ya Uchaguzi Kenya 2022: Kwa nini hesabu inachukua muda mrefu

Na Dickens Olewe BBC News, Nairobi

th

Chanzo cha picha, Reuters

Wakenya bado hawajui rais wao ajaye atakuwa nani zaidi ya saa 45 baada ya vituo vya kupigia kura kufungwa.

Mkuu wa uchaguzi Wafula Chebukati amewataka watu kuwa na subira na kutokuwa na hofu kwamba vyombo vya habari vinatoa hesabu tofauti.

Kila shirika linafanya hesabu zake kulingana na uwekaji wa data kutoka kwa vituo zaidi ya 46,000 vya kupigia kura.

Lakini ni tume ya uchaguzi pekee ndiyo inaweza kumtangaza mshindi.

Hesabu za vyombo vya habari zinaonyesha kuwa wagombeaji wawili wakuu - Raila Odinga na William Ruto – ‘wamekabana koo’ 

"Hatupaswi kuwa na hofu kuhusu tofauti tunazoziona kwenye skrini za vyombo vya habari. Matokeo yanatoka kwenye tovuti moja ya umma; mbinu [ya kila kituo cha utangazaji] ni tofauti," Bw Chebukati alisema.

Alisema mwisho wa kujumlisha matokeo yanapaswa kuonekana "sawa".

Kwa nini inachukua muda mrefu sana?

th

Chanzo cha picha, EPA

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Vikundi vya waandishi wa habari wanaofanya kazi katika vituo mbalimbali vinahusika na kazi ngumu ya kupakia takwimu zilizopokelewa kutoka kwa kila kituo cha kupigia kura moja baada ya nyingine. Kila chombo cha habari kinafanya hivyo kwa kasi tofauti na kuchagua vituo vya kupigia kura kwa mpangilio tofauti.

Linapokuja suala la tume ya uchaguzi, juu ya kuandaa matokeo, maafisa wanahitaji kuthibitisha kila moja - kazi nyingine inayochukua muda .

Maafisa kwa sasa wanalinganisha matokeo ambayo tume ilipokea kwa njia ya picha kutoka kwa vituo vya kupigia kura na karatasi halisi ya matokeo, ambayo inawasilishwa moja kwa moja kwenye kituo cha kujumlisha kura katika mji mkuu, Nairobi.

Hii ni kuhakikisha kuwa matokeo yote mawili yanalingana na sababu kuu kwa nini mambo yanachukua muda mrefu.

Kuhesabu kura katika baadhi ya vituo pia kulicheleweshwa na usafiri hadi Nairobi, haswa na mawakala kutoka maeneo ya mbali, kunaweza pia kuwa sababu za kupunguza kasi.

Wakenya wanajisikiaje?

Kuna hali ya wasiwasi nchini kwani chaguzi zilizozozaniwa huko nyuma zilisababisha ghasia au mchakato mzima kufutwa.

Kufuatia kura ya 2007, watu wasiopungua 1,200 waliuawa na 600,000 walikimbia makazi yao kufuatia madai ya kuibiwa kwa uchaguzi.

Mnamo 2017, hitilafu kubwa za vifaa zilisababisha Mahakama ya Juu kubatilisha matokeo na kuamuru uchaguzi wa urais urudiwe. Viongozi wanakabiliwa na shinikizo la kurekebisha mambo wakati huu.

Nchi mara nyingi inasimama wakati wa uchaguzi, shughuli kote nchini zimepungua na shule zinasalia kufungwa angalau hadi wiki ijayo Jumatatu. Katika wilaya ya kati ya biashara ya Nairobi, mitaa yenye shughuli nyingi mara nyingi haina watu.

Madai ya wizi wa kura ni ya zamani kama nchi. Ilikuwa ni sehemu ya siasa hata kabla ya chaguzi za vyama vingi kuanzishwa tena katika miaka ya 1990, lakini msukumo wa uchaguzi huru na wa haki haujawahi kulegalega.

Baada ya ghasia zilizofuatia uchaguzi wa 2007, vyama vya siasa na wanaharakati walibishania matumizi ya teknolojia badala ya rejista halisi, ambayo inaweza kubadilishwa kwa urahisi, ili kuhakiki wapiga kura.

Uchaguzi wa mwaka huu ni mara ya tatu kwa teknolojia kutumika lakini bado haujafanya uchaguzi ambao haujapingwa mahakamani.

Ripoti za mapema, hata hivyo, zinaonyesha kwamba tume ya uchaguzi huenda hatimaye ikafanikisha lengo hili lisilowezekana na uchaguzi huu.

Tutajua matokeo lini?

Maelezo ya video, Fahamu hatua kuanzia upigaji kura hadi kutangazwa kwa matokeo na tume ya IEBC

Kwa kasi ya kuhesabu kura inayoendelea, vyombo vya habari vya humu nchini huenda vikamaliza kujumlisha matokeo ya muda kabla ya mwisho wa siku Alhamisi.

Ikiwa kuna kiongozi wazi wa kinyang’anyiro sherehe zinaweza kuzuka.

Hata hivyo, ni tume ya uchaguzi pekee inayoweza kutangaza mshindi baada ya kulinganisha na kuthibitisha matokeo.

Kwa mujibu wa sheria, tume ya uchaguzi ina siku saba baada ya siku ya uchaguzi kutangaza matokeo.

Ili kushinda kinyang'anyiro cha urais katika awamu ya kwanza, mgombea anahitaji:

• zaidi ya nusu ya kura zote zilizopigwa kote nchini

• Takribani 25% ya kura zilizopigwa katika kaunti zisizopungua 24.

Vinginevyo upigaji kura unakwenda kwa duru ya pili ambayo kwa mujibu wa sheria inapaswa kufanyika ifikapo tarehe 8 Septemba.