WAFCON 2024: Tanzania yaanza mguu wa kushoto, kocha alia na Luvanga

s

Chanzo cha picha, Twiga stars

    • Author, Ian Williams
    • Nafasi, BBC Sport Africa, Berkane Stadium
  • Muda wa kusoma: Dakika 3

Goli la Saratou Traore katika dakika za lala salama za kipindi cha kwanza lilitosha kuwapa Mali ushindi mwembamba dhidi ya Tanzania (Twiga stars) katika mchezo wa Kundi C, timu hizo zikicheza mchezo wao wa kwanza kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) 2024.

Ulikuwa mchezo wa tofauti kwa kila timu, Mali waliweza kutumia kasi na nguvu dhidi ya Twiga Stars waliocheza kwa mtindo wa pasi na taratibu wakijaribu kutafuta nafasi kwa subira. Hata hivyo, Tanzania walikosa makali ya kutumia vyema na kumalizia mashambulizi yao.

Mchezo huo ulichezwa katika uwanja wa Berkane mbele ya mashabiki wachache sana na na kwa ujumla haukuwa wa kusisimua sana.

Goli pekee la mchezo huo lilifungwa katika dakika ya kwanza ya muda wa nyongeza kipindi cha kwanza, kupitia kwa kiungo Saratou Traore aliyefunga kwa shuti la chini kutoka ndani ya eneo la hatari baada ya walinzi wa Tanzania kushindwa kuokoa mpira wa adhabu kwneye eneo lao.

Mali, maarufu kama Female Eagles, walipata nafasi nyingi nzuri za kufunga. Aissata Traore, ambaye alimaliza mechi akiwa amefungwa bandeji kichwani, peke yake alipoteza nafasi zaidi ya moja za wazi.

Kwa ushindi huo, Mali wameungana na mabingwa watetezi Afrika Kusini kileleni mwa Kundi C wakiwa na alama tatu, baada ya Afrika Kusini kuibamiza Ghana 2-0 usiku wa leo.

Tanzania, ambao sasa wamepoteza mechi zao zote nne walizocheza katika fainali za WAFCON, zikiwemo fainali zilizopita, karibu miaka 15, watakuwa na nafasi ya kurekebisha rekodi yao watakapokutana na Afrika Kusini huko Oujda Ijumaa hii, huku Mali wakisalia Berkane kuwasubiri Ghana mapema siku hiyo hiyo.

Kukosekana kwa nyota wake kwailiza Tanzania

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Clara Luvanga (kulia) anacheza na kikosi cha wanawake cha Al-Nassr akiwa na Christiano Ronaldo, ambaye anacheza kikosi cha wanaume cha Al-Nassr huko Riyadh Saudi Arabia

Tanzania "Twiga stars, iliyorejea katika fainali hizi baada ya miaka 15, ilitarajia kuwa na wachezaji wake nyota wa kimataifa, Clara Luvanga, Opah Clement na Aisha Masaka katika mchezo wa ufunguzi.

Japo walipambana kwa uwezo wao, lakini pengo la kuwakosa nyota hawa lilionekana. Aisha Masaka, mshambuliaji wa Brighton & Hove Albion na Clara Luvanga wa Al-Nassr wao ni majeruhi, wakati Opah, anayekipiga nchini Mexico, anakadi za njano kama ilivyo kwa mlinzi Christer Bahera mwenye kadi ya njano pia.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mara baada ya mchezo huo, kocha wa Twiga Stars, Bakari Shime alikiri kwamba kukosekana kwa nyota hao ilikuwa "tatizo kubwa".

Wakati Tanzania walipokuwa wakishambulia, kiungo mdogo na mwenye kipaji Diana Msewa alionekana kuwa katika kiwango kizuri, hasa katika dakika za mwanzo za mchezo.

Lakini kadri jua lilivyozama na anga la Berkane kuwa jekundu, Mali walianza kutawala mchezo.

Saratou Traore celebrates scoring against Tanzania with her Mali team-mates

Chanzo cha picha, BackPage Pix

Maelezo ya picha, Mali walimaliza nafasi ya nne Wafcon 2018 lakini ilishindwa kufuzu Wafcon iliyofuata ya 2022
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Saratou Traore alianza kwa kujaribu shuti lake la kwanza nje ya lango, kabla ya Aissata Traore kuchelewa kutoa pasi na kupoteza nafasi.

Fatoumata Diarra alipiga shuti la mbali lililookolewa na kipa wa Tanzania, Najiati Idrisa, na mpira ulimkuta Kadidiatou Diabate ambaye alishindwa kuutia kimiani.

Dakika za lala salama kipindi cha kwanza, Saratou Traore aliweza kuwanyanyua mashabiki wachache uwanjani baada ya mpira wa kona kugombewa na kudondokea mbele yake, alifunga kwa utulivu kwa shuti lililokwenda moja kwa moja wavuni.

Tanzania walipata nafasi yao bora zaidi katika dakika za nyongeza za kipindi cha pili, lakini shuti la Elizabeth Chenge liliokolewa kwa ujasiri na beki Aicha Samake wa Mali.

Kwa Mali ushindi huo unia rekodi yao ya kwanza ya kutofungwa katika mchezo wowote wa WAFCON, wakishinda mchezo wao wa kwanza wa ufunguzi kwa mara ya kwanza kabisa.

Tanzania, wawakilishi kutoka Afrika Mashariki sambamba na DRC , pamoja na soka lao zuri, watahitaji kuongeza makali ya mashambulizi yao endapo wanataka kuendelea kubaki Morocco.