WAFCON 2024: Je, Tanzania itaishangaza dunia huko Morocco?

Chanzo cha picha, MWANANCHI
Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (Wafcon) 2024 inaanza wikiendi hii, na Morocco ni mwenyeji wa michuano hii kwa mara ya pili mfululizo.
Baada ya kurudishwa nyuma mwaka mmoja kwa sababu ya maswala ya ratiba, michuano itaanza Jumamosi, Julai 5 wakati wenyeji watakapomenyana na Zambia kwenye Uwanja wa Olimpiki huko Rabat.
Mabingwa mara tisa Nigeria pia wapo uwanjani wikendi ya ufunguzi, wakimenyana na Tunisia katika Kundi B, huku mabingwa Afrika Kusini wakianza kutetea ubingwa wao dhidi ya Ghana katika Kundi C Jumatatu, 7 Julai.
Kati ya mataifa 12 yanayoshiriki Morocco, ni Nigeria na Afrika Kusini pekee ambazo zimewahi kunyanyua kombe la Wafcon. Zambia ilimaliza ya tatu katika mashindano yaliyopita.
Kundi la Tanzania
Kundi C, ambalo Tanzania yupo, kuna timu ya Afrika Kusini, Ghana na Mali. Timu tatu ambazo zimepangwa na Twiga Stars, zipo katika 10 kwenye orodha ya viwango vya ubora wa soka kwa wanawake barani Afrika kwa mujibu shirikisho la mpira wa miguu duniani (Fifa), iliyotolewa Agosti 2024.
Katika orodha hiyo, Afrika Kusini ipo nafasi ya pili, Ghana ikiwa nafasi ya tano na Mali inashika nafasi ya tisa. Na Twiga Stars ipo nafasi ya 27 katika viwango vya ubora kwa soka la wanawake Afrika.
Timu ya taifa ya wanawake ya Afrika Kusini 'Banyana Banyana' ndio mabingwa watetezi wa Wafcon na kabla ya fainali zilizopita, walishika nafasi ya pili katika fainali za 2018.
Banyana Banyana imeshiriki mara mbili fainali za Kombe la Dunia kwa wanawake na mara ya mwisho ilikuwa ni 2023 ilipoishia hatua ya 16 bora.
Timu ya taifa ya wanawake ya Ghana 'Black Queens' imeshiriki mara tatu fainali za kombe la dunia kwa wanawake na zote iliishia hatua ya makundi.
Black Queens imeshiriki mara 12 katika fainali za Wafcon ambapo mafanikio yao makubwa ni kumaliza katika nafasi ya pili mwaka 1998, 2002 na 2006, huku ikiishia katika nafasi ya tatu mara tatu; 2000, 2004 na 2016.
Mali 'Majike ya Tai' haijawahi kushiriki fainali za Kombe la Dunia lakini imecheza Wafcon mara saba na mafanikio yao makubwa yalikuwa ni kumaliza katika nafasi ya nne katika fainali za 2018.
Ikumbukwe hii ni mara ya pili kwa Twiga Stars kushiriki Wafcon ambapo ya kwanza ilikuwa ni 2010 Afrika Kusini, ilimaliza katika hatua ya makundi, ikiwa na pointi moja iliyoipata katika mechi tatu.
Kwenye kundi A lilikuwa na wenyeji Afrika Kusini, Nigeria na Mali ambapo Twiga stars iliruhusu magoli 8 huku ikifunga magoli 3 tu.
Tanzania ina nafasi gani?

Chanzo cha picha, MWANANCHI
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Timu ya taifa ya wanawake ya Tanzania (Twiga Stars) ilifanikiwa kufuzu WAFCON, baada ya ushindi wa jumla wa goli 3-2 dhidi ya timu ya taifa ya wanawake ya Togo, mwezi Disemba 2023.
Licha ya kupoteza mchezo wa mkondo wa pili kwa goli 2-0 mbele ya wenyeji Togo, Twiga stars ilifuzu baada ya ushindi mnono wa goli 3-0 waliopata nyumbani kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza jijini Dar es Salaam.
Tanzania na DRC Congo ndio nchi zinazoshiriki kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki. Zaid ya miaka 10 imepita tangu Tanzania kushiriki kwa mara ya kwanza katika michuono hii. Na hii itakuwa mara ya pili.
Kuna dazeni ya wachezaji wa Twiger Stars wanaocheza soka la kulipwa nje ya Tanzania, katika nchi za Asia, Afrika Kaskazini, America Kusini na Ulaya ambao wameitwa katika kikosi cha timu ya taifa ya wanawake.
Miongoni mwa mafanikio ya hivi karibuni ya timua ya Tanzania, ni kutwa ubingwa wa mashindano ya Wanawake ya Baraza la vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), baada ya kuichapa Kenya bao 1-0 katika mechi ya mwisho iliyochezwa jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi, Twiga Stars ilitwaa ubingwa huo huku ikiandika rekodi ya kutoruhusu bao lolote na ikifumania nyavu mara 13 katika mechi nne.
Mashindano hayo yalizishirika nchi za Kenya, Uganda, Burundi na Sudan Kusini. Mashindano ya sasa ya WAFCON yatazishirika nchi nyingi zaidi na zenye uwezo mkubwa zaidi. Nafasi ya Tanzania itaaluliwa na jinsi watakavyo pachika magoli au watakavyo ruhusu magoli.
Makundi ya WAFCON
Timu 12 zimegawanywa katika makundi matatu ya timu nne.
Wenyeji Morocco wana kibarua kigumu katika Kundi A, baada ya kupangwa na timu ya Zambia ambayo iliwafunga katika michuano ya kufuzu Michezo ya Olimpiki ya 2024. Pia kundi hilo lina Senegal na DR Congo.
Nigeria wanawania taji lao la kwanza tangu 2018 na ni timu bora zaid zaidi barani Afrika ikiwa katika nafasi ya 36 duniani. Itamenyana na Tunisia, Algeria na Botswana.
Kundi C linawakutanisha mabingwa Afrika Kusini na Ghana na Mali, ambao wamerejea katika fainali kwa mara ya kwanza tangu 2018, na Tanzania, ambao wanashiriki mara ya pili kufuatia kucheza kwa mara ya kwanza mwaka 2010.
Kundi A: Morocco, Zambia, Senegal, DR Congo.
Kundi B: Nigeria, Tunisia, Algeria, Botswana.
Kundi C: Afrika Kusini, Ghana, Mali, Tanzania.















