Twiga Stars yarejea WAFCON baada ya miaka 13 na kibarua cha kuvuka hatua ya makundi

.

Chanzo cha picha, TFF

Maelezo ya picha, Licha ya kupoteza mchezo wa mkondo wa pili kwa goli 2-0 mbele ya wenyeji Togo, Twiga stars imefuzu baada ya ushindi mnono wa goli 3-0 waliopata nyumbani kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza jijini Dar es Salaam.

Timu ya taifa ya wanawake ya Tanzania (Twiga Stars) imefanikiwa kufuzu kwa fainali za mataifa ya Afrika, WAFCON zinazotarajiwa kufanyika huko Morocco mapema mwaka 2024 baada ya ushindi wa jumla wa goli 3-2 dhidi ya timu ya taifa ya wanawake ya Togo.

Licha ya kupoteza mchezo wa mkondo wa pili kwa goli 2-0 mbele ya wenyeji Togo, Twiga stars imefuzu baada ya ushindi mnono wa goli 3-0 waliopata nyumbani kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza jijini Dar es Salaam.

Magoli mawili ya Opah Clement na moja la kujifunga la Togo yalitosha kuivusha Twiga stars na kuwa tena timu ya pekee kutoka ukanda wa Afrika mashariki na kati chini ya mwavuli wa vyama vya soka vya kanda hiyo, CECAFA kufuzu kwa mara ya pili kwenye michuano hiyo mikubwa zaidi barani Afrika katika soka la wanawake.

Kufuzu WAFCON si mafanikio pekee ya Twiga stars mwaka huu kufika hatua ya pili ya mtoano wa kutafuta timu zitakazoshiriki WAFCON imewapa nafasi pia ya kufuzu kwenye michuano ya Omlipiki itakayofanyika Ufaransa mwakani 2024.

Kwa ukanda wa Afrika mashariki ni Tanzania pekee imepata nafasi ya kushiriki kwenye fainali hizo ambazo zilianza rasmi mwaka 1991. Uganda na Kenya zimewahi kufuzu hapo awali mara moja kila nchi, Uganda ikishiriki kwenye fainali 2000 na kuishia hatua ya makundi. Kenya ilipata nafasi hiyo mwaka 2016 kwenye fainai zilizofanyika Cameroon wakiwa kundi B na kumaliza nafasi ya mwisho baada ya kushinwa kukusanya hata alama moja.

Twiga stars iliwahi kufanya mwaka 2010 WAFCON ilipofanyika Afrika kusini ambapo waliishia hatua ya makundi.

Kocha msaidizi wa sasa wa Twiga stars Ester Chabruma ndiye alikuwa mchezaji bora kwenye kikosi cha 2010 akiwa chini ya nahodha Sofia Mwasikili ambao wote kwa pamoja walifunga bao moja moja kwenye mashindano hayo sambamba na Fatma Swalehe.

Kabla ya kukutana na Togo, Twiga Stars iliwafurusha wababe Ivory Coast kwa changamoto ya mikwaju ya penati baada ya sare ya 2-2 kwenye matokeo ya jumla nyumbani na ugenini, magoli ya Donisia Minja na Opah Clement katika kipindi cha pili cha mchezo wa marudia yalitosha kuipeleka Twiga Stars hatua ya pili.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Miaka 13 baadaye wanafuzu licha ya ligi kuu ya wanawake kuanza kuchezwa nchini Tanzania miaka kadhaa iliyopita. Lakini pia kuna wachezaji wa Twiga Stars wanaotoka kwenye klabu za nje ya nchi kama Opah Clement anayecheza Besiktasi ya Uturuki. Yupo pia mwanamke wa kwanza mtanzania kucheza ligi ya mabingwa Ulaya, Aisha Masaka anayechezea klabu ya BK Häcken bila kumsahau Enekia Kasonga anayekipiga Eastern Flames ya Saudi Arabia.

Uwepo wa wachezaji wanaocheza kwenye ligi zenye ushidani mkubwa kote duniani kumesaidia kiasi kikubwa mafaniko haya ya Twiga Stars ambayo yalikuwa yakisubiriwa kwa maika 13. Pia ushindani mkubwa wa ligi ya wanawake nchini Tanzania umechangia kuazalisha vipaji vingi vilivyosaidia kuiinua Twiga Stars.

Timu za vilabu vya Tanzania zimeweza kuleta ushindani mkubwa kwa vilabu vingine kwenye ukanda wa Afrika Mashabriki kwa kuwa timu pekee kutoka ukanda huu kushiriki fainali za Klabu bingwa Afrika kwa wanawake tangu ilipoanzishwa mwaka 2021 sasa tuliwaona Simba Queens mwaka 2021/2022 kisha JKT Queens mwaka huu wakicheza hatua ya makundi ya mashindano hayo.

Miaka 13 iliyopita hata ligi ya wanawake ilikuwa haichezwi nchini Tanzania, hali iliyochangia timu ya taifa iliyofuzu wakati huo kutokushinda hata mchezo mmoja kwenye kundi A ambalo lilikuwa na wenyeji Afrika Kusini, Nigeria na Mali ambapo Twiga stars iliruhusu magoli 8 huku ikifunga magoli 3 tu na haikupata hata alama moja.

Pengine mazingira ya sasa ya upatikana ji wa wachezaji na pia ushindani wanaopata ndani na nje ya Tanzania katika ligi Kuu na mashindano mengine kunaiongezea Twiga Stars uwezekano wa kufanya vema Zaidi katika WAFCON ya 2024 hujo Morocco kuliko ilivyokuwa mwaka 2010 huko Afrika Kusini.

Wababe wa michuano hiyo, Nigeria pia wamefuzu kwa mara nyingine wakinyemelea kutwaa ubingwa wa 12 wa fainali hizo pamoja na Morocco ambao ni wenyeji wa michuano hiyo mabingwa wa mwaka uliopita Afrika kusini wanatazamiwa kuwa timu tishio Zaidi.

Timu zingine zilizofuzu ni pamoja na Algeria, Ghana, Botswana, Jamhuri ya kidemokrasi Kongo, Tunisia, Senegal, Zambia na Mali.

Pengine michuano hii itakuwa ya kwanza kwa timu za ukanda wa Afrika mashariki kufika hatua za juu zaidi kwenye mashindano hayo.

Lakini kufikia hatua hiyo ya kufuzun kwa hatua ya mtoano bila shaka itawapasa Twiga Stars kupambana vilivyo ili kuzipiga vikumbo timu za nchi zenye uzoefu mkubwa na ambazo zimewahi kufaidi utamu wa mafanikio kama vile Nigeria, Afrika Kusini na Ghana. Na kwa hakika wakati wa matayarisho ni sasa ili kudhihirisha azma hiyo.

Imeandikwa na Bosha Nyanje

Imehaririwa na Florian Kaijage