WAFCON 2024: Tanzania 'kuibomoa' Mali leo?

Chanzo cha picha, Getty Images
Berkane ni mji ulioko kaskazini-mashariki mwa Morocco, umepakana na Bahari ya Mediterania upande wa kaskazini, Mto Kis na Mkoa wa Oujda upande wa mashariki, mkoa wa Nador upande wa magharibi, na Mkoa wa Taourirt upande wa kusini.
Leo Twiga Stars ya Tanzania itashuka dimbani kupambana NA Mali katika uwanja wa Manispaa ya Berkane. Ndio mchezo wa kwanza kwa timu zote mbili katika michuano ya 13 ya CAF ya Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON). Hapo jana ndugu zao, DRC walichapwa 4-0 na Senegal, Nigeria ikianza vyema mashindano hayo kwa kuilaza Tunia 3-0.
Ni michuano ya wiki tatu nchini Morocco yaliyoanza Julai 5, 2025. Nchi 12 zinashindana katika makundi matatu ya timu nne. Afrika Mashariki inawakilishwa na Tanzania na DR Congo.
Mali kutoka Magharibi mwa Afrika na Tanzania ziko katika Kundi C – ni kundi linalojumuisha pia mabingwa watetezi Afrika Kusini ama Banyana Banyana na Ghana pia kutoka Afrika Magharibi.
Mechi ya pili ya Tanzania itachezwa Alhamisi, 11 Julai, dhidi ya Afrika Kusini kwenye Uwanja wa Honor mjini Oujda. Twiga Stars itahitimisha safari yake ya hatua ya makundi Jumapili, Julai 14, dhidi ya Ghana, kwa mara nyingine tena kwenye Uwanja wa Berkane.
Uwezo wa Mali

Chanzo cha picha, CAF
Mali ilifuzu Kombe la Mataifa ya Afrika Wanawake kwa kuonyesha ubabe katika muda wote wa michezo ya mchujo. Katika raundi ya kwanza, ilimenyana na Jamhuri ya Afrika ya Kati. Mechi ya kwanza, ilichezwa mjini Douala Septemba 22, 2023, ilimalizika kwa ushindi wa 7-1.
Katika mechi ya marudiano mjini Bamako, wenyeji Mali walimaliza kwa kushinda 3-1, na kufikisha jumla ya mabao 10-2.
Katika raundi ya pili, walimenyana na Guinea, tarehe 29 Novemba mjini Bamako, walipata ushindi wa 7-2, na kukamilisha kufuzu mjini Conakry Desemba 5 kwa ushindi wa 3-0. Katika raundi zote mbili, Mali ilifunga mabao 20 na kuruhusu 3 pekee.
Hii ni mara ya 8 kwa Mali kushiriki kombe la Afrika kwa wanawake. Matokeo yao bora zaidi kufikia sasa ni kumaliza nafasi ya 4 mwaka 2018 nchini Ghana, baada ya kufungwa 4-2 na Cameroon katika mechi ya mshindi wa tatu.
Miongoni mwa nyota wao tegemezi katika ufungaji ni Agueissa Diarra. Amekuzwa katika klabu ya FC Super Lionnes mjini Bamako. Mshambuliaji huyu alijiunga na Paris Saint-Germain mwaka 2023, ambako anacheza na nyota wengine wa kimataifa.
Mchezaji mwingine tegemezi ni kiungo Aïssata Traoré mwenye umri wa miaka 28. Kwa sasa anaichezea FC Fleury 91 inayoshiriki ligi daraja la juu nchini Ufaransa, anajulikana kwa ubora wake wa kupiga pasi na uwezo wa kudhibiti mchezo.
Uwezo wa Tanzania

Chanzo cha picha, Mwananchi
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mali na Tanzania zinakutana katika hatua ya makundi ya michuano ya WAFCON kwa mara ya pili; mara yao ya mwisho ni katika mashindano ya 2010, na Mali ilishinda 3-2.
Wakati Mali wanashiriki kwa mara ya nane, Tanzania ni mara yao pili – mara ya kwanza ikiwa ni 2010 katika michuano iliyofanyika nchini Afrika Kusini.
Kwa mujibu wa mtandao wa michezo wa Sportskeeda, katika michezo tisa rasmi ya hivi karibuni, Tanzania imeshinda michezo saba, huku ikitoka sare mchezo mmoja na kufungwa mchezo mmoja.
Wakati Mali imeshinda michezo minne kati ya saba, lakini imeshindwa kupata ushindi katika michezo mitatu.
Tathmini ya CAF katika kundi C inasema, “Tanzania, ambayo mara nyingi hupuuzwa, imeonyesha maendeleo ya wazi katika miaka ya hivi karibuni kutokana na maendeleo ya wachezaji wake vijana na matokeo mazuri katika ukanda wa CECAFA.”
Hivi karibuni timua ya Tanzania, imetwaa ubingwa wa mashindano ya Wanawake ya Baraza la vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) mwezi Juni 2025, baada ya kuichapa Kenya bao 1-0 katika mechi ya mwisho iliyochezwa jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi, Twiga Stars ilitwaa ubingwa huo huku ikiandika rekodi ya kutoruhusu bao lolote na ikifumania nyavu mara 13 katika mechi nne. Ni mashindano yaliyozishirika nchi ya Kenya, Uganda, Burundi na Sudan Kusini.












