Hazina iliyojificha yagunduliwa ndani ya miili yetu — je ina manufaa gani?

..

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 3

Wanasayansi wanasema kuwa sehemu mpya ya kinga imegunduliwa na ni "hazina ya dhahabu" kwa ajili ya antibiotiki za baadaye.

Wamegundua kwamba sehemu ya mwili inayoshughulikia protini pia hutengeneza kemikali inayoua bakteria.

Kulingana na watafiti wa Kiyahudi, ugunduzi huu utabadilisha kimsingi ufahamu wetu kuhusu kinga ya mwili.

Pia utasaidia kutafuta antibiotiki mpya za kutatua tatizo la vijidudu sugu ambavyo havidhuriki kwa dawa za sikuhizi.

Sehemu muhimu ya ugunduzi huu ni proteasome, muundo mdogo unaopatikana katika kila seli ya mwili.

Kazi kuu ya proteasome ni kubomoa protini za zamani, kisha protini mpya hutengenezwa kutokana na hizo.

Hata hivyo, kulingana na mfululizo wa majaribio yaliyotajwa katika jarida la "Nature", proteasome inaanza kufanya kazi tofauti wakati seli inashambuliwa na bakteria.

Inabadilisha kazi yake - inaanza kubadilisha protini za zamani kuwa silaha zinazoshambulia bakteria.

..

Chanzo cha picha, Weizmann Institute of Science

"Tulikuwa hatujui kuhusu tukio kama hili awali," anasema Yifat Merbl, profesa katika Taasisi ya Sayansi ya Weizmann.

"Tuligundua mchakato mpya wa kinga unaotoa ulinzi dhidi ya maambukizi ya bakteria.

Hii hutokea katika kila seli ya mwili wetu na ina uwezo wa kuunda aina mpya kabisa ya antibiotiki za asili."

Watafiti walifanya mchakato uitwao "dumpster diving" ili kugundua antibiotiki hizi za asili.

Zilifanyiwa majaribio kwa bakteria waliokuzwa maabara na panya wenye homa ya mapafu na maambukizi katika damu sepsis.

Kwa mujibu wa watafiti, matokeo yalikuwa sawa na baadhi ya antibiotiki zilizopo sasa.

..

Chanzo cha picha, Weizmann Institute of Science

Maelezo ya picha, Taasisi ya Utafiti ya Weizmann Profesa Yifat Merble na timu yake
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Profesa Daniel Davie,mtaalamu wa sayansi za kibiolojia katika Chuo Kikuu cha Imperial na mtaalamu wa kinga, alisema kwamba ugunduzi huu ni "muhimu sana na wa kusisimua" kwa sababu unaimarisha uelewa wetu kuhusu jinsi mwili unavyozuia maambukizi.

"Kile kinachovutia kuhusu hili ni kwamba ni mchakato ambao haukujulikana awali wa kutengeneza molekuli za kuua bakteria ndani ya seli zetu."

Kwa mujibu wake, kubadilisha mchakato huu kuwa chanzo kipya cha antibiotiki "bado kinahitaji majaribio mengi."

Inakadiriwa kwamba zaidi ya watu milioni moja hufariki kila mwaka kutokana na maambukizi yanayoshindwa kutibika na antibiotiki.

Hata hivyo, licha ya uhitaji mkubwa, hakukuwa na utafiti wa kutosha kuhusu maendeleo ya antibiotiki mpya zinazokidhi mahitaji.

Katika hali hii, kuibuka kwa fursa mpya inakuwa chanzo cha matumaini kwa baadhi ya wanasayansi.

Dkt. Lindsey Edwards, mhadhiri mkuu wa microbiolojia katika King's College London, aliambia BBC: "Hii ni hazina inayoweza kuwa ya antibiotiki mpya, jambo linalosisimua sana.

Hapo awali, ilikuwa lazima kuchimba udongo ili kugundua antibiotiki mpya. Sasa hatutarajii kuziona ndani ya miili yetu."

Wanasayansi wanasema kuna uwezekano wa kuwa na changamoto kidogo katika kuzibadili kuwa dawa, kwa sababu tayari ni bidhaa ya mwili wa binadamu, hivyo "swala la usalama linaweza kutatuliwa kwa urahisi zaidi."

Imetafsiriwa na Martha Saranga