Kwa nini Trump anafuta misaada Afrika Kusini kwa kigezo cha muswada wa ardhi?

Muda wa kusoma: Dakika 6

Rais Trump ametia saini amri ya kusitisha rasmi misaada yote kwa Afrika Kusini, akidai sheria mpya ya ardhi ya nchi hiyo inakiuka haki za binadamu za watu weupe walio wachache nchini humo.

Bw Trump anasema Sheria mpya ya kutwaa ardhi nchini humo inawezesha mashamba yanayomilikiwa na wazungu wachache kutwaliwa bila kulipwa fidia.

Amelitaka baraza lake la mawaziri kuja na mpango wa kuwapatia makazi Waafrikana ambao anadai, "ni waathiriwa wa ubaguzi wa rangi usio wa haki".

Waafrikana ni kabila ambalo lilitokana na wakoloni Wazungu - hasa Waholanzi.

"Afrika Kusini inatwaa ardhi, na inawatendea watu wa tabaka fulani VIBAYA SANA," Rais Trump aliandika kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii.

Mshauri wake wa karibu Elon Musk, ambaye alizaliwa Afrika Kusini, pia aliunga mkono ukosoaji huo - akihoji kupitia jukwaa la mtandao wa kijamii X kwa nini Rais Cyril Ramaphosa alitumia "sheria za ubaguzi wa rangi katika umiliki".

Kwa nini ardhi ni suala muhimu Afrika Kusini?

Zaidi ya miaka thelathini baada ya kumalizika kwa ubaguzi wa rangi, umiliki wa ardhi nchini Afrika Kusini unasalia kuwa suala nyeti sana.

Marekebisho ya ardhi yamekuwa muhimu katika ajenda ya mabadiliko nchini humo tangu kuanzishwa kwa demokrasia mwaka 1994.

Sheria mpya ya kutwaa ardhi iliyopitishwa inatumika kama ukumbusho wa jinsi ardhi ilivyochukuliwa kwa nguvu kutoka kwa watu weusi walio wengi na serikali ya zamani iliyokuwa na ubaguzi wa rangi.

Chini ya Sheria ya Ardhi ya 1913, umiliki wa ardhi kwa watu weusi ulikuwa mdogo hadi 7%. Hii baadaye ilirekebishwa hadi 13% chini ya Sheria ya Native Trust na Ardhi ya 1936 nchini Afrika Kusini.

Sheria hizi zilifungua milango kwa watu weupe kumiliki karibu 90% ya ardhi, huku wengi weusi wakigombania kile kilichosalia.

Matokeo yake, watu weusi walihamishiwa kwenye makazi yenye watu wengi ambako miji midogo iliyopangwa vibaya ilijengwa.

Kama ukumbusho wa dhuluma zilizopita, wiki hii Afrika Kusini iliadhimisha kumbukumbu ya miaka 70 tangu utawala wa kibaguzi kuwaondoa kwa nguvu watu weusi 65,000 kutoka makwao ili kupisha nafasi kwa kitongoji cha wazungu pekee.

Sheria mpya inasemaje?

Sheria mpya inalenga hasa kurekebisha kukosekana kwa usawa wa kihistoria huku ikihamasisha ukuzaji uchumi.

Inaruhusu serikali kutwaa ardhi kwa manufaa ya umma kama vile maendeleo ya miundombinu, ikiwa ni pamoja na kujenga barabara na nyumba, huku ikihakikisha kwamba wamiliki wanalipwa fidia na kutendewa haki.

Sheria hiyo mpya inachukua nafasi ya Sheria ya kutwaa ardhi ya kabla ya utawala wa kidemokrasia 1975, ambayo iliwajibisha serikali kwa kuwalipa wamiliki wa ardhi iliyotwaa, chini ya kanuni ya "uuzaji na ununuzi wa ardhi kwa hiari".

Badala yake, sheria hii inahitaji fidia ya haki kwa ardhi iliyotwaliwa, isipokuwa katika hali maalum ambapo inachukuliwa kuwa "ya haki na inafaa kwa maslahi ya umma" kutoitoa.

Hii inajumuisha ikiwa mali haitumiki na hakuna mpango wa kuiendeleza au kupata faida kwayo, au ikiwa inahatarisha usalama wa watu.

Katika hali hizi, sheria inasema kuwa hakuna kutaifisha bila mchakato wa haki na uangalizi.

Unaweza pia kusoma

Nani anamiliki ardhi ya Afrika Kusini?

Ingawa ubaguzi wa rangi ulimalizika zaidi ya miaka thelathini iliyopita, watu weupe bado wanadhibiti sehemu kubwa ya ardhi inayotumika kwa kilimo nchini humo.

Takwimu za sasa zinaonyesha kuwa watu weupe wanamiliki robo tatu ya ardhi inayomilikiwa kibinafsi, wakati watu wa rangi hiyo wanaunda chini ya 10% ya idadi ya watu kwa jumla.

Nchi inamiliki takriban asilimia 14 ya ardhi.

Kwa nini Trump amekasirishwa na sheria mpya?

Ingawa sheria mpya iko wazi kwamba ardhi inaweza kuchukuliwa pasipo fidia katika hali au mazingira fulani, kuna imani miongoni mwa jamii ya watu weupe wa Afrika Kusini kwamba imetoa nafasi kwa serikali kuchukua mali za binafsi za makazi.

Wale wanaopinga sheria hii wanalinganisha na sera za ugawaji ardhi nchini Zimbabwe ambapo maelfu ya wakulima weupe walilazimishwa kutoka kwenye ardhi zao, mara nyingi kwa ghasia, kati ya mwaka 2000 na 2001.

Uchukuaji huo ulikuwa na lengo la kurekebisha yaliyofanyika kipindi cha ukoloni lakini ulileta mchango mkubwa katika kushuka kwa uchumi wa nchi hiyo.

Madai dhidi ya sheria mpya ya Afrika Kusini yanatolewa na kundi la watetezi wa haki za kiraia la AfriForum, ambalo linazingatia hasa maslahi ya Waafrikana.

Kundi hili lililazimisha msaada wa kimataifa kabla na baada ya Sheria ya Utwaaji ardhi (Expropriation Act) kutiwa sahihi mwezi uliopita.

Watetezi hao wanadai kuwa sheria mpya haitahakikisha ulinzi wa haki ya umiliki ardhi.

Lakini ANC imeshutumu AfriForum kwa upotoshaji wa taarifa na kusambaza hofu. Badala yake, Rais Cyril Ramaphosa amelinganisha sheria mpya na sheria zinazofanana nchini Marekani.

"Kama vile Marekani na nchi nyingine, Afrika Kusini daima imekuwa na sheria za utekelezaji zinazolingana mahitaji ya matumizi ya umma ya ardhi na ulinzi wa wamiliki mali," alisema.

Katika mabadiliko ya kushangaza, rais wa Marekani Trump ametoa hadhi ya wakimbizi kwa wakulima weupe wa Afrika Kusini "wanaokimbia ubaguzi wa rangi unaofanywa na serikali."

Hali halisi ni kwamba wengi wa Waafrikana wanajivunia na wanaendelea vizuri nchini Afrika Kusini. Wengi wameelekea kwenye mitandao ya kijamii kukataa mwaliko wa Trump wa kuhamia Marekani.

Shirika la Waafrikana la Orania Movement limesema wanachama wake hawana azma ya kuondoka nyumbani mwao na hawatafuti kuwa wakimbizi katika nchi nyingine.

Orania ni mji mdogo katika eneo la Karoo ambao ulianzishwa ili kuhifadhi utamaduni wa Waafrikana na una sarafu yake yenyewe.

Je, Afrika Kusini inapata msaada kiasi gani wa kifedha kutoka Marekani?

Amri ya Rais Trump imesitisha karibu dola milioni 440 za msaada wa kifedha kutoka Marekani kwa taifa la Afrika Kusini.

Hata hivyo, ubalozi wa Marekani nchini Afrika Kusini umethibitisha kwamba fedha za PEPFAR, ambazo zinaunda asilimia 17 ya programu ya HIV/AIDS kwa nchi hiyo, hazitakumbwa na athari.

Julius Malema amesema nini?

Julius Malema, kiongozi wa chama cha upinzani kinachodai mageuzi ya kiuchumi (Economic Freedom Fighters), amepinga kauli ya Trump kuhusu muswada mpya wa mageuzi ya ardhi, akisema kuwa ni shambulio dhidi ya uhuru wa nchi na dhihirisho la kiburi cha kikoloni.

Hii ilimfanya Elon Musk kuonyesha wimbo wa zamani wa Malema, ambao ulikuwa na maneno yenye utata, ikiwemo "Dubul'ibhunu – mpige risasi", ambao alielezea kama kuchochea ghasia.

Mnamo mwaka 2010, Malema alijikuta akifikishwa mahakamani kwa kuimba wimbo huo.

Wimbo huo ulitangazwa kama hotuba ya chuki, lakini hukumu hiyo ilibatilishwa baadaye na Mahakama kuu ya Johannesburg, ambayo ilisema kuwa wimbo huo si hotuba ya chuki wala uchochezi wa ghasia.