Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Msukosuko wa upinzani Afrika Kusini baada ya makamu wa Malema kujiuzulu
- Author, Farouk Chothia
- Nafasi, BBC News
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Chama cha upinzani cha Economic Freedom Fighters (EFF) nchini Afrika Kusini, ambacho kimekuwepo kwenye siasa kwa zaidi ya muongo mmoja, kimepata pigo kufuatia kujitoa kwa naibu kiongozi wake Floyd Shivambu na kujiunga na chama cha Rais wa zamani Jacob Zuma - Umhkonto weSizwe (MK) au Mkuki wa Taifa.
Shivambu alionekana kama gwiji wa itikadi za EFF, huku kiongozi wa chama Julius Malema akijivisha vazi la kamanda mkuu - au "mpiga kelele-mkuu," kama wakosoaji wake wanavyomwita kutokana na maneno yake makali ya kutaka kutaifishwa kwa ardhi zinazomilikiwa na wazungu na migodi, na kuondoa ukoloni katika elimu.
Wawili hao walionekana kuwa timu yenye ushawishi, kwani EFF ilipata uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa vijana wa Afrika Kusini, wanaokerwa na kasi ndogo ya mageuzi ya kisiasa na kiuchumi tangu kumalizika kwa mfumo wa ubaguzi wa rangi mwaka 1994.
Lakini EFF ilipata msukosuko mkubwa katika uchaguzi mkuu wa Mei - haikufikia lengo lake la kupanda kutoka nafasi ya tatu hadi ya pili – na badala yake imeshuka hadi nafasi ya nne.
MK imekuwa ndio adui wake wa kisiasa - kama ilivyo kwa chama tawala cha African National Congress (ANC), kimepata kura kutoka kwa vyama vyote viwili na kunyakua nafasi ya tatu katika uchaguzi wa kwanza kushiriki.
"MK imepata kura kutoka kwa wafuasi wa ANC na EFF. Ilibadilisha mkondo wa siasa za Afrika Kusini, na kuifanya ANC kupoteza wingi wake wa wabunge kwa mara ya kwanza tangu 1994," anasema William Gumede, mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Wits School of Governance huko Johannesburg.
Vijana wenye ushawishi
Kuondoka Shivambu ni pigo kwa Malema, kwa sababu wawili hao, wakiwa vijana wenye nguvu za kisiasa, walianzisha EFF kwa pamoja wakati ANC, ikiongozwa na Zuma - ilipowafukuza.
Walifukuzwa baada ya shutuma za kuleta migawanyiko na kukiingiza chama katika mitafaruku.
"EFF ilichukua karibu vijana wote wa ANC, na pia kutawala siasa za wanafunzi katika vyuo vikuu kote Afrika Kusini, huo ndio ulikuwa mvuto wa chama miongoni mwa vijana," anasena Paddy Harper, mwandishi wa habari wa gazeti la Afrika Kusini la Mail & Guardian.
"Malema alikuwa na mvuto wa kupata uungwaji mkono, na Shivambu alikuwa na akili kutoa mwelekeo wa kiitikadi."
"Kwa kuachana kwao, EFF itaingia katika kipindi kigumu. Na hilo litaonekana kote Afrika Kusini, kuanzia vyuo vikuu hadi bungeni, huku EFF ikijaribu kuzuia kupoteza wafuasi zaidi kwenda MK."
Mchambuzi wa masuala ya kisiasa Moeletsi Mbeki anasema, kutengana huko kutaimarisha nafasi ya Malema katika chama, kwani hatakabiliwa tena na tishio kwa mamlaka yake.
"EFF inachukuliwa kama ni dhehebu linaloendeshwa na Malema. Katika mfumo kama huo, kiongozi ndiye kiongozi.”
Mvutano wao
Ishara ya kwanza ya hadharani ya uhusiano wao kutumbukia kwenye matatizo, ilionekana mwaka jana, wakati Malema alipotoa sifa kubwa kwa Shivambu, akimtaja kama mtu mwenye akili, kabla ya kumuonya kutopanga njama dhidi yake.
"Sina huruma dhidi ya watu wanaonifanyia njama, kwa hivyo usijaribu kufanya hivyo dhidi yangu," Malema alinukuliwa akisema kwenye hafla ya chakula cha jioni.
Huku Malema akitarajiwa kugombea tena nafasi ya kiongozi wa chama katika kongamano la EFF mwezi Oktoba, kwa Shivambu, 41, ndio umekuwa wakati wa kuondoka.
MK imemfanya kuwa mratibu wake wa kitaifa – ni cheo cha ukilinganisha na cheo chake alipokuwa EFF, lakini bado ni wadhifa wa juu katika jukumu la kukuza chama.
Lakini Harper anasema, haijuulikani ikiwa ataelewana na Zuma, kutokana na mzozo wao wa hapo awali na ukweli kwamba, rais huyo wa zamani ndiye mkuu wa dhehebu la MK, mwenye sifa ya kuteua na kufukuza kazi mara kwa mara. Ndani ya kipindi kisichozidi mwaka mmoja chama hicho kimekuwa na makatibu wakuu watatu.
Tuhuma za Ufisadi
“Shivambu huenda alishawishiwa kuasi kwani yeye na Malema - licha ya kuwa wote ni wasoshalisti na wazalendo wa Kiafrika - kwa sasa wanakabiliwa na tuhuma kubwa ya ufisadi,” anasema Harper.
Wanatuhumiwa kupokea takribani rand milioni 16 (dola za kimarekani milioni 9), hongo kutoka kwa bosi wa benki ambayo sasa imefutwa, baada ya kukutana naye kwenye jumba la kifahari katika kitongoji cha Johannesburg mwaka 2017.
Tuhuma hizo zimekuja kupitia taarifa iliyovuja ya bosi wa zamani wa benki hiyo Tshifhiwa Matodzi, ambaye amekiri makosa 33 ya rushwa, wizi, utakatishaji fedha na ulaghai, katika kile wadadisi walichoeleza kuwa ni wizi wa benki.
Wote Shivambu na Malema wamekanusha makosa yoyote, lakini uchunguzi wa polisi unaendelea - na wapinzani wao wa kisiasa wataendeleza shinikizo na tuhuma hizo hazitakwisha hivi karibuni.
"Ni kashfa kubwa zaidi ya ufisadi kuikumba EFF, na ikiwa chama kitalazimika kumgeuza mtu yeyote kuwa mwanakondoo wa kafara, basi ingekuwa ni Shivambu - na si Malema," anasema Harper.
"Kwa hivyo, kuhamia kwake MK kunaleta maana kwani kunampa ulinzi zaidi. Ni chama kikubwa kilichojaa watu wanaotuhumiwa kwa ufisadi - akiwemo Zuma mwenyewe."
Rais huyo wa zamani amekana kufanya makosa yoyote.
Sera za Shivambu pia zinafanana na zile za MK, zote zikitetea utaifishwaji wa ardhi zinazomilikiwa na wazungu na umiliki wa serikali wa migodi na benki - sera ambazo zilipitishwa na mataifa mengi ya Afrika baada ya uhuru, lakini sera hiyo iliachwa baada ya kuanguka kwa Umoja wa Soviet zaidi ya miaka 20 iliyopita.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah