Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Julius Malema: Kwa nini mwanasiasa wa Afrika Kusini ameikasirisha serikali ya Kenya?
- Author, Joseph Warungu
- Nafasi, BBC Africa
Tarehe 9 Novemba, wanaume wawili walisimama mbele ya Wakenya kutoa hotuba zilizokuwa zikisubiriwa kwa muda mrefu, zikitenganishwa kwa saa chache na kilomita chache.
Wote wawili walikuwa mubashara kwenye televisheni na wote wawili ni wana majumui wa Kiafrika. Lakini kufanana kwao kuna kikomo.
Mwanamume mmoja, ni Rais William Ruto wa Kenya, alivalia suti rasmi ya bluu. Mwanaume mwingine, ni kiongozi wa upinzani wa Afrika Kusini Julius Malema, alikuwa amevalia suti nyeusi ya kaki kutoka juu hadi chini na kofia nyekundu kichwani.
Hotuba ya Rais wa Kenya ilitolewa huku kukiwa na shamrashamra na sherehe bungeni na ilipokelewa kwa huzuni na uchovu. Lakini kila sentensi katika hotuba ya Malema ilipokelewa kwa shangwe kutoka kwa wasikilizaji wake - wakati wa uzinduzi wa Taasisi ya Pan-African katika Chuo kikuu cha Kenya.
Tangu siku hiyo, hotuba zao zimekuwa kitovu cha ulinganishi na mjadala wa kusisimua nchini Kenya. Hotuba ya Malema ilipeperushwa tena kwenye chaneli kadhaa za mtandaoni za Kenya na video fupi zilisambazwa sana kwenye WhatsApp.
Uamuzi wa Malema kumshambulia Rais Ruto kuhusu masuala kadhaa, ikiwa ni pamoja na kushindwa kutimiza ahadi zake za uchaguzi, ulifurahisha Wakenya wengi.
Kinara huyo wa siasa za upinzani Afrika Kusini, pia alimkosoa Ruto kwa kutomshambulia Mfalme Charles wa Uingereza kuhusu ukoloni wakati wa ziara yake nchini Kenya hivi karibuni.
Mchambuzi wa vyombo vya habari Elvis Ndekwe anasema ili kuelewa kwa nini Wakenya walimuunga mkono kiongozi aliyevunja miiko ya Kiafrika - inayomtaka mgeni asimseme vibaya mwenyeji wake, inabidi urejee matukio ya Machi mwaka huu.
"Iikuwa ni siku ambayo raia wenye hasira katika nchi nne za Afrika waliingia mitaani katika maandamano ya wakati mmoja, kupiga vita gharama kubwa ya maisha. Maandamano hayo ya Afrika Kusini, Kenya, Nigeria na Tunisia yaliongozwa na viongozi wa upinzani, akiwemo Julius Malema."
Ndekwe anaongeza kuwa Kenya tayari ilikuwa na maandamano ya mara kwa mara yakiongozwa na kiongozi wa upinzani Raila Odinga, kupinga kile alichohisi ni wizi katika uchaguzi mkuu wa 2022.
"Wakenya wengi, hasa vijana, walimtambua Julius Malema ambaye alikuwa akipigania jambo linalofanana na lao. Waliona kama anaonyesha mshikamano dhidi ya tawala dhalimu au zisizo jali."
Wasikilizaji Walikuwa Wakimsubiri
Profesa PLO Lumumba, mwenyekiti wa Taasisi mpya ya Pan-African iliyomwalika Malema Kenya, anaunga mkono hoja ya Ndekwe.
"Malema anawakilisha kizazi kipya cha Waafrika ambao wanaanza kueleza masuala yao kwa njia ambayo inavutia watu wengi," aliiambia BBC.
"Kumbuka, hili ni bara changa sana," alisema na kuongeza kuwa Afrika inahitaji kizazi kipya cha viongozi.
Ruto mwenye miaka 58, alifanya kampeni mwaka jana kama mgombea kwa ajili ya kizazi cha vijana dhidi ya kiongozi wa upinzani Raila Odinga mwenye umri wa miaka 78, Malema mwenye umri wa miaka 42 ameonekana kuwa na nafasi nzuri ya kueleza wasiwasi wa kundi hilo kubwa la wapiga kura yaani vijana.
Hata kabla ya maandamano ya nchi nne mwezi Machi, Malema alikuwa mtu mashuhuri mwenye wafuasi wengi nchini Kenya, hasa kutokana na michango yake katika bunge la Afrika Kusini, ambako wanasiasa wenzake wa chama cha Economic Freedom Fighters wanajulikana kwa kuvaa kofia nyekundu, kutoa hotuba kali na mara kwa mara kuvuruga vikao vya bunge.
Kwa hivyo, Malema alipotua Kenya, wasikilizaji walikuwa wanamsubiri.
Malema na Raila
Ndekwe anasema Malema anatoa changamoto si kwa Rais Ruto pekee bali pia kwa wapinzani wenzake.
"Kwa baadhi ya Wakenya, Malema anatazamwa kama kiongozi wa upinzani ambaye hakuna mfano wake. Malema ni kijana, mwenye juhudi, shupavu na asiye na woga, anawasilisha mawazo yake ingawa yanaweza kuwaudhi wengine, vijana hawaoni sifa hizi kwa Raila."
"Hotuba ya Rais wa Kenya ilirudia ahadi zile zile ambazo serikali imezitoa hapo awali, Malema alitoa sauti mbadala, akiikashifu serikali. Ni mazungumzo mazuri badala ya yale yale ya kawaida," anasema mhariri mmoja nchini Kenya ambaye hakutaka jina lake kutajwa.
Serikali ya Kenya Yakasirika
Haistaajabishi serikali ya Kenya kujibu kwa hasira maoni ya Malema. Naibu Rais Rigathi Gachagua amempa ushauri huu: "Tungependa kutoa wito kwa wageni kuheshimu viongozi wa nchi zinazowakaribisha. Tunasafiri ng'ambo na hatutukani viongozi wa nchi hizo wala hatuingilii siasa zao.
"Huyu mtu aliyekuja hapa anajua kila kitu. Alionekana kujua zaidi kuhusu Kenya kuliko sisi. Nilitembelea nchi yake Disemba na wana pata umeme wa mgao kwa saa saba; lakini hatujadili mambo hayo kwa sababu tunawaheshimu."
Serikali haikuwa pekee katika kumjibu Malema. Wakenya wengi wameona kauli zake ni za kuudhi, wakisema mgeni hafai kuwafundisha jinsi ya kuendesha mambo yao. Wengine walikerwa na uamuzi wake wa kutoa hotuba ya ukosoaji siku moja na Hotuba ya Rais kwa Taifa.
Kwanini Malema alialikwa?
"Chaguo hilo limetokana na mambo mengi ya msingi. Moja ni ni kwa sababu Malema amezungumza na anaendelea kuzungumzia kwa ujasiri masuala yanayolihusu Bara la Afrika, ikiwemo biashara huria barani Afrika, uhuru wa watu kusafiri ndani ya Afrika, na Waafrika wasimamie mambo yao,’’ anasema Prof Lumumba
"Malema wa Afrika Kusini pia anawakilisha kizazi kinachosema: "Unaposema tumeondoa ubaguzi wa rangi, ubaguzi wa rangi bado unaendelea." Na hilo linaendana na fikra zangu. Pia ni jasiri na anasema mambo haya bila kuogopa. wengi wetu tunatafuna maneno kwa sababu tunaogopa athari za kusema hayo."
"Kuna Wakenya walio kimya ambao wanahisi kukatishwa tamaa na kile kinachotokea na kile ambacho kimekuwa kikitokea katika ulingo wa siasa za Kenya, kwa ujumla Wakenya ni wengi ni wanafiki. Hawamaanishi wanachosema. Malema kama mgeni alikuja na kusema mambo ambayo tunatakiwa kuyasema, lakini hatuyasemi"
Licha ya Wakenya wengi kumuunga mkono Malema, nyumbani kwao Afrika Kusini ni mtu mwenye utata ambaye amekabiliwa na shutuma za kuchochea mivutano ya kirangi.
Amelaumiwa mara kwa mara kwa matamshi ya chuki, na kura za maoni zinaonyesha chama cha EFF kinashika nafasi ya tatu Afrika Kusini, na kinaungwa mkono na takribani 13% ya wapiga kura.
Huku mwanaume aliyevalia kofi nyekundu akiondoka Kenya, rais mwenye suti ya bluu ana kibarua kigumu cha kuungwa mkono tena na wale wanaotafuta suluhu ya matatizo yao ya kiuchumi na kisiasa kutoka nje badala ya ndani.