Julius Malema - Ana ushawishi kiasi gani katika siasa Afrika kusini

Huenda Julius Malema asiweze kuondosha sifa ya "hamasa kubwa" anayatazamwa kuwa nayo , lakini kiongozi huyo wa chama cha pili kwa ukubwa cha upinzani Afrika kusini mwenye umri wa miaka 38, hatazamwi tu kama mwanasiasa mwenye ghadhabu.

"Mwana wa kiasili", kama anavyotambulika na wafuasi wa chama chake cha Economic Freedom Fighters (EFF), amekigueza chama chake kwa muda wa miaka 6 iliyopita, kuwa kikosi chenye nidhamu kilichoweka ajenda katika maeneo kadhaa ya sera.

Alitimuliwa kutoka chama tawala cha ANC mnamo 2012, Malema, au "Juju" kama anavyoitwa wakati mwingine amekiweka EFF katika nafasi ya kuwa mrithi wa ajenda kali ya ANC na amefichua mapengo ya chama hicho tawala.

Lengo la kiongozi huyo mkuu wa EFF kuhusu ukosefu wa usawa nchini Afrika kusini, na kushindwa kwa ANC kuirudisha ardhi kutoka kwa jamii ndogo ya watu weupe kwenda kwa idadi kubwa ya watu weusi nchini, kumekigharimu uungwaji mkono chama chake cha zamani ambacho kiliongoza vita dhidi ya ubaguzi wa rangi.

Chama cha EFF kilijinyakulia 6% pekee ya kura zilizopigwa mnamo 2014 katika awamu ya kwanza ya uchaguzi mkuu, lakini ushawishi wake unaonekana kuzidi nguvu takwimu hizo.

Wabunge 25 wanaoonekana kuvaa nguo nyekundu na kofia bungeni na mbinu ya kutimuka bungeni, na Malema kutoa mistari ya nukuu, inamaanisha yeye na chama chake amefanikiwa kuwavutia watu kwa wanayoyafanya.

Maneno ya chuki

Tangu kusimama mbele ya umma, amekabiliwa na mizozo, kuwatikisa au kuwaudhi watu tofauti kuanzia makundi ya kutetea haki za wanawake, wakulima wazungu na hata wakuu wake kisiasa.

Amepatikana na hatia mara mbili kwa kutumia maneno ya chuki - mnamo 2010 na 2011 - kwanza kwa kauli aliyotoa dhidi ya mwanamke aliyemtuhumu rais Jacob Zuma kwa ubakaji alafu kwa kuimba nyimbo "Shoot the Boer (Afrikaner)".

Lakini umri hauonekani kumbadili na wala pia elimu haimzui - kwa shahada ya heshima katika filosofia aliyohitimu mnamo 2017.

'Watoto wapenda kulia lia'

Akizungumza na wafuasi kuhusu suala la ardhi mnamo 2016 alionya: "ardhi itachukuliwa kwa namna yoyote ile.

"Hatutoi wito wa kuuawa kwa wazungu, angalau sio kwa sasa. Tunachotaka ni kuishi kwa amani katika ardhi, na hatustahili kumuomba mtu yoyote radhi kwa hilo."

Mnamo 2018 katika mahojino na shirika la utangazaji la Uturuki TRT World aliitetea kauli hiyo na kusema yoyote anayefikiria kuwa kauli hiyo ni sawa na mauji ya kimbari, ni 'mtoto anyependa kulia lia'.

Huenda ukavutiwa na:

Lakini wafuasi wake wanfurahia vibwagizo vyake na Malema anasalia kuwa msemaji wa hadhara ambaye lengo lake la kutetea haki za raia maskini weusi Afrika kusini limemfanya kupendwa na wengi.

Kutokana na hilo, umaarufu wa EFF umeongezeka. Mnamo 2016 katika uchaguzi wa manispaa, chama hicho kimejinyakulia 8% ya kura ya kitaifa.

Alizaliwa mnamo 1981, Malema alilelewa na mamake Flora, mfanyakazi wa nyumbani, katika mtaa wa Seshego katika jimbo la kaskazini la Limpopo.

Anasema alijiunga na tawi la vijana la ANC akiwa na umri wa miaka 9, aliko pokea mafunzo ya kijeshi, na ilimchukua miaka mitano kuchaguliwa kuwa kiongozi wa kieneo wa tawi la vijana la chama hicho cha ANC.

Mambo 7 kuhusu Julius Malema

  • Alizaliwa Machi 3 mnamo 1981 katika jimbo la Limpopo: mamake alikuwa mfanyakazi wa nyumbani na ni mzazi wa kipekee
  • Alipewa jina la utani "Juju"
  • Alitimuliwa ANC mnamo 2012 kwa kuzusha mgawanyiko katika chama
  • Alikizindua EFF mnamo 2013
  • Aliuza nyumba ya kifahari ambayo haijakamilika ujenzi kulipa deni la kodi mnamo 2013
  • Baada ya uchaguzi wa mnamo 2014 wabunge wote wa EFF walifika bungeni wakiwa wamevalia nguo za wachimba mgodi na mayaya
  • Apongezwa kwa kupunguza uzito wa mwili kati ya 2017-18

Alipata fursa katika vuguvugu la wanafunzi, kabla ya hatimaye kuwa kiongozi wa kitaifa wa kongamano la wanafunzi Afrika kusini mnamo 2001.

Lakini ni kutokana na kuchaguliwa kwake kama kiongozi wa tawi la vijana katika ANC mnamo 2008 ndiko kulikomfanya kuwa mshawishi katika siasa za kitaifa.

Hatua zake za kwanza kama kiongozi kumfanyia kampeni Zuma ili kuchukua madaraka - kwanza kama kiongozi wa ANC na baadaye kama rais - akiuambia umati kwamba anaweza 'kuua mtu kwa ajili ya Zuma'.

Suala la ardhi

Lakini uhusiano wa Malema na Zuma uliingia chachu muda mfupi baada ya kiongozi huyo wa zamani kuingia madarakani mnamo 2009. Malema alimtuhumu mshirika wake wa zamani kwa kupuuzia wapiga kura maskini waliomuingiza madarakani.

Na fikra ya kwamba ANC kimejitenga na ufuasi wake na maadili yake ni kilio anachoendelea nacho mpaka leo.

Katika ujumbe kwenye mazishi ya Winnie Madikizela-Mandela mwaka jana, mpambanaji wa kupinga ubaguzi wa rangi na aliyekuwa mkewe Nelson Mandela, Aligusia ombi lake marehemu kwamba Malema arudi katika chama cha ANC.

Akizungumza na maelfu ya watu mbele ya rais Cyril Ramaphosa na uongozi mzima wa ANC alisema: "Mama ulituambia ni lazima turudi ANC, tulikusikia. Lakini tunakwenda kwa ANC ipi? Kwa watu wale wale waliokusaliti?"

Linapokuja suala kuu la umiliki wa ardhi EFF kimeweka ajenda

Mnamo February mwaka jana, Malema alianzisha mjadala bungeni kuhusu mageuzi ya ardhi akisema: "Muda wa mapatano umemalizika; sasa ni wakati wa haki".

ANC kiliunga mkono hoja ya EFF wakati huo iliyotaka kubadili katiba kuruhusu serikali kuichukua ardhi pasi kulipa fidia. Rais Ramaphosa amesema suala hilo litashughulikiwa, na ANC kimekiri katika manifesto yake kwamba " suala la ardhi halijashughulikiwa ipasavyo".

Lakini Malema ameshutumiwa kwa kuwa mnafiki.

Mnamo 2013, mamlaka ya kodi nchini ilisema anadaiwa deni la kodi la zaidi ya $1m. Kumekuwa na maswali mengi kuhusu zilikotoka pesa hizo.

Ili kulipa deni la kodi hiyo, mwanasiasa huyo alilazimika kuuza nyumba yake ya kifahari ambayo haijakamilika ujenzi katika mtaa wa kifahari Johannesburg-Sandton.

Malema pia amekabiliwa na mashtaka ya udanganyifu na rushwa ambayo baada ya miaka mitatu, yalitupiliwa mbali mnamo 2015 kutokana na kucheleweshwa kwa muda mrefu kumshtaki, jaji aliamua.

Mashtaka hayo yanahusiana na kandarasi ya serikali lakini daima alikana mashtaka hayo na kusema ni ya kisiasa.

Lolote analorushiwa kiongozi huyo wa upinzani katika miaka kumi iliyopita - na yapo mengi tu - hayaja athiri mvuto wake.

Kura za kutafuta maoni zinaashiria kwamba chama kinaweza kupata angalau 10% ya kura katika uchaguzi, na kuhakikisha kwamba sauti ya Malema inaendelea kusikika kwa muda fulani ujao.