Maporomoko ya jaa la Kiteezi Uganda yangeweza kuepukika?

.
Muda wa kusoma: Dakika 5

Akijitahidi kuwa mkakamavu, mkusanyaji takataka Okuku Prince mwenye umri wa miaka 22 anakumbuka wakati mwili wa rafiki yake wa karibu ulipopatikana kwenye jaa kubwa la takataka katika jiji kuu la Uganda, Kampala.

Maporomoko ya ardhi katika jaa la Kiteezi Agosti mwaka jana yaliua watu 30, akiwemo rafiki yake Sanya Kezia.

"Nadhani baadhi ya watu bado wako chini ya jaa la takataka," aliambia BBC.

Wengi wao walijitafutia riziki kwa kuosha na kuuza vitu vyovyote vilivyotupwa walivyopata ambavyo bado vina thamani - chochote kuanzia nyavu za kuvulia samaki hadi chupa za plastiki na glasi, na vifaa vya zamani vya kielektroniki.

Mchezo wa kutupiana lawama ulianza baada ya kutokea kwa maporomoko ya ardhi kati ya halmashauri ya jiji la Kampala na serikali kuu kwa uzembe, huku baadhi ya waliofariki wakiwa bado chini ya tani za takataka bila kupewa heshima ya kuzikwa.

Wakati matrekta ya serikali hatimaye yalipochimba kuutoa mwili wa Kezia, ulikuwa na majeraha usoni mwa kijana huyo wa miaka 21.

Ilikuwa tukio la kutisha kwa rafiki yake kumuona akiwa amegubikwa na uchafu unaonuka na kuoza.

"Hatuko salama hapa. Isipokuwa [waboreshe] jaa hili, labda walisawazishe. Vinginevyo, watu hawako salama," amesema Bw Prince, ambaye kabla ya kuwa mzoaji taka alikuwa akisomea sheria katika Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Uganda.

Pia unaweza kusoma:
.

Chanzo cha picha, AFP

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Hakuweza kumudu ada ya masomo baada ya familia yake kuyumba kifedha, utaratibu wake wa kila siku sasa na kwenda kwenye maktaba ni mambo mawili tofauti.

Ukosefu wa ajira kwa vijana uko katika kiwango cha juu nchini Uganda, na kuna wengi kama Bw Prince ambao mara nyingi huhatarisha afya zao na kuacha ndoto zao ili kutafuta riziki.

"Mimi huja hapa kwenye jaa la takataka asubuhi, nakusanya mifuko ya nailoni, naichukua naiosha na kuiuza," amesema Bw Prince. "Ninapata shilingi 10,000 [sawa na $2.70 au £2.10] kwa siku."

Kuporomoka kwa jaa hilo kulimwacha katika dhiki zaidi ya kifedha kwa sababu alikuwa akijipatia riziki kutokana na jaa hilo - lakini alilazimika kuhama kwa usalama wake.

Nyumba za wengine pia ziliharibiwa wakati wa shughuli za uokoaji.

Pesa za fidia zimelipwa kwa familia za walioaga dunia, lakini si kwa karibu watu 200 waliopoteza makazi yao, mamlaka za eneo hilo zimekiri hilo kwa BBC.

Viongozi "wanasubiri uthathmini na ugawaji wa bajeti", anasema Dkt Sarah Karen Zalwango, mkuu mpya wa afya ya umma na mazingira katika Mamlaka ya Mji Mkuu wa Kampala (KCCA).

Wengine wanahoji kuwa kuporomoka kwa jaa la Kiteezi hakungeepukiki kwa sababu za msingi zilizopuuzwa.

"Huwezi kuwa na watu milioni nne, ukachukua taka zao zote zilizochanganywa - zinazoharibika na zisizoharibika - na kuzitupa kwenye eneo moja. Hapana, sivyo [tunavyopaswa] kufanya hivyo. Lakini tumekuwa tukifanya hivyo kwa zaidi ya miaka 20," Frank Muramuzi, mpangaji mipango mijini katika jiji la Kampala, anaiambia BBC.

Jaa la Kiteezi lilitengenezwa mwaka 1996, kwa ufadhili wa Benki ya Dunia, ili kutoa hifadhi moja kubwa ya taka ngumu zinazozalishwa mjini Kampala.

Lakini kwa sasa idadi ya watu katika jiji la Kampala imeongezeka.

Ndege wawindaji wanaweza kuonekana wakiruka juu.

.
Maelezo ya picha, Eneo kubwa la kutupa takataka la Kiteezi lina takriban miaka 30

Wakazi na wafanyabiashara wa jiji hilo husababisha wastani wa tani 2,500 za taka kila siku, nusu yake ikiishia katika maeneo mengine ya kutupa taka ya jiji - kubwa zaidi likiwa Kiteezi.

Lakini tatizo ni kwamba Kiteezi inakosa vifaa vya kuchakata, kuchambua na kuchomea vinavyohitajika katika maeneo ya kutupa takataka.

"Kwa kila safu ya takataka ikirundikana, tabaka za chini huwa dhaifu, haswa mchakato wa kuoza wa taka zilizotupwa na kusababisha joto kuongezeka," Bw Muramuzi anaeleza.

"Bila ya kuwepo kwa maeneo ya kutolea hewa, methani na gesi zingine husalia kuwa zimenaswa chini, na kuzidisha udhaifu wa muundo ulioshikiliwa."

Hata hivyo hili linaweza kurekebishwa kwa urahisi, anaongeza, mradi tu serikali ijitume katika ufuatiliaji na ukaguzi wa mara kwa mara wa kimazingira, kijamii na kiuchumi.

Kama hilo lingekuwepo, "maafa yaliyotokea Kiteezi yangeepukika," anasema.

Kwa hivyo, ikiwa suluhisho ni rahisi hivi, kwa nini halijatekelezwa?

Jibu linaonekana kuwa mchanganyiko wa mvutano wa madaraka na usimamizi mbaya wa kifedha.

Jukumu la mwisho la kuhakikisha Kampala ina "mazingira safi, na endelevu" ni la KCCA, lakini Meya Erias Lukwago, kutoka chama cha upinzani cha Forum for Democratic Change, anasema ofisi yake haina uwezo wa kuleta mabadiliko hayo.

"Msaada wote ambao tumekuwa tukipata ni kwa hisani ya washirika wa maendeleo na wafadhili kama vile Bill and Melinda Gates, GIZ, na WaterAid ... lakini uwezo wao ni mdogo sana," meya wa Kampala alisema hivi karibuni.

"Kama tungekuwa tunapata ufadhili wa kutosha kutoka kwa serikali kuu, tungekuwa mbali sana hivi sasa."

Serikali haijasema lolote ikiwa kama itatenga fedha kwa ajili ya jaa hilo kubwa zaidi katika mji mkuu wa Kampala.

.

Chanzo cha picha, AFP

James Bond Kunobere, afisa wa usimamizi wa taka ngumu katika jiji la Kampala, anakiri kwamba kuporomoka kwa jaa hilo mwaka jana kulikuwa ishara ya kile ambacho kinahitajika kufanywa.

Kwa sasa, mamlaka katika mji mkuu wa Uganda wanaandaa mipango ya kugeuza taka ngumu na kupunguza kurundikana kwa taka jijini humo.

Lakini wanataka umma kuchukua jukumu pia. Kwa sasa watu wanalipa kampuni moja kati ya saba za kibinafsi za taka zinazofanya kazi Kampala kukusanya takataka zao, lengo likiwa ni kuzitenga na kuwepo kwa mchakato wa kuzikuchakata tena.

"Hatujabadilisha mawazo ya wakazi ya kutenga taka," Bw Kunobere aliambia BBC.

"Ukizitenga, taka zitakwenda maeneo tofauti. Ukizichanganya, zote huenda sehemu moja – kwenye jaa."

Wataalamu wanasema mipango kama hii ni muhimu lakini sio suluhisho kwa matatizo makubwa ya kimuundo huko Kiteezi.

Soma zaidi:

Imefasiriwa na Asha Juma