Kwanini kuna shinikizo la kubadili majina ya barabara nchini Uganda?

f

Chanzo cha picha, SWAIBU IBRAHIM

    • Author, Na Swaibu Ibrahim
    • Nafasi, BBC Swahili, Kampala
  • Muda wa kusoma: Dakika 3

Mahakama Kuu nchini Uganda imeiagiza halmashauri ya jiji la Kampala kuanzisha mchakato wa kubadilisha majina ya baadhi ya barabara za mji huo, ambayo yanawaenzi waliokuwa maafisa katika utawala wa ukoloni wa Uingereza.

Uamuzi huu, wa Mahakama umetolewa baada ya mwanaharakati wa haki za kibinadamu nchini Uganda John Ssempebwa mnamo mwaka uliopita kuwasilisha malalamiko katika mahakama akidai kuwa hatua ya kuendelea kutumia majina ya viongozi wa zamani wa kikoloni katika baadhi ya barabara inakiuka heshima ya Uganda kama taifa huru.

Katika malalamiko yake, Ssempebwa aliifahamisha mahakama kuwa halmashauri ya mji bado inatumia majina ya baadhi ya wakoloni wakiwemo Fredrick Lugard ambaye alifahamika kwa kuendeleza sera mbaya za kikoloni nchini Uganda na barani Afrika.

Licha ya miaka 62 tangu Uganda kupata uhuru wake kutoka kwa Uingereza, barabara nyingi mjini Kampala bado zinatumia majina ya walikouwa viongozi wa kikoloni.

Mwaka 2020, zaidi ya watu 5,000 waliweka saini katika malalamiko yaliolenga kubadilisha majina ya baadhi ya barabara mjini Kampala, na baadye kuwasilishwa kwa spika wa bunge wakati huo Rebecca Kadaga.

Katika uamuzi wake, hakimu Musa Ssekaana ameagiza uongozi wa halmashauri kuanza mchakato wa kubadilisha majina ya baadhi ya bara bara ili kuashiria utajiri wa mila na utamaduni pamoja na historia pana ya Uganda, badala ya kuwaenzi waliokuwa viongozi wa utawala wa ukoloni wa Uingereza.

Lini shinikizo hili lilianza?

vc

Chanzo cha picha, SWAIBU IBRAHIM

Kwa muda mrefu wanaharakati wa haki za kibinadamu na watu mbali mbali nchini Uganda wamekuwa wakiongoza kampeni ya kubadilisha majina hayo ili kuondokana kabisa na kumbukumbu mbaya za utawala wa ukoloni wa Uingereza.

Mnamo mwaka 2019, wanaharakati waliomuomba Erias Lukwago meya wa mji wa Kampala kuuanzisha mchakato huo.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mwezi Juni tarehe 8, watu 5,786 waliweka saini katika malalamiko ya kushinikiza mchakato wa kubalisha majina, na kuwasilisha malalmiko hayo kwa spika wa bunge wa wakati huo, Bi Rebecca Kadaga na halamashauri ya jiji la Kampala.

Malalmiko hayo yalikuwa yakilenga kupiga jeki harakati za kuondokana na majina ya kikoloni kutoka kwenye barabara za mji wa Kampala na baadhi ya maeneo muhimu katika jamii nchini Uganda.

Mwaka 2021, Kadaga alimuandikia barua Waziri Mkuu wa Wakati huo bwana Ruhakana Rugunda kumuomba ashughulikie malalamiko hayo.

Tangu Juni 18 mwaka 1894 Uganda ilianza kuwa koloni ya Uingereza hadi Oktoba 9 mwaka 1962 ilipopata uhuru wake. Ndani ya kipindi hicho cha zaidi ya miaka baadhi ya viongozi wa utawala wa kikoloni wanashtumiwa kwa kutekeleza maovu dhidi ya Waganda.

Wanaharakati wa haki za kibinadamu na baadhi ya raia hivyo wanadai kuwa kutokana na madhila ya kikoloni, majina ya viongozi wao hayapaswi kuwa katika barabara za mji mkuu wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki

Maelezo zaidi:

Imehaririwa na Yusuph Mazimu