Kwanini mpango wa chanjo ya mifugo Kenya unapingwa vikali?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Wycliffe Muia, BBC News & Peter Mwai, BBC Verify
- Nafasi, Nairobi
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Mpango kabambe wa kutoa chanjo kwa mifugo yote nchini Kenya unatarajiwa kuanza wiki hii huku kukiwa na upinzani mkali kutoka kwa wafugaji ambao unasukumwa na madai ya kupotosha kuhusu chanjo hizo.
Haitawagharimu wakulima chochote kupata chanjo ya mifugo yao kwani serikali inasema inatekeleza muswada huo.
Lakini Robert Nkukuu, ambaye anafuga ng'ombe katika eneo la Mai Mahiu kaunti ya Nakuru, takribani kilomita 50 kaskazini-magharibi mwa mji mkuu, Nairobi, alielezea jinsi limekuwa suala la gumu tangu Rais William Ruto atangaze mpango huo Novemba mwaka jana.
"Ikiwa jamii hapa itafahamu kuwa unapendelea chanjo itakuua sasa hivi. Kwa hivyo acha kuizungumzia, hatutaki," aliiambia BBC.
Lengo la serikali ni kuchanja takribani ng'ombe milioni 22 na mbuzi na kondoo milioni 50 katika kipindi cha miaka mitatu.
Hivi sasa ni 10% tu ya mifugo ya kitaifa inayopata chanjo zinazohitajika na mamlaka inasema wanataka kuongeza kiwango hicho hadi 85% ili kufanya mazao ya mifugo ya Kenya kustahili kuuzwa nje ya nchi.
Rais, ambaye ni mmiliki wa shamba na ana mifugo mingi mwenyewe, amesema chanjo hizo ni muhimu kwa kupanua sekta hiyo kwa kudhibiti ugonjwa wa midomo na miguu kwa ng'ombe na peste des petits ruminants (PPR), pia hujulikana kama tauni ya kondoo na mbuzi.
Lakini baadhi ya wale wanaopinga mpango huo wanaamini mwanzilishi mwenza wa Microsoft Bill Gates anafadhili mpango huo, ikichochewa na watu kuchapisha video za mahojiano yaliyomshirikisha akizungumzia chanjo ya ng'ombe ili kudhibiti uondoaji wa methane.

Chanzo cha picha, AFP
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Methane inayotolewa na mifugo huchangia takribani 15% ya uzalishaji wa hewa chafu duniani kila mwaka, makadirio ya Umoja wa Mataifa yanaonesha. Ni gesi chafu baada ya hewa ya ukaa (CO2).
Jonathan Mueke, afisa mkuu katika wizara ya kilimo ya Kenya, amekanusha kuwa Gates anahusika katika mpango wa chanjo ya mifugo, akiongeza kuwa si bilionea wa Marekani na mfadhili au vyanzo vingine vya kigeni vilivyotoa ufadhili.
Lakini hii haijasimamisha nadharia za njama zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, mara nyingi na watu mashuhuri.
Caleb Karuga, mwandishi wa habari wa zamani na sasa ni mkulima mwenye ushawishi mkubwa, alichapisha kwenye X kwamba angepinga chanjo hiyo, akisema hakuna mtu atakayechanja mifugo yake "kwa sababu Bill Gates alisema hivyo".
Ledama Olekina, Seneta wa upinzani na mfugaji maarufu, aliandika kwenye X: "Kuna mamilioni ya ng'ombe huko Uropa na Marekani na hakuna hata mmoja kati yao anayechanjwa kwa ajili ya kuzaa ...wangu hawatachanjwa."
Gates amewekeza hapo awali katika miradi ya kupunguza uzalishaji wa methane kutoka kwa ng'ombe na anafadhili kampuni ya Marekani inayopambana kutengeneza chanjo, kama ilivyo kwa wawekezaji wengine wa Marekani.
Lakini Prof Ermias Kebreab kutoka Chuo Kikuu cha California, Davis nchini Marekani, ambaye amefanya utafiti wa jinsi ya kupunguza utoaji wa methane kutoka kwa mifugo, aliiambia BBC kwa sasa hakuna chanjo ya mifugo kwa ajili ya kupunguza utoaji wa methane.
"Natamani tungekuwa na moja lakini bado inafanyiwa utafiti na hakuna mtu ambaye amefikia hatua ya kujaribiwa wanyama," alisema.
Hata hivyo, uhakikisho kama huo umefanya kidogo kuzima moto wa kutoelewana kuhusu nia ya kampeni ya chanjo.
Hata hivyo, uhakikisho kama huo umefanya kidogo kuzima kutoelewana kuhusu nia ya kampeni ya chanjo.
Kutokuwa na imani kunachochewa na baadhi ya wanasiasa wa upinzani, ambao wamesema chanjo hizo zitabadilisha maumbile ya mifugo, na hivyo kusababisha wanyama wenye kasoro.
"Ruto anaendeleza ajenda mbaya ya kigeni. Mpango huu ni wa kizembe na lazima ukomeshwe," alisema Kalonzo Musyoka, kiongozi wa upinzani, muda mfupi baada ya mpango huo kutangazwa.
Wakati BBC ilipomuuliza Musyoka kuhusu madai kwamba chanjo hizo zinaweza kuwa na madhara kwa ng'ombe, msemaji wake alisema kampeni ya chanjo hiyo ilikuwa "ukiukaji wa katiba".
Aliongeza kuwa "imegubikwa na usiri" na serikali haijaweka wazi maelezo kuhusu rasilimali, utekelezaji au maelezo ya kiufundi kuhusu chanjo.
Mapendekezo kwamba chanjo za mifugo zitabadilisha vinasaba vya wanyama ni ya kupotosha, kulingana na Profesa Ermias.
"Ni sawa na watu kupata chanjo ya kupambana na magonjwa mbalimbali. Hakuna ripoti kwamba husababisha ulemavu au kubadilisha DNA," msomi huyo aliiambia BBC.

Rais Ruto amepuuzilia mbali maoni ya wale wanaopinga chanjo hizo akisema ni "upotovu, usio na busara na labda wa kijinga".
"Sisi sote ambao tumechanjwa, kuna mtu ameacha kujamba?" Ruto alisema huku akipuuzilia mbali madai hayo ya methane kuwa "upuuzi".
Hata hivyo wadadisi wanasema kuenea kwa nadharia hizo za njama kunatokana na mawasiliano duni ya Ruto mwenyewe pamoja na imani ndogo kwa serikali yake kufuatia maandamano ya kupinga ushuru mwaka jana na msururu wa kashfa za ufisadi.
Serikali imekabiliwa na msukosuko mkubwa kuhusu nyongeza ya ushuru iliyoletwa tangu Ruto kuwa rais 2022 na kuifanya kutopendwa sana. Juni mwaka jana ililazimika kuondoa muswada wa fedha wenye utata ambao ungejumuisha ongezeko zaidi la kodi.
Alphonce Shiundu, mhariri wa Kenya katika shirika la kuangalia ukweli la AfricaCheck, anasema serikali sasa ilikuwa inakabiliwa na "upungufu wa uaminifu" kwa jinsi ilivyowasilisha kampeni ya ufugaji.
Ruto alipotangaza kwa mara ya kwanza, maelezo yalikuwa machache na haikujulikana ni nini wanyama gani hao wangechanjwa.
Hii ndio wakati zana zinazofuatilia machapisho ya mitandao ya kijamii kwenye X zinaonesha kuwa kulikuwa na ongezeko kubwa la kutajwa kwa Gates na ng'ombe kwa akaunti zilizoorodheshwa kama Kenya.
Hasira hiyo ilikua mjadala wa kitaifa, wachora vibonzo hata wakishinikiza haki za ng'ombe kwenye mitandao ya kijamii zikiwa na picha zilizoandikwa "My fart my choice".
Chama cha Madaktari wa Mifugo nchini (KVA) kimeitaka serikali kusitisha zoezi la utoaji chanjo na kufanya kampeni ya kuelimisha umma kwanza.
"Kufanywa kuwa siasa kwa zoezi la chanjo kumeathiri vibaya kampeni nzima, na hivyo kuukengeusha umma kutoka kwa lengo la kudhibiti magonjwa," Dk Kelvin Osore, mwenyekiti wa KVA, aliiambia BBC.
Lakini Dk Allan Azegele, mkurugenzi wa huduma za mifugo katika wizara ya kilimo, alisema haiwezi kucheleweshwa kutokana na mlipuko mkubwa wa ugonjwa wa hivi karibuni wa miguu na mdomo katika maeneo ya magharibi.
Hii imelazimisha masoko kadhaa ya mifugo kufungwa mwezi huu na viongozi wameweka hatua kali za kuwekewa dhamana katika maeneo hayo.
"Hatuwezi kusubiri... kwa sababu ni ghali zaidi kukabiliana na milipuko. Inabidi tuchukue hatua badala ya kuchukua hatua," Dk Azegele aliiambia BBC.
Alisema ugonjwa wa mguu na mdomo haukuwa na matibabu maalum, na kufanya hatua ya kuzuia kwa kutumia chanjo kuwa muhimu.

Waziri wa Kilimo Mutahi Kagwe amejaribu kumhakikishia kila mtu kuwa zoezi hilo litakuwa la hiari na ameahidi kuwashirikisha wadau wote "kuondoa habari potofu" inayohusu suala hilo.
Serikali pia imekuwa ikiwahakikishia Umma kuwa chanjo hizo zinazalishwa hapa nchini.
Lakini baadhi ya wafugaji bado wanaapa kupinga mpango wa chanjo, wakitaja uwezekano wa ushawishi wa kigeni na kutoiamini serikali.
David Tiriki, mfugaji katika kaunti ya Kajiado, kusini mwa Nairobi, aliiambia BBC kuwa hataruhusu wanyama wake kuchanjwa, akitaja hofu ya usalama.
"Ninashuku kuna mtu anajaribu kuingiza virusi kwenye mifugo yetu ili matajiri waanze kuuza dawa hiyo kwa wafugaji masikini ambao hata hawawezi kumudu," alisema.
BBC ilizungumza na mfugaji mmoja mdogo kutoka kaunti ya Makueni, kusini-mashariki mwa Nairobi, ambaye aliunga mkono mpango huo.
Lakini Ngemu Musau aliitaka serikali kufanya mchakato mzima kuwa wazi zaidi.
"Nataka uhakikisho kuwa ng'ombe wangu watakuwa sawa baada ya chanjo," aliiambia BBC.
"Kuna haja kwa serikali kufanya kampeni kubwa za kuelimisha umma."
Imetafsiriwa na Lizzy Masinga na kuhaririwa na Ambia Hirsi












