Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kinachofuata ni kipi?Macho yote sasa katika mahakama ya Juu zaidi baada ya Odinga kukataa matokeo
Safari ya Wakenya kuacha nyuma mchakato mzima wa kumchagua rais mpya na kuendelea na Maisha ya kawaida imerefushwa sasa baada ya Raila Odinga kuyakataa matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi William Ruto .Odinga amesema anaelkea katika mahakama ya juu Zaidi kupinga matokeo hayo yaliyotangazwa na tume ya uchaguzi .
Ikiwa Bw Odinga, mgombeaji wa Chama cha Azimio la Umoja-One Kenya, atawasilisha rufaa ya kupinga matokeo katika Mahakama ya Juu zaidi.ombi hilo litasikizwa na jopo la majaji saba.
Majaji hao ni Jaji Mkuu Martha Koome, Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu, Mohamed Ibrahim, Smokin Wanjala, Njoki Ndung’u, Isaac Lenaola na William Ouko.
Majaji watatu kati ya saba walibatilisha uchaguzi wa Rais Uhuru Kenyatta mwaka wa 2017. Jaji Mkuu Koome na Jaji Ouko, walijiunga na Mahakama ya Juu Zaidi katikati ya mwaka wa 2021.
Siku saba tu za kuwasilisha rufaa
Mtu yeyote anayetaka kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais ana siku saba za kuwasilisha ombi baada ya tarehe ya kutangazwa kwa matokeo. Mahakama ya Juu, ambayo ina mamlaka ya pekee ya kusikiliza ombi la uchaguzi wa urais, inatakiwa kuamua ombi hilo ndani ya siku 14 kuanzia tarehe ya kuwasilishwa na uamuzi wake utakuwa wa mwisho.
Ikiwa hakuna ombi lililowasilishwa katika Mahakama ya Juu, Rais Mteule Willian Ruto na Naibu Rais Mteule Rigathi Gachagua wataapishwa Jumanne, Agosti 30 kinyume na Septemba 12 iwapo ombi litawasilishwa.
Ikiwa matokeo ya uchaguzi wa urais yatapingwa, kuapishwa kutafanyika siku ya saba kufuatia tarehe ambayo Mahakama ya Juu itatoa uamuzi wa kutangaza uchaguzi huo kuwa halali. Ikiwa Mahakama ya Juu itabatilisha matokeo ya urais jinsi yalivyofanyika 2017, uchaguzi mpya utafanyika ndani ya siku 60.
Shughuli za bunge zinaweza kuendelea?
Ndiyo, Bunge litafanya kikao chake cha kwanza licha ya ombi linaloendelea la kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais.
Katiba inataka kwamba wakati wowote Bunge jipya linapochaguliwa, Rais, kwa notisi katika gazeti la serikali, atateua mahali na tarehe ya kikao cha kwanza cha Bunge jipya, ambacho kitakuwa si zaidi ya siku 30 baada ya uchaguzi.
Hii ina maana kuwa Rais anayeondoka Kenyatta atalazimika kuitisha kikao cha kwanza cha Bunge la 13 kabla ya Septemba 9 iwapo ombi la uchaguzi litasalia.
Mara baada ya Bunge kuitishwa, wabunge 349 na maseneta 67 watachagua maspika wao wapya ambao wataapishwa na makarani husika. Mara baada ya kuapishwa, maspika watamuapisha kila mbunge. Mgombea kiti cha spika lazima aungwe mkono na angalau theluthi mbili au 233 kati ya wabunge 349 katika Bunge la Kitaifa.
Mmoja lazima aungwe mkono na thuluthi mbili au 45 kati ya maseneta 67 ili kuchaguliwa kuwa Spika wa Seneti.
Makabidhiano ya madaraka
Katiba inasema Rais atakabidhi vyombo vya madaraka kwa Rais mteule, lakini iko kimya ikiwa ni lazima awepo katika hafla hiyo.
Imekuwa desturi nchini Kenya kwa kiongozi anayeondoka madarakani kukabidhi vyombo vya dola kwa Rais ajaye.
Katiba inasema Rais mteule lazima aapishwe afisini na aidha Jaji Mkuu (CJ), au naibu wake wakati Jaji mkuu hawezi kuongoza hafla hiyo kwa sababu ya hali zisizoepukika.
Sherehe ya kuapishwa lazima ifanyike kati ya saa nne asubuhi na saa nane mchana
Rais anayemaliza muda wake atamkabidhi mrithi wake vyombo vya madaraka na mamlaka.
Katiba inaainisha vyombo vya mamlaka na mamlaka kuwa ni upanga na Katiba.
Wengi watangoja kuona ikiwa Bw Kenyatta atahudhuria hafla ya kuapishwa kwa Dkt Ruto akiwa amepinga kuwania kwake na kuunga mkono kinara wa upinzani Bw Odinga.
Serikali mpya itaanza kazi lini?
Hii inategemea ikiwa mzozo utahamia Mahakama ya Juu.
Hakuna muda wa kikatiba, lakini baada ya kuapishwa Rais mpya anatarajiwa kutaja Baraza lake la Mawaziri. Mnamo 2013, ilimchukua Rais Kenyatta wiki mbili kuwasilisha majina manne ya Baraza lake la Mawaziri lenye wanachama 18, ikionyesha aina ya mazungumzo, kusaka watu na kukaguliwa kabla ya uteuzi wao.
Katiba inasema Rais atateua na, kwa idhini ya Bunge, atateua Mawaziri.
Baada ya kupokea orodha ya waliopendekezwa, Bunge litakuwa na siku 21 za kuwahakiki, kuwaidhinisha au kuwakataa waliopendekezwa kwenye Baraza la Mawaziri. Ikiwa hakuna ombi lililowasilishwa kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais, Rais Mteule anatarajiwa kuunda serikali mpya baada ya siku 14 za kutangazwa kwa matokeo.
Ikiwa ombi la uchaguzi litawasilishwa, Rais Mteule atataja Baraza la Mawaziri baada ya Septemba 12 tofauti na Agosti 30 ikiwa hakuna ombi la kupinga matokeo ya kura.
Hili pia linaweza kuchelewa hadi baada ya siku 60 ikiwa Mahakama ya Juu itabatilisha tangazo la Dkt Ruto kuwa Rais Mteule.
Rais ‘kwa jina’ bila mamlaka?
Rais Kenyatta alipoteza mamlaka kadhaa mnamo Agosti 9 Wakenya walipoenda kwenye Uchaguzi Mkuu na akaingia katika awamu ya muda ya uongozi wa mpito .
Alipoteza mamlaka ya kuteua majaji wa mahakama kuu, kuteua afisa yeyote wa umma, kuteua, au kumfukuza kazi waziri, Katibu wa kudumu na maafisa wengine wa Serikali.
Rais anayemaliza muda wake hawezi kutumia mamlaka ya kuteua, au kumfukuza kamishna mkuu, balozi, au mwakilishi wa kidiplomasia au ubalozi.
Katiba pia inamnyima Bw Kenyatta uwezo wa huruma na yeye, kwa hivyo, hawezi kuwasamehe wafungwa.
Katiba pia inapunguza mamlaka ya Rais ya kutoa taadhima ya heshima kwa jina la wananchi na Jamhuri. Wakati wa awamu ya uongozi wa muda, Rais Mteule atapokea taarifa za usalama kutoka kwa Huduma ya Kitaifa ya Ujasusi, Vikosi vya Ulinzi vya Kenya na Huduma ya Kitaifa ya Polisi.
Kamati ya Makabidhiano ya Ofisi ya Rais, ambayo ndiyo inayoongoza mchakato wa mpito, inatakiwa pia ili kurahisisha mawasiliano kati ya Rais anayemaliza muda wake na Rais Mteule.
Ina jukumu la kuandaa usalama wa Rais mteule, vifaa na wafanyikazi muhimu kwa Rais mteule, kuratibu taarifa za Rais mteule na maafisa husika wa umma na kuandaa hafla ya kuapishwa.