Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je uchaguzi wa urais Kenya utarudiwa au ushindi wa William Ruto utaidhinishwa?
Na Yusuf Jumah
BBC Swahili
Ni swali ambali lipo katika ndimi za wengi nje na ndani ya Kenya -Je,mahakama ya juu itafanya uamuzi gani kuhusu kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais?
Baada ya wiki nzima ya kila upande kutoa maombi na mawasilisho mbele ya majaji saba wa mahakama hiyo ya juu zaidi ,ngoja ngoja ya siku 14 sasa inafika tamati kesho ,Jumatatu tarehe 5 .
Nchi imesalia tulivu, lakini chini chini kuna wasi wasi kuhusu athari za uamuzi utakaotolewa.
Wasi wasi wenyewe ni kuhusu kitakachofuata na uamuzi wenyewe utapokelewaje na pande husika za kisiasa?
Uchaguzi wa tarehe 9 Agosti ulikuwa wa ushindani mkali sana na matokeo yake yamezua mgawanyiko nchini .
Rais mpya iwapo atajulikana kesho ama baadaye atakuwa na kibarua kikubwa cha kwanza ,kuinganisha nchi.
Lakini ,kesi hii ya Raila Odinga na Martha Karua kupinga kutangazwa kwa William Ruto kama rais mtuele imekuaje mahakamani na uamuzi wake utakuwa na yapi kwa mustakabali wa Kenya?
Uamuzi wenyewe utakuwa na yapi mazito hasa kuhusu mwelekeo wa siasa za Kenya na demokrasia ya taifa hilo?
Jitihada za kuishawishi mahakama ya Juu
Mjadala umekuwa juu ya uamuzi unaoweza kutolewa na majaji katika kesi hiyo ya kupinga matokeo ya uchaguzi na wadadisi wamependekeza uwezekano wa moja kati ya hali hizi tatu .
Mahakama ya juu inaweza kuunga mkono uamuzi wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kwa kumtangaza William Ruto kuwa rais aliyechaguliwa kihalali, au inaweza kubatilisha matokeo ya uchaguzi huo na kuamuru marudio au uchaguzi mpya.
Hata hivyo kuna wachache ambao wanafikiri inaweza kukabidhi ushindi kwa muungano wa Azimio kwa kumtangaza Odinga kama mshindi .
Majaji walianza kwa kurahisisha kazi yao kwa kuandaa orodha ya masuala tisa ambayo yanafaa kuamualiwa .
Masuala hayo ndio yatakayobeba msingi wa uamuzi wao wa mwisho .
Bw Odinga, kiongozi wa upinzani ambaye alipoteza uchaguzi wake wa tano wa urais kwa kura chache, anadai kuwa uchaguzi huo uliibwa na ameiomba Mahakama ya Juu zaidi ama kubatilisha matokeo yaliyotangazwa na mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Agosti 15 na kuamuru kura ya marudio au kumtangaza mshindi.
Timu yake ya wanasheria iliteta mahakamani kwamba kulikuwa na wizi mkubwa wa kura, ikitaja tofauti fulani katika hesabu ya kura katika vituo vya kupigia kura na yale yaliyopitishwa kielektroniki hadi kituo cha kitaifa cha kujumlisha kura jijini Nairobi.
Bw Odinga pia alidai kuwa baadhi ya wageni, ikiwa ni pamoja na raia wa Venezuela waliokamatwa na raia wa Kenya wakiwa na vifaa vya uchaguzi wiki moja kabla ya uchaguzi, waliruhusiwa kufikia mfumo wa tume ya uchaguzi ili kuvuruga matokeo kwa kumpendelea Dkt Ruto.
Mawakili wanaomwakilisha rais mteule na tume ya uchaguzi walitetea IEBC na kuitaka mahakama kuadhinisha matokeo hayo, wakitaja baadhi ya madai katika ombi hilo kuwa "ya kubuni".
Iwapo wengi wa majaji watatupilia mbali malalamiko ya kiongozi wa upinzani na kuunga mkono matokeo yaliyotangazwa na tulme ya uchaguzi, rais mpya ataapishwa Septemba 13 kuchukua nafasi ya Uhuru Kenyatta.
Iwapo watabatilisha ushindi wa Dkt Ruto na kuamuru uchaguzi urudiwe, hata hivyo, Wakenya watangonja hadi Novemba ambapo rais mpya atachukua mamlaka.
Iwapo mahakama itakubali maombi ya Bw Odinga ya kutaka mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati afunguliwe mashtaka na kuzuiwa kuendesha uchaguzi wa marudio, muda wa mpito unaweza kurefushwa hata zaidi.Hatua hiyo itamfanya rais Uhuru Kenyatta kuendelea kusalia madarakani .
Mawakili wa Dkt Ruto, katika mawasilisho yao mbele ya majaji wa Mahakama ya Juu, walidokeza uwezekano wa kipindi cha mpito cha muda mrefu kutumbukiza nchi katika mzozo wa kikatiba, ikizingatiwa kuwa Rais Kenyatta kwa sasa anahudumu mamlaka yake ya muda akiwa na mamlaka finyu katika baadhi ya maamuzi muhimu ya kiutawala.
Makabidhiano yametiwa doa?
Kando na Tume ya IEBC kujipata imepakwa tope baada ya mgawanyiko kuzuka miongoni mwa makamishna wake ,taasisi nyingine muhimu ambayo imejipata katika hali ngumu ni Baraza la Taifa la Ushauri wa Usalama(NSAC) ambalo sasa litapambana kujirejeshea hadhi baada ya kutolewa madai mazito kuhusu wajibu wake katika kujaribu kushawishi mshindi wa uchaguzi wa urais .
Wajumbe wa Baraza la Kitaifa la Ushauri wa Usalama (NSAC), chombo kikuu cha usalama nchini kinachoongozwa na rais, wamelazimika kutuma wakili katika Mahakama ya Juu ili kukanusha madai kwamba walijaribu kumshinikiza Bw Chebukati amtangaze Bw Odinga mshindi.
Iwapo matokeo hayo yataidhinishwa, huenda wakajipata katika hali mbaya ya kutekeleza majukumu yao baada ya majina yao kuburuzwa kwenye kesi ya Mahakama ya Juu na timu za wanasheria za rais mteule na mwenyekiti wa IEBC.
Chini ya sheria na desturi za mpito wa mamlaka nchini Kenya, kamati hiyo, miongoni mwa mambo mengine, inatarajiwa kurahisisha mawasiliano kati ya rais anayeondoka na rais mteule na rais huyo pia awe anapokea taarifa za kijasusi.
Makamishna wanne waliopinga IEBC pia wanataka Mahakama ya Juu kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa urais kwa sababu hayakutimiza matakwa ya sheria.
Makamu mwenyekiti wa IEBC Juliana Cherera na makamishna Justus Nyang’aya, Irene Masit na Francis Wanderi waliambia mahakama kupitia mawakili wao kuwa walizuiliwa na Mwenyekiti Wafula Chebukati kuthibitisha na kujumlisha matokeo. Wakili mkuu Paul Muite, aliyewaakilisha makamishna hao wanne, alimshtumu Bw Chebukati kwa kuendesha tume hiyo kama ‘chombo ‘ cha mtu mmoja.
Hata hivyo, Ruto, IEBC na mawakili wa Chebukati walishikilia kuwa tume hiyo halimaanishi timu nzima ya makamishna, bali mwenyekiti na wafanyikazi wa kiufundi pekee.
Aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Prof Githu Muigai, ambaye anaongoza timu ya wanasheria wa tume ya uchaguzi, alisema kesi hiyo ilihusu ukweli na idadi, hata hivyo walalamishi wameleta madai mengine yasiyo na umuhimu.
"Walalamishi wamejaribu kubishana kila hoja nyingine isipokuwa nambari. Malalamiko hayo yanatoa madai mazito ya asili ya uhalifu. Yote hayo, bila hata chembe ya ushahidi, hasa inavyomhusu mheshimiwa Chebukati. Kukashifiwa kwa mwenyekiti huyu ni zaidi ya chochote tulichowahi kuwa nacho katika mahakama hii’ Prof Muigai alisema.
“Mwenyekiti anapotangaza matokeo kwa mfano yeye ndiye tume. Anasema kuwa sio michakato yote ya IEBC inayohitaji mkutano na upigaji kura.
Kamau Karori, wakili mkuu wa timu ya Dkt Ruto, aliongeza kuwa kuhusisha makamishna wote katika kujumlisha na kuhakiki kutamaanisha kuwa wote saba watahitajika kutekeleza shughuli sawa kwa nyadhifa zingine za uchaguzi.
Baada ya kuchunguza maombi hayo, Mahakama ya Juu zaidi ikiongozwa na Jaji Mkuu na rais wa Mahakama ya Juu Martha Koome ilipunguza madai na kadhia nyingi katika kesi nane za kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais wa Agosti 9 hadi masuala tisa, ambayo matokeo yake yataamua iwapo Ushindi wa Ruto utaidhinishwa.
Mahakama itatoa uamuzi kuhusu maagizo yatakayotolewa, ambayo huenda yakajumuisha kubatilisha uchaguzi huo na kuamuru tume ya uchaguzi kufanya uchaguzi mpya ndani ya siku 60, kuidhinisha ushindi wa Dkt Ruto au kufutilia mbali cheti alichopewa na kumpa Bw Odinga jinsi alivyoimba mahakama .
Seneta mteule wa Busia Okiya Omtata ameteta kuwa hakuna mgombeaji aliyefikia kiwango cha asilimia 50+1 ya kura kama alivyotangaza Bw Chebukati mnamo Agosti 15 .
"Kwa hivyo, haikuwa sahihi kwa mwenyekiti kujumlisha asilimia kwa kila chama hadi pointi mbili za desimali," Bw Omtatah alisema, akiongeza kwamba kwa kutoa kwamba mgombeaji atakayepata zaidi ya nusu ya kura zote zilizopigwa ndiye mshindi wa uchaguzi wa urais, Katiba haiachi nafasi ya kasoro yoyote.
Kulingana na maombi ya Bw Odinga, Mahakama ya Juu zaidi iliamuru kwamba kura zilizopigwa katika vituo 15 katika maeneo tofauti ya kaunti zichunguzwe na kuhesabiwa upya.
Jaji Mkuu Martha Koome, naibu wake Philomena Mwilu na Majaji Mohamed Ibrahim, Smokin Wanjala, Njoki Ndung’u, Isaac Lenaola na William Ouko mnamo Jumatatu waliagiza kwamba masanduku ya kura za urais kwa vituo teule vya kupigia kura yafunguliwe ili kukaguliwa, kuchunguzwa na kuhesabiwa upya. Majaji hao pia waliamuru fomu zenye makosa zilizotiwa saini na Mwenyekiti wa IEBC Chebukati zipewe walalamishi Khelef Khalifa, George Osewe, Ruth Mumbi, Grace Kamau, Raila Odinga na Martha Karua.
Hofu ya mgawanyiko zaidi nchini
Kuna hofu kwamba kwa njia yoyote ambayo uamuzi huo utafanywa kutakuwa na mgawanyiko mkubwa kijamii nchini Kenya na kudhoofisha sifa za nchi kama kielelezo cha demokrasia katika eneo hilo.Uchaguzi uliokamilika umeiacha nchi na makovu ambayo lazima yashughulikiwe bila kujali uamuzi ambao utatolewa na mahakama .
Uchaguzi wa marudio au mpya utakuja na tatizo jingine - ni nani atasimamia uchaguzi katika siku 60 ikiwa IEBC itafunguliwa mashtaka - na katika hali yake ya sasa ya kutokuwa umoja? Je, Mahakama itatoa zuio la kimuundo pale inaposimamia uchaguzi wenyewe? Je, wapinzani watakubali Chebukati kusimamia hili hata kwa usimamizi wa mahakama? Je, mchakato huu wenyewe unaweza kuzua ombi jingine la kupinga matokeo? Je, rais anaweza kusalia madaakani hadi kipindi cha Chebukati kama mwenyekiti kikamilike?
Athari za uamuzi wa Mahakama
Kurudiwa tena kwa uchaguzi kunahatarisha kuzua mvutano zaidi nchini. Tayari, kutokuwa na uhakika kumelaumiwa kwa kuporomoka kwa shilingi na kupanda kwa mfumuko wa bei za bidhaa .
Mfumuko wa bei ulifikia asilimia 8.5 wiki hii inayokamilika- kiwango cha juu zaidi katika miezi 62 - kutoka asilimia 8.3 mwezi Julai, kutokana na kupanda kwa bei za vyakula na mafuta.
Shilingi ya Kenya iliendelea kudhoofika, kwa kiasi fulani kutokana na mzozo wa uchaguzi wa urais. Kufikia Agosti 31, shilingi ilikuwa imeshuka kwa asilimia 0.03 hadi Ksh120.05 dhidi ya dola ya Marekani huku mahakama ya Juu ilipoanza kusikiliza mawasilisho ya walalamishi.
Akiba ya sarafu za kigeni ilikuwa imeshuka hadi $7.6 bilioni -sawa na miezi 4.39 ya malipo ya uagizaji - katika wiki inayoishia Agosti 25, kutoka $7.74 bilioni, sawa na miezi 4.46 ya bima ya uagizaji, wakati wa wiki inayoishia Julai 28.
Taifa linapongojea uamuzi huo wa mahakama ya juu ,kuna moja au mawili ambayo hayatafutika-kwanza ,ni hali ya ukomavu wa Kenya kama taifa linaloweza kutumia asasi zake za ndani kusuluhisha masuala makubwa ya kisiasa na kisheria ili kulinda demokrasia yake na pili mkondo wa siasa za nchi hautawahi kuwa sawa baada ya uamuzi wa hapo kesho .