Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
‘’Mutuombee…’’ majaji watoa wito huo wanapojitayarisha kutoa hukumu yao
Kusikilizwa kwa kesi ya kupinga matokeo ya urais kumekamilika Ijumaa huku Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu akitoa ombi la kuwaombea majaji wanaporejea kufanyia kazi kuandika na kutoa uamuzi wa kesi hiyo.
“Mutuombee tunapoanza awamu inayofuata.
Sio sehemu ngumu sana lakini inahitaji umakini wa hali ya juu na kwa sababu hiyo tunakuomba utuombee Mungu atusaidie tuendelee katika ari ile ile tuliyokuwa nayo katika mwaka mmoja uliopita na tuwe na utambuzi wa hali ya juu sana, tutarudisha kwa Kenya hukumu ambayo si tofauti na kile ambacho Wakenya wanatarajia,” Mwilu alisema.
Mwilu katika hotuba yake ya mwisho alifahamisha pande zote kwamba katika Mahakama ya Juu, wanafanya kazi kama timu na kwamba hakuna aliye na kura ya turufu.
“Kila siku, mahakama ilikuwa na msimamizi wa kuhakikisha unafuata unachostahili kufanya. Kama hukuona, leo nilikuwa nilikuwa msimamizi. Siku ambayo wengi walicheka, Dkt. Smokin Wanjala alikuwa msimamizi. Tunafanya kazi kama timu hapa, tunafafanua majukumu ili tusiongee kwa wakati mmoja. Hakuna hata mmoja wetu aliye na kura ya turufu lakini tunaye kiongozi wa timu,’’ alisema.
Mwilu alipongeza vyama kwa jinsi walivyoendesha shughuli zao.
‘’Kama kulikuwa na tabia mbaya, hatukuziona. Tunawakushukuru kwa kufanya kazi ndani ya muda uliowekwa na tuliowapa. Ikiwa uliona kupata shinikizo kwa sababu ya muda, jilaumu kwa sababu mulitupa siku 14 kufanya kile kinachopaswa kufanywa kwa mwaka mzima, kama ungetuuliza sisi. ”
Kwa upande wake, Jaji Mkuu Martha Koome aliiomba nchi iwaombee wanapotoa hukumu ambayo inakuza ‘’Katiba yetu na inakuza demokrasia yetu na kuleta maelewano nchini.’’
Kesi hiyo imeendelea kwa muda wa siku tatu huku mawakili wakiwasilisha hoja za kuunga mkono pingamizi zao na upande wa walioshtakiwa nao, wakijitetea.
Wakati wa kesi hiyo siku ya Ijumaa, mawakili wa walalamikaji walishutumu tume ya uchaguzi kwa kukosa kutii maagizo ya kufungua seva ili kuchunguzwa.
Mawakili wanaomwakilisha mwanasiasa mkongwe Raila Odinga waliitaka mahakama kubatilisha ushindi wa Rais mteule William Ruto, kwa madai kuwa kulikuwa na kasoro.
Katika majibu yao, mawakili wa walalamikiwa, ambao ni pamoja na Bw Ruto na tume ya uchaguzi, walijitetea wakiiomba mahakama kutupilia mbali kesi hiyo kwa sababu hakuna ushahidi uliotolewa kuthibitisha uchaguzi huo uliibiwa.
Kinachosalia sasa ni kusubiri uamuzi ambao unaweza kubadilisha hali ya kisiasa ya Kenya.
Sasa jukumu limesalia kwa majaji saba ambao sasa wanafanyia kazi kilichowasilishwa mbele yao kabla ya mahakama hiyo ya Juu Zaidi kutoa umauzi wake.
Hukumu itatolewa Jumatatu.
Iwapo Mahakama ya Juu itaidhinisha uchaguzi wa Ruto, ataapishwa Septemba 13.
Na iwapo uchaguzi huo utabatilishwa, Wakenya watalazimika kurejea kwenye uchaguzi ndani ya siku 60.