Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

‘Maafisa wa IEBC waliharakisha tangazo la mshindi wa uchaguzi wa Urais kwasababu walihofia usalama wao’ - Wakili wa IEBC

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kupitia wakili wake George Murugu imesema kuwa ilitangaza kwa 'haraka' matokeo ya Urais kufuatia wasiwasi wa usalama wa wafanyikazi wake.

Moja kwa moja

  1. Maafisa wa polisi wajiandaa huku mahakama ya juu ikitarajiwa kutoa uamuzi Jumatatu

    Wakuu wote wa polisi katika mikoa na kaunti wametakiwa kujiandaa kwa matukio yoyote yanayoweza kutokea kutokana na uamuzi wa Mahakama ya Juu utakaotolewa Jumatatu, Septemba 5.

    Kulingana na taarifa ya gazeti la The Standard, naibu Inspekta Jenerali Edward Mbugua amewaandikia wakuu wa usalama akiwataka wawe macho na kuandaa maagizo ya jinsi ya kukabiliana na matokeo ya uamuzi wa mahakama.

    Katika barua hiyo ya tarehe mosi Septemba, Mbugua pia aliwataka maafisa wa usalama kupeleka nakala za mpango wao wa utekelezaji kwa makao makuu ya huduma ya Polisi ya Kenya usiku ya Ijumaa.

    "Kulingana na uamuzi wa mahakama ya juu , tunatarajia matukio mbalimbali kutoka kwa wananchi kama vile vurugu na uharibifu wa mali. Mnaelekezwa kuandaa maagizo ya operesheni ya jinsi ya kukabiliana na athari hizo ,” barua hiyo ilisema kama ilivyonukuliwa na gazeti la The standard.

    Haya yanajiri saa chache baada ya onyo lililotolewa na ubalozi wa Marekani jijini Nairobi kwa raia wake wanaosafiri kwenda katika Kaunti ya Kisumu kabla ya uamuzi wa Jumatatu.

  2. ‘Maafisa wa IEBC waliharakisha tangazo la mshindi wa uchaguzi wa Urais kwasababu walihofia usalama wao’ - Wakili wa IEBC

    Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kupitia wakili wake George Murugu imesema kuwa ilitangaza kwa 'haraka' matokeo ya Urais kufuatia wasiwasi wa usalama wa wafanyikazi wake.

    Alisema tume hiyo ilifanya uamuzi wa kutotangaza majimbo 27 yaliyosalia licha ya kujumlishwa na kuthibitishwa.

    Alisema matokeo yalikuwa tayari kwa kutangazwa na Profesa Abdi Guliye lakini kutokana na tishio lililokuwa likijitokeza, walichagua kutangaza matokeo ya urais pekee.

    Murugu aliongeza kuwa unyanyasaji wa mara kwa mara ambao wafanyakazi wa tume hiyo walikuwa wakikabiliana nao ambao ni pamoja na kukamatwa na vitisho ndio ulisababisha uamuzi huo.

    "Yeye [Chebukati] alizingatia kuhusu usalama wa wafanyikazi wake ambao wakati huo walikuwa wakikabiliwa na kukamatwa, kutekwa nyara na kujeruhiwa kwa maafisa wakiwemo makamishna," alisema.

    Bwana Murugu alikuwa akijibu swali kutoka kwa majaji wa mahakama ya juu kuhusu ni kwanini waliharakisha kutangaza matokeo bila kujumlisha matokeo mengine ambayo tayari yalikuwa yamethibitishwa.

  3. Nabii wa Uganda anayetuhumiwa kuwachapa viboko waumini akamatwa

    Mtu mmoja anayejiita nabii kutoka Uganda amefunguliwa mashtaka ya kushambulia na kusafirisha watu.

    Nabii Kintu Dennis wa Hoima Empowerment Church International alionekana kwenye video iliyosambazwa sana mtandaoni akiwachapa viboko waumini wa kanisa lake.

    Polisi walimkamata kijana huyo mwenye umri wa miaka 42 siku ya Jumatano wiki hii pamoja na waumini wengine wanne wa kanisa hilo kufuatia malalamiko kuhusu video hiyo.

    Amerekodi akiamuru viongozi wa kanisa kwenda mbele ya kanisa kuchapwa viboko au kuacha kuhudhuria maombi na kupoteza fursa ya kushika kipaza sauti chake.

    Wakati huo wote, kutaniko lilitazama wakati mmoja baada ya mwingine wahudumu wakichapwa huku muziki laini wa piano ukipigwa.

    Nabii Kintu aliwaambia wachunguzi kwamba alikuwa akifanya tu onesho la jinsi Yesu alivyowatendea wale aliowakuta wakiuza bidhaa kanisani, taarifa ya polisi ilisema.

    Mamlaka pia inadai kuwa alikuwa akifanya kazi kinyume cha sheria. Msako uliofanywa katika kanisa lake ulipata fimbo tatu ambazo polisi wanadai vilikuwa vikitumiwa kuwapiga waumini wa kutaniko lake.

    Alikuwa amezuiliwa hadi Septemba 7. Uganda ina makanisa kadhaa ya kiinjili yanayofanya kazi kote nchini.

    Hayadhibitiwi na mengi yanaendeshwa na wanaume na wanawake waliojiweka wakfu kwa Mungu.

    Unaweza kusoma:

  4. 'Iwapo Chebukati atashtakiwa, Uhuru ataendelea kuhudumu hadi rais mpya aapishwe'

    Wakili Willis Otieno alijibu maswali ya Mahakama ya Juu kuhusu iwapo kutakuwa na pengo iwapo mahakama ya juu itaamua kumfungulia mashtaka mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Wafula Chebukati.

    Kulingana na Otieno, Kifungu cha 142 cha Katiba kinasema kuwa Rais ambaye yuko madarakani anaendelea hadi atakapochaguliwa mpya.

    “Rais atashika madaraka yake kwa muhula unaoanza tarehe ambayo Rais aliapishwa, na kumalizika wakati mtu anayefuata aliyechaguliwa kuwa Rais kwa mujibu wa Ibara ya 136 (2) (a) anapoapishwa,” ibara ya 142 ya Katiba inasema.

    Kwa hakika, Katiba katika 142 (2) inaongeza kuwa mtu hatashika madaraka ya Rais kwa zaidi ya mihula miwili.

    Otieno alishikilia kuwa Chebukati hajazuiliwa kufa na anaweza kujiuzulu lakini hii haimaanishi kuwa Tume na uchaguzi bado hautaendeshwa nchini.

    "Mahakama hii haifai kukwepa iwapo itaona inafaa kumfungulia mashtaka Mwenyekiti Bw Chebukati kwa makosa na njia ya pekee ambayo ameshughulikia uchaguzi kwa madhara ya Wakenya," aliongezea.

  5. Watu wawili wahukumiwa kifungo baada ya kuua simba sita Uganda,

    Hakimu wa mahakama ya Buganda Road mjini Kampala Glayds Kamasanyu amewahukumu wanaume wawili miaka 8 na miezi saba baada ya kupatikana na hatia ya kuwaua simba sita kwa kuwatilia sumu.

    Akitoa hukumu hiyo alisema ushahidi uliotolewa umethibitisha wawili hao waliingia mbuga ya wanyama ya Queen Erizabeth iliyoko wilaya ya Kasese magaharibi mwa Uganda mwaka jana na kuwapatia sumu simba hao.

    Kwa mujibu wa hakimu Kamasanyu, mtu anayetenda makosa hayo anastahili kifungo cha maisha lakini kwa sababu washtakiwa walikiri kutenda mauaji ya simba hao 6, ili kupata fedha za kujikimu baada ya janga la Covid 19 ndiyo sababu wamepewa kifungo hicho.

    Msemaji wa Mamlaka ya wanyama pori nchini Uganda Bashir Hangi ameifahamisha BBC kuwa wamefurahishwa na hukumu iliyotolewa ili kuwa fundisho kwa watu wengine wanaofanya uwindaji haramu.

    Kwa pindi cha janga la covig19 mwaka 2020 hadi 2021 zaidi ya Simba 11 waliuawa na wawindaji haramu amesema Bashir Hangi.

    Kukiri kwao na pia ushahidi bayana ulithibitisha kuwa wao ndio waliwaua aina ya simba wa kipekee walio na sifa ya kupanda juu ya miti hasa katika vipindi vya jua kali.

    Simba hao ni adimu na wamo katika hatari ya kuangamia duniani kwani hupatikana tu tena kwa uchache katika mbuga fulani za Uganda, Tanzania, Kenya na Afrika Kusini. Ni kwa ajili hii ndipo simba hao ni kivutio kikubwa kwa watalii na hivyo kuwezesha nchi kuingiza kiasi kikubwa cha fedha za kigeni.

  6. Wakili wa Raila aonyesha fomu katika seva ya IEBC ilio na jina la raia wa Venezuela

    Wakili wa Raila aonyesha fomu katika seva ya IEBC ilio na jina la raia wa Venezuela

    Wakili wa mlalamishi Raila Odinga katika kesi anayopinga uchaguzi wa Rais Mteule William Ruto katika mahakama ya Juu Julie Soweto alionyesha moja kwa moja kanda ya video ilioonesha hitilafu kutoka kwa tovuti ya tume ya uchaguzi nchini Kenya IEBC..

    Wakati wa kusikilizwa kwa kesi ya kupinga uchaguzi wa urais, alitoa fomu katika tovuti hiyo kutoka Shule ya Msingi ya Gacharaigo katika Kaunti ya Murang’a iliyokuwa na jina la raia wa Venezuela Jose Camargo.

    "Mahali nilipo muhuri wa IEBC unaonekana umepachikwa juu ya muhuri mwingine. Tumeombwa tuonyeshe jinsi takwimu zinavyobadilishwa. Tukiangalia kura zilizopigwa, nambari ya kwanza ni ya Raila Odinga aliyepata 55, Ruto 260. , Mwaure 1 na Wajackoyah 0.

    Iwapo tutajumlisha jumla ya kura zilizopigwatunapata 316. Jumla ya kura zote zilizopigwa katika fomu hii ni 321, ikiwa ni tofauti na kile tulichoona. Hii ikimaanisha kwamba tayari hesabu hiyo ina makosa’’, alisema

    ‘’Tuliambiwa na bwana Eric Gumbo wakili wa IEBC kwamba hakukuwepo raia wa kigeni katika uchaguzi huu. Tuliambiwa kwamba hawakuweza kuingilia seva za IEBC . Tazama Juu kushoto katika fomu hii kuna jina la Jose Camargo. Huyu ndiye mtu aliyefanya maamuzi ya uchaguzi huu. Je jina hili liliingiaje hapa?’’ , aliuliza

    Bi Soweto alihoji kwamba bwana Carmago ndiye aliyekuwa akiingilia fomu zote 34ª katika seva ya tume ya Uchaguzi ya IEBC.

    ‘’Ishara ya kuingilia fomu hizi iliwachwa. Kwa Neema ya Mungu , tulipata kitu . Hili hatukujifanyia. Hivi ndivyo mambo yalivyofanyika’’

    Hatahivyo akimjibu wakili Mahat Somane alisema alichokionyesha Julie Soweto mahakamani kwa jina Jose Carmago kilikuwa ni fomu ghushi ya 34A na sio fomu asilia.

    ''Kilichotokea ni kwamba PO alichukua picha ya fomu na kuiwasilisha kwa portal. Madai ya kwamba mtu anayeitwa Jose Carmago alijaribu kuingilia habari kwenye tovuti sio kweli'', alijibu.

  7. Myanmar: Aung San Suu Kyi ahukumiwa miaka 3 zaidi kwa 'udanganyifu wa uchaguzi'

    Mahakama inayosimamiwa na jeshi nchini Myanmar imemhukumu Aung San Suu Kyi kifungo cha miaka mitatu jela kwa tuhuma za udanganyifu katika uchaguzi, mawakili wake wameiambia BBC.

    Bi Suu Kyi - kiongozi wa zamani wa nchi hiyo - sasa amehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kwa makosa 11, huku mashtaka kadhaa yakisalia.

    Amekanusha mashtaka yote, na kesi hizo zimeshutumiwa na makundi ya kutetea haki za binadamu kama zile za kisiasa.

    Iwapo atapatikana na hatia kwa mashtaka yote, anaweza kufungwa jela kwa takriban miaka 200.

    Hukumu hiyo mpya ni pamoja na kazi ngumu, mawakili wake walisema. Mshindi huyo wa Tuzo ya Nobel mwenye umri wa miaka 77 ametumia muda wake mwingi kizuizini chini ya kizuizi cha nyumbani katika mji mkuu wa Nay Pyi Taw.

    Raia na vyombo vya habari havijapata fursa ya kusikiliza kesi za watu binafsi na jeshi limewazuia wanasheria wake kuzungumza na waandishi wa habari.

    Mahakama ilimpata na hatia ya kufanya udanganyifu katika uchaguzi mkuu wa Novemba 2020, ambao chama chake, National League for Democracy (NLD), kilishinda kwa wingi.

    Jeshi lilianzisha mapinduzi mwaka jana baada ya kudai kuwa kulikuwa na udanganyifu mkubwa wa wapiga kura katika kura hiyo, lakini waangalizi huru wa uchaguzi walisema kuwa uchaguzi huo "unawakilisha matakwa ya watu".

  8. Odinga macho kwenye runinga mawakili wakimtetea

    Mawakili wa mgombea aliyeshindwa katika uchaguzi wa urais wa Agosti 9 nchini Kenya wanapinga ombi lake la kupinga matokeo katika Mahakama ya Juu katika mji mkuu, Nairobi.

    Wameonyesha kanda za video zinazodai kuwa fomu za matokeo zilibadilishwa ili kumpendelea rais mteule WIlliam Ruto.

    Lakini madai haya yamekanushwa na mawakili wa Tume ya Uchaguzi na wale wa Bw Ruto.

    Majaji saba wa Mahakama ya Juu watamaliza kusikiliza kesi katika saa zijazo ili kuandika hukumu ambayo itatolewa wiki ijayo Jumatatu.

    Akaunti rasmi ya Twitter ya Bw Odinga imeshirikisha mtandaoni picha ya mwanasiasa huyo mkongwe wa Kenya akifuatilia shughuli za mahakama kwenye runinga.

  9. Ethiopia: Hofu huku makumi ya watu wakiuawa katika mashambulizi ya Oromia

    Wakazi wa magharibi mwa Ethiopia wanasema wanaishi kwa hofu kufuatia mashambulizi ambapo takriban watu 50 wanahofiwa kuuawa katika sehemu moja katika eneo la Oromia.

    Wakaazi wa eneo hilo wanasema vikosi vya usalama viliondoka eneo hilo hivi majuzi na wanawalaumu wanamgambo wa kundi la Fano kwa ghasia zilizotokea mapema wiki.

    Nyumba zilichomwa moto na mali kuporwa wakati wa mashambulio hayo. Mamlaka za eneo hilo bado hazijajibu ombi la BBC la kupata kauli yao.

    Wakati vita vya kikatili vya wenyewe kwa wenyewe vilipoanza upya kaskazini mwa nchi hiyo hivi majuzi baada ya kusitisha mapigano kwa miezi mitano, eneo la magharibi mwa Ethiopia limeendelea kukumbwa mashambulizi ya mara kwa mara ya vurugu.

    Maeneo mengine ya nchi pia yameendelea kukabiliwa na ghasia za mara kwa mara.

    Maelezo zaidi:

  10. Upinzani nchini Angola wawasilisha pingamizi la kisheria dhidi ya matokeo ya uchaguzi

    Chama kikuu cha upinzani nchini Angola, Unita, kinasema kuwa kimewasilisha pingamizi la kisheria dhidi ya matokeo ya uchaguzi wa wiki iliyopita.

    Chama tawala cha MPLA - ambacho kimekuwa madarakani tangu 1975 - kilitangazwa kuwa mshindi wa kura, ingawa kwa idadi ndogo.

    Afisa mkuu wa Unita, Faustino Mumbika, aliambia shirika la habari la Ufaransa kwamba malalamishi yaliwasilishwa kwa Tume ya Kitaifa ya Uchaguzi siku ya Alhamisi.

    Unita - ambayo ilipata matokeo yake bora zaidi ya uchaguzi - imesema uchaguzi huo ulikumbwa na dosari.

  11. Joe Biden asema 'ajenda ya Maga' inatishia demokrasia ya Marekani

    Wafuasi wa ajenda ya Donald Trump ya "Make America Great Again" (Maga) ni tishio kwa demokrasia, Rais Joe Biden amesema.

    "Viguvugu la Maga limedhamiria kurudisha nchi hii nyuma," alisema katika hotuba yake ya kwanza huko Pennsylvania.

    Kevin McCarthy wa chama cha Republican alijibu kuwa Bw Biden "alijeruhi vibaya roho ya Marekani".

    Hotuba hizo zinakuja miezi miwili kabla ya uchaguzi wa katikati ya muhula, ambao utaamua usawa wa madaraka huko Washington.

    Rais wa chama cha Democratic alitoa hotuba yake Alhamisi usiku kutoka Ukumbi wa Uhuru huko Philadelphia, ambapo Azimio la Uhuru wa Marekani lilitiwa saini.

    Akitumia mada yake ya kampeni ya 2020 kuwatia "moyo Wamarekani". Alisema hakuwa akiwashutumu Wamarekani wote milioni 74 waliompigia kura Bw Trump miaka miwili iliyopita.

    "Sio kila Republican, ama Warepublican wengi, ni Maga Republican," alisema. "Lakini hakuna swali," Bw Biden aliendelea kusema, "kwamba chama cha Republican leo kinaongozwa, kinaendeshwa na kutishwa na Donald Trump na Maga Republican, na hiyo ni tishio kwa nchi hii."

    Rais alisema wafuasi wa Trump walichukulia umati wa watu ambao walivamia Bunge la Marekani mwaka jana kama wazalendo badala ya waasi.

    "Kwa muda mrefu," aliendelea, "tulijiambia kwamba demokrasia ya Marekani imehakikishwa. Lakini sivyo. Tunapaswa kuitetea. Ilinde. Simameni kwa ajili hiyo. Kila mmoja wetu."

    Wakati wote wa hotuba hiyo mtu alisikika akipiga kelele na kupuliza pembe, kulingana na mwandishi wa BBC katika eneo la tukio.

  12. Angie Okutoyi asonga mbele hadi Fainali Nyingine ya Kimataifa ya wachezaji wawili

    Mchezaji tenisi anayetamba nchini Kenya Angela Okutoyi anatazamiwa kuwania fainali nyingine ya taji la wachezaji wawili baada ya kutinga fainali ya J1 Repentin pamoja na mshirika wake wa Poland Malwina Rowinska.

    Wawili hao walitinga fainali nchini Canada bila kutoa jasho baada ya wapinzani wao Wakanada Ellie Daniels na Alexia Jacobs kuamua kusafiri mapema kwa US Open.

    Michuano hiyo nchini Kanada ya maandalizi ya Junior US Open naye Okutoyi ambaye yuko kwenye Droo kuu huko Flashing Meadows anatarajiwa kusafiri baada ya fainali.

    Okutoyi na mwenzake wa Poland waliagwa katika raundi ya kwanza kabla ya kuwashinda wenzao wa Kanada Eliana Kook na Anna-Raphaelle Serghi 6-4, 6-2 katika raundi ya pili.

    Waliendelea msururu wa makali yao katika robo fainali ambapo waliwaduwaza Irina Balus na Nikola Daubnerova kutoka Slovakia kwa seti za moja kwa moja za 6-4, 6-4.

    Bingwa huyo wa Wimbledon Doubles mwenye umri wa miaka 18 hakuwa na bahati katika mashindnao ya mchezaji mmoja kwani alipoteza kwa Ela Nala Milic wa Slovakia 7-6, 6-4.

    Fainali itachezwa Ijumaa usiku na kisha atasafiri kwa US Open ambapo yeye ndiye yupo katika droo kuu huko Flushing Meadows.

  13. Ripoti ya Uchunguzi wa sumu ya Enyobeni : Inasema wahanga walikosa hewa

    Ripoti ya uchunguzi wa sumu kuhusiana na vifo vya vijana 21 wa Afrika Kusini katika baa eneo la East London mwezi Juni, unaonyesha kuwa walikosa hewa kutokana na msongamano wa watu, familia za wahanga zinasema.

    Vijana 21 walianguka na walipatikana wakiwa wamelala sakafuni katika kilabu cha pombe cha Enyobeni.

    Sasa, ndugu wanahoji kuaminika kwa ripoti hiyo na hawajaridhishwa nayo.

    Maafisa wamekuwa wakizungumza na familia za wahanga faraghani, wakisema ni siri.

    Maafisa wa wizara ya afya wamekataa kufichua sababu ya kifo, huku msemaji wa Wizara ya Afya ya jimbo la Eastern Cape, Siyanda Manana akisema ni nje ya "matarajio kwamba michakato itafuatia".

    Mhanga mwenye umri mdogo zaidi, ambaye alikuwa katika sherehe katika kilabu cha pombe kusherehekea kumalizika kwa mitihani ya nusu muhula, alikuwa na umri wa miaka 13 tu, na wengi miongoni mwao walikuwa chini ya umri wa miaka 18.

    Mmoja wa wale waliokuwepo katika eneo wakati wa mkasa huo awali aliiambia BBC kwamba eneo hilo lilikuwa limejaa watu kupita kiasi.

  14. Cristina Fernandez de Kirchner: Makamu wa rais wa Argentina aponea chupuchupu kuuawa

    Makamu wa rais wa Argentina ameponea chupuchupu kuuawa baada ya silaha ya mtu aliyekuwa na bunduki kukwama alipokuwa akimlenga.

    Cristina Fernandez de Kirchner alikuwa akiwasalimia wafuasi wake nje ya nyumba yake wakati mwanaume mmoja alipojitokeza kutoka kwa umati na kumnyooshea bunduki usoni.

    Rais Alberto Fernandez alisema bunduki hiyo ilikuwa na risasi tano lakini ilishindwa kufyatua ilipofyatuliwa.

    Bi de Kirchner yuko katikati ya kesi ya ufisadi na alikuwa akirejea kutoka mahakamani. Anakanusha mashitaka dhidi yake

    Polisi walisema mtu huyo , ambaye vyombo vya habari vya eneo hilo vilimtaja kuwa ni mwanaume mwenye umri wa miaka 35 wa Brazil, ametiwa mbaroni. Wanajaribu kuchunguza sababu za shambulio hilo.

    Akihutubia taifa Alhamisi usiku, Bw Fernandez alilaani mshambuliaji huyo na kusema jaribio la kumuua Bi de Kirchner lilikuwa mojawapo ya matukio makubwa zaidi tangu nchi hiyo irejee kwa demokrasia mwaka wa 1983.

    "Tunaweza kutokubaliana, tunaweza kuwa na kutoelewana kwa kina, lakini matamshi ya chuki hayawezi kufanyika kwa sababu yanazua vurugu na hakuna uwezekano wa kutokea kwa vurugu pamoja na demokrasia," Bw Fernandez alisema.

    Kanda zilizosambazwa kwenye vyombo vya habari vya ndani zilionyesha mwanaume huyo akilenga bunduki inchi moja kutoka kichwani mwake na akionekana kujaribu kumpiga risasi. Kisha anainamisha kichwa chake lakini hakuna risasi zilizopigwa.

  15. Putin hatahudhuria mazishi ya Gorbachev

    Rais wa Urusi Vladimir Putin hatahudhuria mazishi ya Mikhail Gorbachev, kiongozi wa mwisho wa Muungano wa Usovieti, Kremlin imethibitisha.

    Msemaji wa ofisi ya rais Dmitry Peskov amesema kwamba mpango wa kazi wa Putin hautamruhusu kuhudhuria hafla hiyo siku ya Jumamosi.

    Alisema kuwa kiongozi wa Urusi alitoa heshima zake za mwisho katika hospitali ya Moscow ambako Bw Gorbachev alifariki Jumanne, akiwa na umri wa miaka 91.

    Mageuzi ya Gorbachev yalisaidia kumaliza Vita Baridi, lakini alishuhudia kuvunjika kwa Muungano wa Usovieti, jambo ambalo Bw Putin alililalamikia.

    Katika mwaka 2005, Rais wa Urusi alisema kuwa kuvunjika kwa USSR kulikuwa "janga kubwa la siasa ya kieneo la karne ya 20’’

    Hatahivyo, katika rambi rambi zake alizozitoa kwa njia ya telegramu, Bw Putin aliandika ujumbe wa maridhiano zaidi, akimuelezea Gorbachev kama "mwanasiasa na kiongozi wa taifa ambaye alikuwa na athari kubwa katika historia ya dunia ".

    Alhamisi, Televisheni ya Urusi ilimuonyesha Bw Putin akiweka shada la maua mekundu ya waridi kando ya jeneza la Gorbachev katika hospitali ya Moscow Central Clinical

    Unaweza pia kusoma:

    • Gorbachev aliweka historia lakini alikuwa na 'mapenzi' na Magharibi: Urusi
    • Mikhail Gorbachev:Kiongozi wa Soviet aliyesaidia kumaliza Vita baridi
    • Kwa picha: Maisha ya kiongozi wa zamani wa Usovieti Mikhail Gorbachev
  16. Hujambo na karibu tena kwa matangazo yetu mubashara leo Ijumaa tarehe 02.09.2022