Maafisa wa polisi wajiandaa huku mahakama ya juu ikitarajiwa kutoa uamuzi Jumatatu

Chanzo cha picha, Getty Images
Wakuu wote wa polisi katika mikoa na kaunti wametakiwa kujiandaa kwa matukio yoyote yanayoweza kutokea kutokana na uamuzi wa Mahakama ya Juu utakaotolewa Jumatatu, Septemba 5.
Kulingana na taarifa ya gazeti la The Standard, naibu Inspekta Jenerali Edward Mbugua amewaandikia wakuu wa usalama akiwataka wawe macho na kuandaa maagizo ya jinsi ya kukabiliana na matokeo ya uamuzi wa mahakama.
Katika barua hiyo ya tarehe mosi Septemba, Mbugua pia aliwataka maafisa wa usalama kupeleka nakala za mpango wao wa utekelezaji kwa makao makuu ya huduma ya Polisi ya Kenya usiku ya Ijumaa.
"Kulingana na uamuzi wa mahakama ya juu , tunatarajia matukio mbalimbali kutoka kwa wananchi kama vile vurugu na uharibifu wa mali. Mnaelekezwa kuandaa maagizo ya operesheni ya jinsi ya kukabiliana na athari hizo ,” barua hiyo ilisema kama ilivyonukuliwa na gazeti la The standard.
Haya yanajiri saa chache baada ya onyo lililotolewa na ubalozi wa Marekani jijini Nairobi kwa raia wake wanaosafiri kwenda katika Kaunti ya Kisumu kabla ya uamuzi wa Jumatatu.












