Kwa nini China na Urusi zinapatanisha vita vya Israel na Palestina?

Muda wa kusoma: Dakika 7

Na Paula Rosas

BBC Spanish

Kwa muda mrefu China na Urusi zimekuwa zikiunga mkono juhudi za Palestina, Lakini katika miaka ya hivi karibuni, China na Urusi zimechukua jukumu jipya lisilo la kawaida: kupatanisha kati ya Israeli na Palestina katika vita vilivyoanza katika Ukanda wa Gaza karibu mwaka mmoja uliopita.

Mwezi Julai, makundi kadhaa ya Wapalestina, ikiwa ni pamoja na Hamas na Fatah, walikutana katika mji mkuu wa China Beijing kufikia makubaliano kwa lengo la kuunda "serikali ya mpito ya maridhiano ya kitaifa" ya kuongoza Ukanda wa Gaza baada ya vita kumalizika.

Na makundi hayo yalikutana katika mji mkuu wa Urusi Moscow mwezi Februari kutafuta makubaliano kama hayo.

China na Urusi zinadumisha uhusiano na nchi muhimu katika kanda hiyo, ikiwa ni pamoja na Iran, Syria na Uturuki. Tofauti na Marekani, ambayo inashindana kwa ajili ya kuongoza, China na Urusi hazilitambui Hamas kama kundi la kigaidi, kwa hivyo hazikuwa na tatizo katika kuwaalika kwenye mazungumzo hayo.

Je, hatua hizi zitazaa matunda yoyote? Wataalamu waliozungumza na BBC walisema kuwa haiwezekani.

Lakini kuna swali jingine muhimu ambalo wengi wanauliza: Je, China na Urusi zinatarajia kupata nini kutokana na hatua hizi?

Kuna malengo mawili makuu ya kuzingatia: kwanza, kuongeza ushawishi katika jumuiya ya kimataifa na kukabiliana na Marekani na ulimwengu wa Magharibi.

Kutoka Mao Zedong hadi Xi Jinping

Tangu kuanzishwa kwa Jamhuri ya Watu wa China mwaka 1949, China imekuwa ikiunga mkono juhudi za Palestina.

Mwenyekiti Mao Zedong, baba mwanzilishi wa China, aliiona Israel kama Taiwan: ngome ya ubeberu wa Magharibi, iliyojengwa kudhibiti vikosi ambavyo vinaweza kupinga utaratibu wa kimataifa ulioanzishwa na Marekani.

Ahmed Abudu, mtafiti katika, taasisi ya sera za kimataifa ya Uingereza, Chatham House, aliiambia BBC kuwa matamshi kama hayo ya kupinga ukoloni yalionyesha kuwa taifa hilo jipya la China "lilikuwa na hisia ya uzoefu wake katika mateso ya Wapalestina".

Lakini msaada wa China kwa Palestina haukuishia tu kwa maneno ya kejeli. Mwenyekiti Mao, ambaye aliunga mkono harakati za ukombozi duniani kote, pia alitoa silaha kwa shirika la ukombozi wa Palestina (PLO) na alikuwa na ushawishi mkubwa juu ya itikadi yake.

Hata hivyo, wakati Rais Deng Xiaoping alipoingia madarakani mwaka 1978 na kubadilisha sera ya uchumi wa China kwa kueneza kauli mbiu, "Ni fahari kupata utajiri," mabadiliko pia yalijitokeza katika sera ya kigeni ya China.

Ili kutekeleza maono ya uchumi wa soko la kijamaa, serikali ya China ilifungua ulimwengu kupitia mageuzi. Hii ilihitaji kuhama kutoka kwa itikadi hadi uhalisia katika mafanikio, na ikawa na hamu zaidi ya kupanua uhusiano wa kidiplomasia na dola kubwa na dola za kati ulimwenguni kote kuliko kusaidia watendaji wasio wa serikali.

Wakati huo huo, Abudu anaeleza kuwa hali ilibadilika tena wakati Rais Xi Jinping alipoingia madarakani mwaka 2012. Rais Xi alianza kuanzisha vipengele vya kiitikadi tena katika sera za kigeni, lakini kwa upande mwingine, pia anafanya kazi ili kukidhi maslahi ya vitendo ya China. Na mgogoro wa Israeli na Palestina ni mfano mzuri wa ufafanuzi huu.

Kutoka Stalin hadi Putin

Wakati huo huo, uhusiano kati ya Urusi na Palestina una mwanzo tofauti. Wakati Israel ilipotangazwa kuwa taifa mwaka 1948, Muungano wa Usovieti chini ya Joseph Stalin ulikuwa moja ya nchi za kwanza duniani kuitambua.

"Wakati huo, Israel ilikuwa nchi ya kijamaa, na nchi jirani (katika Mashariki ya Kati) ambazo bado zilionekana kama makoloni ya Ulaya," Mark Katz, profesa wa sayansi ya siasa katika chuo kikuu cha George Mason nchini Marekani, aliiambia BBC Idhaa ya Kihispania.

Lakini Israel haikuelekea kuwa taifa la kijamaa, na katikati ya miaka ya 1950, kiongozi wa Usovieti Nikita Khrushchev aliunga mkono utaifa wa Kiarabu.

"Sababu ya Palestina ilikuwa muhimu sana kwa Muungano wa Usovieti," Profesa Katz aliongeza, "kwasababu wakati Marekani iliiunga mkono Israeli, Muungano wa Usovieti uliiunga mkono Palestina, jambo ambalo liliongeza umaarufu wa Palestina kati ya nchi za Kiarabu."

Lakini wakati sababu ya Palestina ilikuwa suala la kanuni kwa Waarabu wengi, lilikuwa ni suala la urahisi kwa mamlaka ya Usovieti.

Msukumo wa China wa kupatanisha mzozo kati ya Israel na Palestina huenda ukahusiana zaidi na ushindani wake na Marekani na taswira inayotaka kuijenga katika jumuiya ya kimataifa, kutokana na hadhi yake mpya kama taifa kubwa duniani.

"China inataka jumuiya ya kimataifa kuiona kama nguvu ya busara na inayowajibika inayovutiwa na upatanishi na kujenga amani," Abudu alielezea.

Wakati huo huo, mamlaka ya China inajaribu "kutangaza utaratibu mbadala wa dunia wa utaratibu wa sasa unaoongozwa na Marekani," hasa miongoni mwa nchi za dunia ya tatu, ambazo nyingi zinaiunga mkono Palestina, alisema.

"China pia haina wazo la namna ya kuiunganisha Palestina au jinsi ya kutatua mzozo tata kati ya Palestina na Israel," Abudu ameongeza. "China haina jukumu kubwa katika kutatua mzozo huu."

Utaratibu mbadala wa Dunia

Wakati huo huo, China ni muuzaji mkubwa wa mafuta duniani, na nusu ya mafuta hayo inayanunua kutoka nchi za Mashariki ya Kati na Ghuba ya Uajemi.

Je, juhudi za China za kupatanisha mzozo kati ya Israel na Palestina zinahusishwa na maslahi ya kiuchumi? Abuu akasema: "Hapana."

"Nchi nyingi za Kiarabu zimerejesha uhusiano na Israel, na zile ambazo bado hazijafanya hivyo, kama Saudi Arabia, ziko tayari kufanya hivyo mara tu machafuko ya Gaza yatakapopungua. China inaelewa hili na haihusiani na masuala hayo mawili."

Kwa maneno mengine, maelezo ni kwamba hakuna nchi itakayoacha kusafirisha mafuta kwenda China kwasababu ya msimamo wa China juu ya mzozo huu.

Kuondoa tahadhari ya vita nchini Ukraine

Wakati huo huo, Profesa Katz anaeleza kuwa kwa Urusi, mgogoro kati ya Hamas na Israel umekuwa muhimu sana katika kugeuza ufuatiliaji wa jumuiya ya kimataifa wa vita nchini Ukraine.

Kwakweli, sio tu kwamba habari kuhusu vita nchini Ukraine kwa kiasi kikubwa zimesogezwa nyuma tangu Oktoba 7 mwaka jana, lakini pia baadhi ya silaha ambazo washirika wa Ukraine, hasa Marekani, walikuwa wakipeleka Ukraine sasa zinaelekea Israeli.

Profesa Katz alisema, "Mamlaka za Urusi zinaona nchi za Magharibi kama zinatumia viwango viwili kwa kuishutumu Urusi kwa kuikalia Ukraine huku wakibaki kimya kuhusu kile Israel inachokifanya kwa Wapalestina."

Hamas, ambayo ilichukua udhibiti wa Ukanda wa Gaza mwaka 2007, sio mshirika wa Palestina anayependelewa na Urusi kutokana na itikadi yake ya Kiislamu, lakini hiyo haimaanishi kuwa Urusi haitashirikiana na kundi hilo au hata kuutumia uhusiano wake na kundi hilo.

Profesa Katz anaamini moja ya sababu ambazo Putin alighushi uhusiano na Hamas ni "kuizuia Hamas kuunga mkono makundi ya jihadi ndani ya Urusi, hasa Chechnya."

Na mkakati huo ulifanikiwa. Wakati wa uvamizi wa Urusi dhidi ya Georgia mwaka 2008, "wote Hamas na Hezbollah waliunga mkono msimamo wa Urusi juu ya Georgia, na kwa kiwango kidogo, hawakuunga mkono moja kwa moja sababu ya Waislamu ndani ya Urusi pia," anaelezea.

Hata hivyo, wataalamu wanaamini kwamba ingawa Urusi ina uhusiano na Hamas, haijatoa silaha kwa Hamas. Sababu moja ya hili, wanasema, ni kwamba Israeli haitaki kuhatarisha kutoa silaha sawa kwa Ukraine.

Abudu amesema jukumu la upatanishi wa Urusi ni sehemu ya juhudi za mataifa ya magharibi "kuepuka kutengwa kimataifa" kufuatia uvamizi wake nchini Ukraine, na kuongeza kuwa "inaonekana kuna baadhi ya mataifa ya Ghuba hasa ambayo yako tayari kuendelea kushirikiana na Urusi."

Sera na malengo tofauti

Wakati baadhi ya malengo ya China na Urusi yanaweza kuingiliana, hasa kudhoofisha ushawishi wa Marekani katika Mashariki ya Kati na Ulimwengu wa tatu, njia zao ni tofauti sana.

Kwanza kabisa, Urusi inaingilia kijeshi katika eneo hilo, kama ilivyofanya katika vita vya Syria, na China haina nia ya kufanya hivyo.

Abudu alisema China inataka kudumisha utaratibu wa kikanda katika Mashariki ya Kati, kuubadilisha kidogo ili kukidhi maslahi yake, wakati Urusi "inataka kuiharibu kabisa na kuijenga upya kutoka mwanzo kwa njia inayoinufaisha Urusi."

China imeongeza kuwa ina matumaini kuwa mzozo huo utatatuliwa kupitia kuundwa kwa taifa la Palestina ambalo linaweza kuwa na ushawishi mkubwa.

Urusi, kwa upande mwingine, inafikiria tofauti. Mtafiti Abudu anaamini kwamba Urusi haitaki kutatua mzozo kati ya Israel na Palestina, lakini inajifanya tu kutafuta suluhisho.

"Ikiwa mgogoro huu utatatuliwa, hakuna upande (Israel wala Palestina) utahitaji Urusi, na wote wawili watazingatia maendeleo ya kiuchumi. Kisha watalazimika kutegemea nchi za Magharibi, China, au zote mbili."

"Urusi inafaidika na ukosefu wa utulivu, lakini sio sana," Katz alihitimisha. "Wanataka sufuria ichemke, lakini hawataki ichemke."

Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi