Unajua ususi na mtindo wako wa nywele unaweza kukupa saratani?Utafiti mpya wabaini

Naomi braiding Ifeanyi's hair
Maelezo ya picha, Utafiti mpya umeibua wasiwasi kuhusu nywele bandia zinazotumiwa katika ususi.
    • Author, Chelsea Coates
    • Nafasi, BBC News
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Mitindo ya nywele ya kusuka kwa kuongezea nywele zingine bandia ama asili ni maarufu sana kwa wanawake weusi, ikiendelea kupendwa na watu mashuhuri na akina mama wa ukoo. Lakini sasa, maswali yanaibuka kuhusu athari zake kwa afya yetu.

Mchakato wa kusuka unaweza kuchukua hadi saa tano, ambapo watalamu wa nywele hugawanya sehemu ndogo za nywele kwa ustadi na kuziunganisha na nyongeza za nywele bandia.

Licha ya muda mrefu unaohitajika saluni, ususi umekuwa ukihusiana na urahisi kwa upande wangu.

Nilipokuwa mdogo, ususi ulikuwa kwa ajili ya likizo, kwani mtindo huu uliniwezesha kuogelea bila kuhofia nywele zangu kuvurugika.

Hadi sasa, mimi bado nachagua ususi ninapotaka kupumzika kwa miezi michache bila kusumbuka na kufumua nywele, au ninapotaka kujaribu rangi mpya bila kuhatarisha afya ya nywele zangu kwa kutumia rangi ya kudumu.

Chelsea

Chanzo cha picha, Chelsea Coates

Maelezo ya picha, Napenda aina hii ya kusuka kwenye, ni mtindo ninaopenda hasa kama nahudhuria hafla kubwa kubwa

Hata hivyo, utafiti mpya unaonyesha kuwa nywele bandia zinazotumiwa na wanawake wengi weusi zinaweza kuwa na madhara kwa afya zao.

Shirika lisilo la faida la Marekani, Consumer Reports, lilifanya majaribio kwa sampuli kutoka kwa aina 10 kumi maarufu za nywele bandia za kusuka na kugundua kuwa zote zilikuwa na kemikali zinazoweza kusababisha saratani, na nyingine zilikuwa na madini ya risasi.

Mara baada ya ripoti hiyo kuchapishwa, mitandao yangu ya kijamii na makundi ya WhatsApp yalijaa 'linki' za ripoti hiyo, zikionya kuhusu hatari zilizofichwa kwenye nywele zetu.

Ifeanyi's braids
Maelezo ya picha, Utafiti huo unasema nywele nyingi bandia zinaweza kuwa na kemikali zinazoweza kusababisha saratani

James Rogers, mkuu wa majaribio ya usalama wa bidhaa katika Kampuni ya Consumer Reports, alisema matokeo haya ni ya kutia hofu kwa sababu wanawake wanakuwa katika mgusano wa moja kwa moja na kemikali hizi hatari kwa muda mrefu wanapokuwa na nywele zao zilizofumwa na kusukwa vichwani mwao.

"Tunaamini kwamba kila unapokutana na kemikali hatari, madhara yake hujilimbikiza na huongezeka baada ya muda."

Hata hivyo, alisisitiza kuwa utafiti zaidi unahitajika, akisema: "Tunatumai hii itaanzisha mjadala, siyo tu katika ngazi ya udhibiti, bali pia ndani ya jamii zetu, kuhusu umuhimu wa kupata taarifa sahihi."

Abigail, Josee and Naomi stand outside the salon
Maelezo ya picha, Kwa karibu miaka 30, Josée (katikati) ameendesha saluni yake na binti zake Abigail (kushoto) na Naomi (kulia)

Josée na binti zake Abigail na Naomi, ambao wanafanya kazi naye saluni, wameona ongezeko la wateja wapya, hasa baada ya kusaidia kutengeneza nywele za wigi lililotumiwa na mhusika Elphaba katika filamu Wicked, moja ya filamu zenye mapato makubwa zaidi mwaka 2024.

Hata hivyo, baadhi ya wateja wao wameingiwa na wasiwasi.

Kwa Kellie-Ann, ambaye anasukwakwa mara ya kwanza katika saluni ya Josée, anasema ripoti hii imemshtua sana.

Kellie-Ann getting hair done
Maelezo ya picha, Kellie-Ann ameanza kutafuta chapa mbadala za nywele baada ya utafiti kutoka

"Naona ni mbaya kwamba makampuni yamekuwa yakitufanyia haya kwa miaka mingi. Tunastahili bora zaidi," anasema.

Kwa sasa, anatafuta chapa za nywele zisizo na kemikali hatari na plastiki, na anasema marafiki zake wengi pia wanafanya hivyo.

"Wanawake wengi niliowazungumzia wamekubaliana kuwa nywele zinazoweza kuharibika kiasili ni bora, pia ni nzuri kwa mazingira."

Ifeanyi in the hairdresser
Maelezo ya picha, Ifeanyi anataka kuona wadau wa tasnia ya nywele nyeusi wanajitolea zaidi kutengeneza bidhaa salama
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kwa upande mwingine, Ifeanyi, ambaye pia amekuwa akisuka nywele zake tangu utotoni, anasema ripoti hiyo haimtishi sana.

Anahoji kuwa watu huweza kukutana na kemikali hatari kila siku kupitia vyakula vilivyosindikwa, pombe, na sigara.

"Ni vyema kuwa waangalifu - lakini siamini kwamba tunapaswa kuachana kabisa na mtindo huu wa nywele."

Ana wasiwasi kuwa mijadala katika mitandao ya kijamii inaweza kuwafanya watu waogope kusukwa, jambo ambalo linaweza kuwa na athari mbaya kwa wafanyabiashara weusi katika sekta ya nywele.

Mwaka 2021, Treasure Tress, kampuni ya urembo ya Uingereza, iligundua kuwa wanawake wa Kizungu wa Uingereza walitumia £168 milioni kwa bidhaa za nywele kwa mwaka. Tafiti za awali za L'Oréal zilionyesha kuwa wanawake weusi nchini Uingereza hutumia mara sita zaidi ya gharama kwa ajili ya nywele zao ikilinganishwa na wanawake wengine.

"Ilikuwa bora kuona makampuni ikifanya juhudi kuhakikisha bidhaa zao ni salama kwa watumiaji, badala ya kutufanya tuhisi kuwa baadhi ya tamaduni zetu za asili ni mbaya," anasema Ifeanyi.

photo of Tendai Moyo at a conference

Chanzo cha picha, Tendai Moyo

Maelezo ya picha, Tendai Moyo founded Ruka during the pandemic

Kwa wengine, mabadiliko katika mtazamo kuhusu nywele bandia yanafungua milango kwa biashara mpya.

Tendai Moyo alianzisha kampuni yake inayouza nywele za asili kutoka Kusini-Mashariki mwa Asia mwaka 2021, ikiuza pia nywele bandia zinazoweza kuharibika kiasili, zilizotengenezwa kwa nyuzi za collagen.

Tangu kuchapishwa kwa utafiti huu, ameona ongezeko kubwa la mahitaji, hasa Marekani.

Lakini anasema hii ni sehemu ya muelekeo mpana, kwani tangu janga la COVID-19 litokee, watu wengi walijaribu mitindo mipya ya nywele wakiwa nyumbani.

Close-up of Kellie-Ann's hair being braided
Maelezo ya picha, Tendai anafikiri wanawake wengi zaidi waligeukia mitindo ya kusuka nywele za mitindo inayodumu muda mrefu

Hata hivyo, moja ya changamoto kubwa ni bei ya bidhaa mbadala.

Nywele za Kampuni yake zinagharimu mara 2.5 zaidi ya chapa za kawaida zinazopatikana madukani.

Ifeanyi anasema bei hizi si rahisi kwa wanafunzi kama yeye: "Unapotumia pesa kununua nywele hizi, ni sawa na gharama ya kusukwa, kwa hivyo unajikuta unalipa mara mbili."

Tendai anajitetea kwa kulinganisha na vyakula vyenye afya dhidi ya vyakula vyenye afya, akisisitiza kuwa bidhaa zake zinaweza kutumika tena, hivyo kusaidia kupunguza gharama kwa muda mrefu.

Naomi plaits Ifeanyi's hair
Maelezo ya picha, Naomi says her job empowers other women - and herself

Katika saluni ya Josée, Naomi anasisitiza kuwa ususi si kazi tu, bali ni utamaduni unaounganisha familia.

"Nimekuwa nikisuka tangu nilipokuwa na miaka sita," anasema huku mama yake akitabasamu kwa fahari.

"Ni kazi inayotupa nguvu," anaongeza, akisema kuwa ni heshima kufanya kazi inayowawezesha wanawake wengine kujisikia vizuri na wenye kujiamini.

Licha ya hofu inayoongezeka kuhusu athari za kiafya, ususi unabaki kuwa sehemu muhimu ya utamaduni wa wanawake weusi.

Kama Ifeanyi anavyosema: "Aina ya nywele tunazotumia zinaweza kubadilika, lakini utamaduni wa kusuka hautapotea."