Je, wasiwasi kuhusu Trump, ni fursa kwa China?

Muda wa kusoma: Dakika 5

Ikiwa China ina hasira na Marekani kwa kuweka ushuru wa ziada wa 10% kwa bidhaa za China, basi inafanya kazi kubwa kuificha hasira hizo.

Canada na Mexico ziliapa kulipiza kisasi na Waziri Mkuu wa Canada, Justin Trudeau alisema nchi yake "haitarudi nyuma" alipotangaza ushuru wa 25% kwa bidhaa za Marekani.

Rais wa Marekani Donald Trump kisha alikubali kusitisha kwa muda ushuru wa forodha kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka nchi zote mbili baada ya kufikia makubaliano nao. Hata hivyo, ushuru kwa China, unapangwa kuanza kutekelezwa Jumanne.

Mwaka 2018, wakati Trump alipozindua awamu ya kwanza kati ya nyingi za ushuru kwa bidhaa za China, Beijing ilitangaza "haiogopi vita vya Biashara."

Wakati huu, imetaka mazungumzo na Marekani. Na ripoti zinaonyesha mazungumzo ya simu kati ya Trump na Xi Jinping yanaweza kufanyika wiki hii.

Hii haimaanishi kuwa tangazo hilo litasimama. Litaendelea. Kwa sababu ushuru wa 10% ulioongezwa katika muhula wake wa kwanza kwa makumi ya bidhaa za China bado upo.

Na kimya cha China ni kwa sababu haitaki kuwatiwa hofu raia wake, wakati ambao wengi wao tayari wana wasiwasi juu ya athari za kiuchumi.

Lakini uchumi wa China hautegemei Marekani kama ilivyokuwa zamani. Beijing imeimarisha mikataba yake ya kibiashara barani Afrika, Amerika Kusini na Kusini Mashariki mwa Asia. Sasa ni mshirika mkubwa zaidi wa kibiashara wa zaidi ya nchi 120.

10% ya ziada ya ushuru inaweza isitoe faida ya kisiasa ambayo Trump anaitaka, anasema Chong Ja Ian kutoka Carnegie China.

"China inaamini inaweza kustahimili ushuru wa 10% - ndio sababu China iko kimya (kuliko Canada na Mexico). Hakuna sababu ya kuzozana na utawala wa Trump isipokuwa kuwe kuna faida ya kweli kwa Beijing."

Pia unaweza kusoma

Fursa kwa China?

Rais Xi Jinping pia anaweza kuwa na sababu nyingine: pengine ameona fursa.

Trump anazua mgawanyiko nyumbani kwake, na kutishia kuongeza ushuru hata kwa Umoja wa Ulaya (EU) katika mwezi wake wa kwanza ofisini. Hatua zake zinaweza kuwafanya washirika wengine wa Marekani kujiuliza, kipi kitawatokea.

Kinyume chake, China itataka kuonekana mshirika mtulivu, thabiti na pengine mwenye kuvutia zaidi kwa kibiashara za kimataifa.

"Sera ya Trump ya Marekani kwanza, italeta changamoto na vitisho kwa karibu nchi zote ulimwenguni," anasema Yun Sun, mkurugenzi wa masuala ya China katika Kituo cha Stimson.

"Kwa mtazamo wa ushindani wa Marekani na China, kuzorota kwa uaminifu wa Marekani kutainufaisha China."

Akiwa kiongozi wa nchi yenye uchumi wa pili kwa ukubwa duniani, Xi hajaficha nia yake ya China kuongoza ukuu wa dunia.

Tangu mwisho wa janga la Covid, amesafiri sana, na amezisaidia taasisi kuu za kimataifa kama vile Benki ya Dunia na mikataba ya tabia nchi ya Paris.

Vyombo vya habari vya serikali ya China vimeonyesha hilo kama kuzikumbatia nchi zote ulimwenguni na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia.

Kabla ya hapo, wakati Trump aliposimamisha ufadhili wa Marekani kwa WHO mwaka 2020, China iliahidi fedha za ziada. Matarajio ni makubwa kwamba Beijing inaweza kuingilia kati kujaza pengo la Marekani tena, kufuatia kujiondoa kwa Washington kutoka WHO. China inaweza kutaka kujaza pengo hilo, licha ya kuzorota kwa uchumi wake.

Katika siku yake ya kwanza baada ya kurejea ofisini, Trump alisimamisha misaada yote ya kigeni inayotolewa na Marekani, ndiye mfadhili mkuu zaidi wa misaada duniani. Ingawa baadhi ya misaada imerudi.

John Delury, mwanahistoria wa China na Profesa katika Chuo Kikuu cha Yonsei huko Seoul, anasema sera ya Trump ya 'Marekani Kwanza' inaweza kudhoofisha nafasi ya Washington kama kiongozi wa kimataifa.

"Kuongeza ushuru kwa washirika wakuu wa biashara na kufunga misaada ya kigeni, hutuma ujumbe kwamba Marekani haipendi ushirikiano wa kimataifa," anasema.

Katika azma yake ya kutaka ukuu wa kimataifa, Beijing imekuwa ikitafuta nafasi hiyo kwa miaka 50 iliyopita - na mashaka yanayoletwa na Trump yanaweza kusaidia kufanikisha hilo.

Washirika wapya

"Washirika wengi wa Marekani, hasa katika eneo la Pasifiki, wana sababu ya kufanya kazi na Beijing, lakini pia wana sababu za kuwa waangalifu. Ndiyo maana tumeona Japan, Korea Kusini, Ufilipino na Australia zikishirikiana zaidi kwa kiasi fulani kwa sababu ya hofu waliyonayo juu ya China."

Kuna uwezekano wa kuwepo kwa uhusiano wa pande tatu kati ya Australia, Japan na Korea Kusini, unaochochewa na "athari za utawala wa Trump," kulingana na Taasisi ya Masuala ya Kimataifa ya Australia.

Nchi zote tatu zina wasiwasi juu ya nguvu za China katika Bahari ya Kusini mwa China, pamoja na Ufilipino. Pia wana wasiwasi kuhusu uwezekano wa kutokea vita dhidi ya kisiwa kinachojitawala cha Taiwan.

Kwa muda mrefu Taiwan imekuwa mojawapo ya masuala yenye utata katika uhusiano wa Marekani na China, huku Beijing ikilaani uungwaji mkono wowote kutoka Washington kwa Taipei.

Lakini inaweza kuwa vigumu kwa Washington kujibu uchokozi wa China, ikiwa Trump anatishia mara kwa mara kuitwaa Canada au kuinunua Greenland.

Nchi nyingi za eneo hilo zimetumia uhusiano wao wa kijeshi na Washington kusawazisha uhusiano wao wa kiuchumi na China. Lakini kwa kuihofia Beijing na mashaka juu ya Marekani, wanaweza kuunda miungano mipya ya Asia, bila ya mataifa makubwa duniani.

Utulivu kabla ya dhoruba

Jibu la China limekuwa kimya zaidi kuliko Canada na Mexico tangu Trump atangaze ushuru. Wizara ya biashara ilitangaza mipango ya kuchukua hatua za kisheria na kutumia Shirika la Biashara Ulimwenguni kuwasilisha malalamiko yake.

Lakini kesi hiyo haina tishio kubwa kwa Washington. Mfumo wa utatuzi wa mizozo wa WTO umefungwa tangu 2019. Donald Trump, katika muhula wake wa kwanza wakati huo - alizuia uteuzi wa majaji kushughulikia rufaa.

Kwa sasa, China imesalia tulivu labda kwa matumaini ya kufanya makubaliano na Washington ili kuepusha ushuru zaidi na kuzuia uhusiano kati ya nchi hizo mbili zenye uchumi mkubwa zaidi duniani kuwa mbaya zaidi.

Lakini wengine wanaamini kuwa uhusiano mzuri hauwezi kudumu kwani Republican na Democrats, wote wanaiona China kama tishio kubwa kwa sera ya kigeni na kiuchumi.

"Kutotabirika kwa Trump, kukurupuka na uzembe wake bila shaka yatasababisha mshtuko mkubwa katika uhusiano wa nchi hizo mbili," anasema Wu Xinbo, profesa na mkurugenzi katika idara ya mafunzo juu ya masuala ya Marekani katika Chuo Kikuu cha Fudan.

"Zaidi ya hayo, timu yake ina watu wenye misimamo mikali, wana misimamo kuliko wale waliopo China. Ni jambo lisiloepukika kwamba uhusiano wa nchi hizo mbili utakabiliwa na misukosuko mikubwa katika miaka minne ijayo."

Kwa hakika China ina wasiwasi kuhusu uhusiano wake na Marekani na madhara ambayo vita vya kibiashara vinaweza kuyaleta kwa uchumi wake unaodorora.

Lakini pia itakuwa inatafuta njia za kutumia mvutano huo wa sasa, kuiweka jumuiya ya kimataifa katika njia yake na ndani ya ushawishi wake.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah